WANASHIKA mabomba, kuta za hospitali, vitanda vya wagonjwa na kuwasalimia kwa mikono wagonjwa wao. Baada ya kushika na kutoka nje ya hospitali hawanawi mikono yao.
Hali hiyo nimeiona katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya, hospitali ya mkoa wa Rukwa na hospitali zingine hapa nchini wakati nafanya utafiti wa masuala ya afya ya uzazi mwaka 2012 na mwanzo wa mwaka 2013.
Baada ya kushuhudia hayo, nilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya madaktari kuhusu jambo hili ambao waliomba hifadhi ya majina yao.
Walisema kuwa huo wote ni uzembe wa viongozi wa hospitali husika.
Nikadodosa kuwa uzembe huo ni uzembe wa namna gani! Walisema uzebe huo unatokana na viongozi wa hospitali hizo kutoweka matangazo ya kuwataka wanaoona wagonjwa kunawa mikono yao baada ya kuingia na kutoka wodini.
Nilipojaribu kwenda mbali zaidi kutokana na niliyoyaona ambapo baadhi ya hospitali hazina bomba za maji nje ya hospitali au sehemu ya wazi, madaktari hao waliendelea kusema huo pia ni uzembe.
‘’Kuna sheria kabisa zinautaka uongozi kuhakikisha nje ya hospitali kuna kuwa na bomba la maji na katika maeneo yote kuwe na matangazo yanayowaelekeza wananchi kuwa wakitoka kuwaona wagonjwa wao au kutibiwa ni muhimu wanawe mikono yao’’ walisema kwa nyakati tofauti mdaktari hao.
Walisema kuwa sheria hiyo inautaka uongozi wa hospitali kununua sabuni na kuweka katika bomba za maji nje ya hospitali zote lakini haifuatiliwi kutokana na uzembe wa mamlaka za kuhoji kukaa kimya.
Walizitaja faida za kunawa mikono kwa sabuni baada ya kutoka kuwaona wagonjwa kuwa ni kupunguza baadhi ya magonjwa ya maambukizi.
‘’Mtu anapoingia hospitalini, anashika mabomba ambayo wagonjwa wameshika, anashika kuta na hata kusalimiana na wagonjwa hali ambayo inaweza kueneza magonjwa kirahisi kama sehemu hiyo iliyoshikwa kuna mgonjwa alishika na kuacha vimelea vya ugonjwa’’ alisema daktari mmoja wa hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Nini kifanyike? Majibu na uwezekano wa kufuata sheria hizo upo mikononi wa madaktari wa hospitali zetu nchini kwa kushirikiana na Wizara ya afya na usatwi wa jamii.