Safari yangu kuelekea kijiji cha Nyaminywiri

Stella Mwaikusa

Safari yangu kuelekea Mkoa wa Pwani Wilaya ya Rufiji kata ya Kipugira katika kijiji cha Nyaminywiri, nikitokea Dar es salaam naweza kuiita ni safari ya tofauti si utofauti wa eneo ila ni namna nilivyoweza kusafiri.

Hii ina maana kwamba gari nililotumia wakati wa safari, barabara, watu niliosafiri nao  mazingira ya kwenye gari, na namna nilivyoingia kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Nyaminywiri, eneo ambalo ndio mahali hasa nilipokusudia kwenda, na kukaa kwa muda wa wiki mbili nikifanya kazi iliyonipeleka.

Nilianza safari yangu tarehe 1 oktoba 2012 asubuhi na mapema maana ni gari  moja tu ilikuwa inafanya safari zake kutoka Dar es salaam mpaka Mloka sehemu ambayo iko karibu na pori la hifadhi la Selou, ambapo  Nyaminywiri  ni kijiji kinachopitiwa  na gari hilo.

SAFARINI

Kutokana na ugeni niliokuwa nao sikukata tiketi mapema, nikiwa na imani kuwa nitapata usafiri kutokana na taarifa nilizokuwa nazo awali kwamba siku hizi usafiri wa kuelekea Lindi na Mtwara si tatizo.

Kumbe nilikuwa nimekosea sana kwani gari nililotakiwa kusafiri nalo haliendi njia ya Lindi, ila gari ikifika mji wa Kibiti mji ambao unapatikana katika wilaya ya Rufiji, linaelekea upande wa kulia barabara inayoelekea mji wa Mloka karibu kabisa na pori la  hifadhi ya Selou.

Kutokana na hali hiyo nikajikuta nakosa kiti kwa maana ya siti na kujikuta nasimama huku nikiwa nimebanwa sana kutokana na wingi wa watu waliokuwemo kwenye gari.

Lakini kama haitoshi kondakta wa gari hiyo alikuwa akisisitiza abiria wasogee nyuma ili nafasi ipatikane na abiria wengine waweze kuingia, lakini ukweli sehemu hiyo ya nyuma ambayo kondakta alikuwa akiisisitiza kulikuwa hakuna nafasi  na abiria wengi wakiishia kuingia kwenye gari na kujikuta wakikosa nafasi ya kuweka hata mguu.

Mwendo wa saa nne nikiwa nimesimama ndani ya gari nikafanikiwa kuona nje na niliona  mji uliochangamka watu wakifanya biashara mbalimbali, nilipokuwa katika hali ya kutaka kuuliza nikashtushwa na sauti ya kondakta,  “Kibiti hiyo kula ni dakika tano vinginevyo unaachwa”  

Nikajikuta natoa tabasamu dhaifu si kwa sababu nilikuwa nimefika Kibiti ila nikaona ni muda wa kupata hewa ya nje ambayo kwa kweli kwa mara ya kwanza katika maisha yangu niliona thamani ya hewa hiyo.

Faraja ilirejea niliposhuka kwenye gari baada ya kupokelewa na harufu  nzuri ya supu ya kuku wa kienyeji huku mamantilie wa eneo hilo wakiwa wamesimama kila mmoja akifanya juhudi ya kuhakikisha abiria au wateja wanaingia kwenye mgahawa wake.

Nikatamani kuagiza vipande vingi vya kuku ambapo paja na vipande vingine vikubwa vikiuzwa kwa shilingi 1000 lakini nikakumbuka sauti ya kondakta ikionya kwenye akili yangu ni dakika tano tu vinginevyo unaachwa!

Nikajikuta naagiza kipande kimoja ili niweze kumaliza haraka na kuwahi ndani ya gari, maana ukichelewa si kwamba utalikosa gari tu bali itakuwa ni vigumu kupita na kwenda sehemu yako ya awali kutokana na msongamano uliopo ndani ya gari.

Naweza kusema niliweza kumaliza supu ile ya kuku wa kienyeji na kuwahi ndani ya gari, safari hii nilisogea mwisho wa gari ili kuepuka usumbufu wa kusogezwa.

Kondakta ambaye hakuwa rafiki wa abiria hasa pale anapoona abiria wengine ambao hawajapanda bado, kwani alikuwa haamini kama gari yake inaweza kujaa huku akiwa bado anahitaji pesa ya abiria walioko chini.

Safari iliendelea na baada ya dakika kama  tano hivi tukaingia kwenye barabara ya vumbi, hali ambayo iliongeza adha ndani ya gari ile , ambapo yalizuka mabishano wengine wakitaka madirisha yafunguliwe ili vumbi likiingia ndani ya gari liweze kutoka huku wengine wakitaka madirisha yafungwe ili vumbi isiingie ndani.

Kabla sijafikiria nisaidie kundi gani kati ya makundi hayo mawili, nilishtuka baada ya kujikuta narushwa na gari na kujigonga  kwenye eneo la juu la gari hiyo kutokana na mashimo na michanga ya barabara hiyo  ya Dar es salaam kwenda Mloka.

Nikiwa na naugulia maumivu yale sikuona  kama kuna mtu yeyote aliyeonekana kushtushwa na hali ile pamoja na kwamba wapo wengine  walipatwa na maswahibu kama yangu.

Abiria walitulia kimya kama hakuna kilichotokea hali iliyonifanya na mimi nitulie maana waswahili wanasema ukiwakuta wenyeji wana chongo na wewe inabidi ung’oe jicho moja ili ufanane nao.

Nikiwa katika hali ile mara nikasikia sauti ya wanawake waliokaa viti vya mbele wakianza kupiga kelele, tushushe! tushushe bwana, wanaume wakimtaka dereva asimamishe gari.

Baada ya muda nikaelewa kelele zile zilitokana na nini kwani, gari tuliyokuwa tumepanda ilikuwa ikirudi nyuma baada ya kushindwa kupandisha mlima.

Akili yangu ilikuwa haijafikiri bado nini cha kufanya, nikajikuta nainamisha kichwa sikumbuki nilikuwa nawaza nini kwa muda ule, vilio vya akinamama vikizidi na wengine wakiendelea kuomba Mungu ili aweze kutunusuru na mabaya, au niseme lile gari liweze kusimama bila kuleta madhara.

Nilipojaribu kuchungulia eneo ambalo gari lile lilikuwa likielekea sikuweza kuona kitu kutokana vumbi kubwa lililokuwa linatimuka,  baada ya muda tukatingishwa kwa nguvu na hatimaye gari likasimama, lakini tulikuwa tumerudi nyuma kama kilometa moja hivi.

Kelele ziliendelea hasa za akinamama wakidai kushushwa lakini baadae dereva akapaza sauti na kuomba abiria wawe watulivu, kwani kilichotokea ni bahati mbaya na akaahidi hali ile haitatokea tena.

Bahati nzuri abiria wakamuelewa na safari ikaanza, lakini kabla gari haijaenda mbali ikaanza tena kurudi nyuma ambapo abiria wakaanza kumzonga dereva asimamishe gari ili washuke.

ajali-njiani

Naweza kusema Mungu alikuwa upande wetu kwani baada ya muda gari ile iliweza kusimama na abiria wakashuka wengi wakiwa ni akinamama, watoto na wanaume wachache huku idadi kubwa ya wanaume wakibaki ndani ya gari.

Tulilazimika kutembea umbali wa kilometa moja  huku gari ikipandisha taratibu ikiwa na abiria wachache ambao ni akina baba na vijana wa kiume, baada ya muda tukawa tayari tumeshapanda gari na safari ikaendelea.

Hali ya kujigonga na gari likiinamia upande mmoja iliendelea na kuifanya safari ile kuwa ya kipekee, kwani naweza kusema hakuna cha kufurahia katika safari ile.

Nilikuwa nimebeba camera sikuweza kupiga picha hata moja nikiwa ndani ya gari kutokana na wingi wa abiria na namna gari ilivyokuwa ikinesanesa kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Hali ile ilinilazimisha niulize kila baada ya dakika chache umbali uliobakia kabla ya kufika katika kijiji cha Nyaminywiri, ambapo jirani yangu alionekana kukerwa na maswali yangu na baadae akaniambia nitulie tukikaribia ataniambia.

Haikuwa karibu kama nilivyodhani kwani ni mwendo wa saa 4 kutoka  mji wa Kibiti kwa hiyo msomaji unaweza kupata picha hali ilikuwaje, kwa ujumla naweza kusema ni mwendo wa saa nane toka Dar es salaam mpaka Kijiji cha Nyaminywiri.

Nikiwa nimeanza kuizoea hali iliyokuwemo ndani ya gari mara namuona abiria aliyekuwa amekaa akimwambia kondakta amshushe kituo kinachofuata, nikafurahi kwamba angalau nitaweza kupumzika.

Mambo hayakuwa kama nilivyotarajia kumbe utaratibu wa watu wa maeneo yale abiria anayeshuka ndiye mwenye maamuzi ya nani atakaa kwenye kiti alichokuwa amekalia.

Nikajikuta naendelea kusimama na akaitwa abiria ambaye alionekana kufahamiana na yule  abiria aliyekuwa akishuka, ilinikera lakini sikuwa na namna  ya kufanya zaidi ya kutulia na kusubiri taarifa ya jirani yangu ambaye kwa muda ule ndiye aliyekuwa mwenyeji wangu ndani ya gari.

Taarifa nzuri masikioni mwangu kwa siku ile ni pale niliposikia sauti ya kondakta akiwataka abiria wanaoshuka vijiji vya Kipo, Kipugira na Nyaminywiri kusogea mbele kwani karibu tutafika maeneo hayo.

Japo ilikuwa ni taabu kupita kuelekea mbele ya gari lakini kwa upande wangu ilikuwa ni kazi rahisi ukilinganisha na adha iliyokuwepo mle ndani ya gari.

Hatimaye nikafika kijiji cha Nyaminywiri na kazi ikawa moja kudai tiketi yangu kitendo kilichoonekana kumkera kondakta na kuniona ni mtu wa ajabu, si umefika tiketi ya nini? aliuliza kondakta, maswali yake hayakunikatisha tamaa ya kupata kile nilichoamini ni haki yangu.

Baada ya kuendelea kudai tiketi yangu, ikasikika sauti ya jamaa mmoja toka ndani ya gari lile mwenye asili ya kiasia, mpe bwana asitucheleweshe huyo! Nikapewa tiketi yangu huku kondakta akiishia kusonya na gari ikaondoka, hiyo haikunipa taabu nikaiweka tiketi yangu kwenye mkoba huku nikiangazaangaza eneo lile.

Niliweka begi langu chini nikiwa nimebeba mkoba wangu, najiuliza sehemu ninayotakiwa kwenda kutokana na ukweli kwamba sikuwa na ndugu au mwenyeji wangu yeyote katika kijiji hicho cha Nyaminywiri, hali ilionyesha kwamba hakuna dalili ya kuwepo kwa nyumba za wageni katika kijiji hicho.

Nikiwa naangaza huku na kule nafanikiwa kuiona shule ya msingi nikajikuta naanza kuondoka na kuelekea shuleni lakini kitu ambacho nilikiona sio cha kawaida ni ile hali ya watu kuniangalia kwa kunishangaa hivi.

Baadae nikajua kwamba watu wa maeneo yale wote wanafahamiana kwa hiyo walipoiona sura ngeni wakawa na kiu ya kujua nimetokea wapi na nimefika pale  kufanya nini.

Nilifika shuleni ikiwa ni muda wa saa tisa na kupokelewa na mwalimu zamu wa siku hiyo aliyenitajia jina moja tu la  Mhinge.

Baada ya kumueleza nia na sababu ya mimi kuwa pale akaniambia yeye hawezi kufanya lolote akanipeleka kwa mwalimu mkuu, Ismail Kinyanguli ambaye aliweza kunipa mahali pa kulala baada ya kuridhika na maelezo yangu.

Chumba nilichopewa kulala kilikuwa kikitumiwa na wavulana ambao walihamishiwa chumba kingine na mimi nikapata nafasi ya kuweka mizigo yangu naweza kusema ni chumba cha kawaida ambacho paa lake likiwa limeliwa na mchwa.

Madirisha yakiwa hayana pazia yako wazi na mlango wa chumba unarudishwa tu hauna cha kufungia, kwa hiyo unapolala unatakiwa kuviringisha msumari ili usijibamize lakini mtu au mnyama anaingia bila shida.

Ilipofika jioni hofu iliniingia baada ya kugundua kwamba mlango wa nje yaani wa kuingilia ndani nao hauko imara  unarudishwa tu, huku nikiambiwa katika maeneo hayo kuna nguruwe pori ambao huzunguka  kwenye maeneo hayo wakati wa usiku kula korosho.

Uzalendo  ukanishinda ikabidi niongee na mwenyeji wangu anitafutie binti yeyote ambaye naweza kulala nae angalau nijue tuko wawili.

Kulipookucha safari yangu ilikuwa kwenda ng’ambo ya mto Rufiji ambako niliambiwa wakazi wengi wa kijiji hicho wanaishi, bahati nzuri mwenyeji wangu akanitafutia kijana ambaye atanipeleka huko,

Tulitumia mwendo wa saa moja kuufikia mto Rufiji, njiani tukikutana na watu mbalimbali ambao wametokea ng’ambo ya pili ambako tulikuwa tukielekea.

Tukapanda mtumbwi ambao tulilipia shilingi 100 kila mmoja hiyo ni nauli ya kwenda na kurudi, safari ilianza vizuri ila tulipofika katikati ya mto ndipo hali yangu ilipobadilika.

mto-rufiji-mtumbwi

Ni kwamba wenyeji wangu ambao ni abiria wenzangu waliniambia wanasikia harufu ya kiboko mtoto, na wanahisi mama yake atakuwa maeneo hayo.

Kawaida  ni kwamba kiboko anapokuwa na mtoto mdogo basi huona kila mtu au kitu kinachopita karibu na mwanae ni adui, na kinachotokea ni kwamba anapindua mtumbwi.

Habari ile haikuwa njema kwani pamoja na upepo mzuri uliokuwa ukipuliza nikajikuta navuja jasho kwa woga, lakini kwa bahati nzuri tukafika ng’ambo na kufanikiwa kufanya kazi iliyonipeleka.

Lakini wakati wa kurudi ikabidi nimuuliza kijana aliyenipeleka kujua  hali ya mto rufiji, ndipo akaniambia kwamba kuna mamba wengi na viboko ndani ya mto huo na kwamba tayari wameshaleta madhara  kwa wakazi wa kijiji hicho.

Akanikumbusha kijana mmoja ambaye tulipishana nae wakati tunaelekea ng’ambo akiwa hana mkono, kumbe aliliwa mkono huo na mamba alipokuwa akivua samaki.

Akaniambia hata wavuvi wa mto huo huvua wakiwa katika mitumbwi tofauti na maeneo mengine, na akaongeza kwamba mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi na watoto 9 wa shule ya msingi Nyaminywiri wakafariki dunia.

Habari zile hazikuwa njema ukizingatia kwamba naenda kuvuka tena kurudi eneo nililofikia yaani ng’ambo ya pili, bahati nzuri  tulivuka salama na kufika ng’ambo ya pili salama.

Nina mengi ya kusimulia kutokana na safari yangu ya Nyaminwiri lakini kwa leo ngoja niishie hapa ila naweza kusema nimepata uzoefu na kujifunza vitu vingi.

Japokuwa nilipokuwa ndani ya gari na mtumbwi nilipata wakati mgumu ila sasa naweza kusema safari yangu ya Nyaminwiri ilikuwa ya maana kubwa, yenye historia mpya katika maisha yangu.

Naishukuru Tanzania Media Fund (TMF) kwa kunipa nafasi ya kuyaona haya niliyoyaona na kujifunza mazingira tofauti ya kazi yangu ya uandishi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *