SEKTA ya utalii hapa nchini imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kutokana na kuwepo fursa mbalimbali za utalii.
Hata hivyo sekta hii muhimu na nyeti bado imeonekana kutothaminiwa na kupewa umuhimu katika kuhifadhi na kulinda rasilimali zilizopo katika hifadhi mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo kumekuwa na ujangili uliokithiri unaopelekea kutoweka kwa rasilimali katika hifadhi mbalimbali hapa nchini.
Miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo na mianya ya ujangili katika maeneo ya hifadhi ni pale serikali inapoamua kutoa vibali kwaajili ya biashara za wanyamapori na mimea.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia mianya hiyo kuwarubuni kwa kiasi kidogo cha fedha wananchi wanaoishi karibu na hifadhi ili waweze kuwaibia rasilimali hizo.
Kama serikali haitachukua hatua za makusudi za na haraka kudhibiti hali hiyo hiyo huenda rasilimali adimu kama wanyama na mimea ambayo inapatikana katika maeno ya Tanzania pekee duniani kote zikatoweka kabisa.
Katika hotuba ya waziri wa maliasili na utalii Ezekiel Maige wakati akiwasilisha Bungeni mkadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2011/2012, alisema kuwa kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, Wizara inaendelea na mchakato wa kuandaa Kanuni za kuwezesha utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi mwaka 2010-2015 ambapo pamoja na mambo mengine ilani imeagiza kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Utalii; kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira, upandaji miti na kukuza shughuli za ufugaji nyuki.
Aidha, Ilani inaitaka Wizara, kukuza utalii wa ndani na nje; kupanua wigo wa vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na utalii wa kihistoria, utamaduni, michezo na mazingira, Vilevile, Ilani inaitaka Wizara kuelekeza jitihada katika kuboresha huduma zinazotolewa katika Sekta ya Utalii.
Alisema Mwaka 2010/2011, Kanuni za maeneo matano zimekamilika na kuanza kutumika. Maeneo hayo yanahusu Uwindaji wa Kitalii; Uwindaji wa Wenyeji; Ukamataji Wanyamapori; Leseni ya Biashara ya Nyara.
Pia waziri huyo alisema Kanuni nyingine kwenye maeneo sita zitakamilishwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo Maeneo hayo ni: Uanzishaji na Usimamizi wa Mashamba, Bustani za wanyamapori; Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori; Matumizi ya Wanyamapori yasiyo ya uvunaji; Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo katika hatari ya kutoweka (CITES); Uchimbaji wa Madini katika Mapori ya Akiba na Maeneo Tengefu, na Utendaji kazi wa Kikosi Dhidi Ujangili.
Hata hivyo wananchi wengi waishio katika maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyamapori wamekuwa wakilalamikia utaratibu wa kutolewa kwa vibali vya biashara za wanyamapori na mimea kwani biashara hizo zimekuwa zikisababisha kuwepon na ujangili katika maeneo mengi ya hifadhi.
Mmoja wa wanakamati za mazingira katika hifadhi ya msitu wa kimboza uliopo kijiji cha mwarazi wilaya ya Morogoro Sania Kambi anaelezea masikitiko yake juu ya vibali hivyo vinavyotumika vibaya na kusababisha kutokuwepo na mahusiano mazuri baina ya wananchi hao na idara za maliasili.
“Mfano mzuri ni hapa katika kijiji hiki kinachozunguka hifadhi hii ya Kimboza, awali awali sisi kama kamati ya mazingira tulikuwa tunatunza msitu huu kwa kufanya doria na pia bhata kama wanakuja watalii tunawapokea na kuwapeleka katika msitu huu ambapo kama kijiji kilikuwa kinanufaika kwa kupata kiasi cha shilingi elfu 10 kwa siku” alisema
Alisema kuwa kwa sasa watalii hao hawapitii kwao na badala yake wanakuja moja kwa moja wanaingia kayika msitu huo kwa kibali cha kutoka moja kwa moja wilayani hali ambayo imesababisha wananchi hao kukata tamaa ya kufanya doria na hivyo kutelekeza msitu huo.
Alisema kuwa wanakijiji hao walitenga eneo na kujenga campu kwaajili ya kufikia watalii ambao waliweza kuingiza fedha sambamba na kuwapatia ajira pale wanapohitajika kuwahudumia ambapo kwa sas utaratibu huo haupo.
“Yaani kwa sasa unakuta watu wanakuja na vibali vyao vya kukata mbao au vya kuwindia sasa sisi kama wananchi tumekuwa tukifanya doria bila manufaa yeyote na kwamba tumeamua kuacha” alisema
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibungo ulipo msitu huo Musa Chande alisema kuwa awali wananchi wa eneo hilo walijitolea kulinda msitu huo kwa zamu wakiamini kuwa ni mali yao lakini utaratibu huo wa kutolewa vibali bila kuwashirikisha na pia kutokuwepo na kiasi cha fedha zinazobakia kijijini hapo imewakatisha tamaa.
Pia alisema kuwa mbali na hiyo takribani miaka minne sasa hakuna bwana miti yeyote katika hifadhi hiyo na hivyo msitu kuwa huru jambo linalowafanya hata majangili kuingia kiolela.
“Ushahidi wa kuwepo kwa majangili upo wazi kwani mapema mwaka huu alikamatwa mtu akiwa na mijusi 100 aina ya Mabalagaja kwa jina la kitaalam ni Gwencko williamsiis sasa huyo alikamatwa je ni wangapi wanaopita bila kukamatwa?” Alihoji mwenyekiti huyo.
Hata hivyo utafiti niliofanya juu ya bei halisi ya mijusi hiyo kutoka kijijini hapo nni shilingi 2000 hadi 3000 ambapo wafanyabiashara haramu nao wanauza mijusi hiyo nje kwa kiasi cha dola 100 hadi 150 kwa mjusi mmoja, ambapo kwa seti ya mijusi kwa maana ya jike na dume ni dola 200.
Mzee mohamed Hasan (72) ambaye ameishi katika kijiji hicho kwa miaka mingi alisema kuwa kwa sasa msitu huo umekuwa ukipoteza uasili wake siku hadi siku kutokana na uvamizi huo.
“Miaka 20 iliopita msitu huu ulikuwa huwezi kuingia hovyo, watu walikuwa wanakwenda katika msitu huo ndani katika maeneo maarufu kwaajili ya shughuli za kimila kama vile Choka la Hawi ambapo lilikuwa eneo la kuchomea watu wanaobainika kuwa ni wachawi.”
Alisema kuwa eneo lingine lilikuwa ni nyoka mkali eneo ambalo linamaji yenye nyoka ambaye anamanyoya kama kuku na pia kuna muda wake anawika kama kuku hivyo watu walikuwa wakienda kwaajili ya kufanya mila zao.
Alisema kuwa pia kulikuwa na eneo lililokuwa likiitwa pango la mjerumani ambalo hadi sasa baadhi ya watu wasio waaminifu wamekuwa wakidanganya kuwa kuna madini ya mekyuri jambo ambali si sahihi ila lilikuwa ni pango la Mjerumani pamoja na Dago la njiwa ambapo ni eneo ambalo wapo njiwa hadi sasa.
“Miti mingi ya asili kama vile mikongo, mivule, mikangazi mipilipili kwa sasa imetoweka kabisa kwa sababu ya uvunaji haramu ambao kwa siku za nyuma hakukua na utoaji wa vibali vya kuwinda wala kukata miti hiyo” alisisitiza
Aliongeza miaka hiyo hakukuwa na mtu anayeruhusiwa kuingia katika msitu huo na silaha kama kisu au panga na mtu akifanya hivyo alichukuliwa hatua na hivyo kulikuwa na siku maalumu ya kufanya usafi katika msitu huo ili kuepusha mioto.
“Kwa sasa msitu upo wazi miti mnayoiona ipo nje tu, zamani msitu huu ulifunga, kulikuwa na wanyama hata simba walikuwepo lakini sasa wanyama wote wanatoweka’’ alisema.
Afisa maliasili wilaya ya Morogoro Ande Malango alikiri kuwepo kwa uvamizi huo katika msitu huo wa hifadhi ya Kimboza na kudai kuwa ulizni ni hafifu katika hifadhi hiyo na kwamba hiyo inatokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha kudhibiti uharifu huo.
“Idara hii iko chini ya mkurugenzi na hapa mimi kama afisa maliasili sina gari , unakuta nikipata ya ujangili nashindwa kukimbia katika eneo la tukio hadi taratibu za kuomba gari, mafuta na dereva ambazo zinachukua muda na marab nyingine unakuta majangili wameshatoweka”.
Alisema kuwa rasimali kama mijusi hiyo na vinyonga ambavyo vipo katika msitu huo havipatikani duniani kote na kwamba wamekuwa ni rahisi kuibiwa kutokana na maumbile yake kwani ni rahisi kubeba.
“Mfano wale mijusi 100 waliweza kufungwa katika kimfuko kama cha mkate kilichotengenezwa na neti kama ya mbuu, sasa kama hakutakuwa na ulinzi wa kutosha bado majangili hawa wataendelea kuiba na kusababisha kupotea kwa rasilimali hizi’’ alisema
Alisema kuwa kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi za chini na kwamba watu wawe wanakagulkiwa hata katika pochi bila kudharau mtu.
Hata hivyo afisa huyo alidai kuwa sheria zinamapungufu na hivyo kusababisha majangili hao kutozwa faini ndogo ambapo wamekuwa wakidharau na kurudia vitendo hivyo.
Alisema kuwa kama kungekuwa na sheria za kuwabana majangili hao kulipa faini kubwa ingekuwa vigumu kuendela na biashara hizo haramu.
Ushauri wangu:
Ili kuweza kudhibiti hali hii ni lazima serikali ipitie upya sheria za wanyamapori na kuzifanyia marekebisho hasa katika adhabu pale mtu anapobainika kufanya ujangili.
Pia serikali ina kila sababu ya kudhibiti ujangili huo kwa kuweka ulinzi wa kutosha katika maeneo mbalimbali hasa katika viwanja vya ndege ili kukabilina na hali hiyo.
hapo nimekupata,ni vizuri sisi sote tukawa askari