Uchakavu wa majengo kero kwa wahudumu wa afya Rufiji

Stella Mwaikusa

Wauguzi wa zahanati za Ndundunyikanza, Kipugira na Mtanza, zahanati zinazopatikana kata ya Kipugira wilaya ya Rufiji , wanalalamikia hali ya uchakavu wa nyumba zao, vyoo pamoja na majengo ya zahanati.

Shani Mopei muuguzi katika zahanati ya Kipugira anasema tangu alipofika katika zahanati hiyo mwaka 2004 hakuna ukarabati uliofanyika kwenye nyumba yake  na  zahanati ambayo imechakaa na kuleta muonekano mbaya na wasiwasi kuhusu  usalama wake na wagonjwa.

Anasema tayari zahanati ina nyufa sehemu mbalimbali, na ameshatoa taarifa mara nyingi lakini akasema viongozi wa wilaya wanatembelea hapa na kuona hali hii, lakini bado ukarabati haujafanyika.

kipugira

Naye muuguzi wa zahanati ya Mtanza, Fatma Mpakwaku anasema nyumba yake imechakaa, hata zahanati pia imekuwa ni nyumba ya popo kutokana na kuchakaa.

Anasema pamoja na kuchakaa kwa nyumba yake na zahanati, choo cha zahanati nacho kimeharibika na kuwafanya wagonjwa wanaofika hapo, kwenda kupata huduma   ya choo katika  shule ya msingi ambayo iko jirani na zahanati hiyo.

“Kama unavyoona choo kimejaa na hakina mlango,  hali hii imedumu kwa muda wa miezi sita sasa” anaeleza Fatma.

Dollo Victor mganga mkuu wa zahanati ya Ndundunyikanza anasema katika zahanati yake kuna tatizo la uchakavu wa vyoo, na kufanya hali inayowapa wakati mgumu wagonjwa wanaofika kuhudumiwa katika zahanati hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Rufiji Nurdin Babu, anasema anaelewa umhimu wa choo katika zahanati ila aliita hali hiyo kwamba ni moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *