Utapiamlo wakithiri Wilayani Bunda, Mara

Mariam Mkumbaru

Zaidi ya watoto 294 wapo hatarini kupoteza maisha kwa kuumwa ugonjwa wa utapiamlo katika kata ya Kibara na Kisori kwenye Jimbo la Mwibara wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Sababu kubwa ya watoto hao kuugua ugonjwa huo ni kutokana na kukosa lishe bora kutoka katika familia zao ikiwemo kama, samaki, mayai, maziwa, mboga za majani, matunda na vyakula vingine vyenye madini mwilini.

mtoto-mgonjwa-utapiamlo

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dokta Rainer Kapinga alisema kuwa, idadi kubwa ya watoto wanaugua ugonjwa huo wapo katika jimbo la kibara na kisori Magharibi mwa wilaya hiyo, ambako kumekubwa na ukame kwa kiasi kikubwa.

"Kati ya watoto 17,570 wa wilaya hii watoto 294 wanaumwa utapiamlo sawa na asilimia 1.5, hii ni hatari kwa sababu watoto hao wanauwezekano mkubwa wa kupoteza maisha kwa kukosa matibu sahihi pamoja na lishe bora kwa sababu eneo hilo kuendelea kukubwa na ukame, na familia mbalimbali kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya tatizo hilo kwa watoto wao,"alisema Dokta Kapinga.

Aidha Dokta Kapinga alisema kuwa, kufuatia kukithiri kwa tatizo hilo la utapiamlo kwa watoto mbalimbali katika wilaya hiyo, Wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali wa masuala ya afya, wameiagiza wilaya hiyo kutenga pesa maalumu katika bajeti ya mwaka huu ili kusaidia kutatua tatizo hilo.

Dokta Kapinga alisema kuwa ndio tupo katika maandalizi ya kuandaa bajeti ya mwaka  mpya wa fedha 2013 hadi 2014, tayali tumetenga asilimia 2 hadi 3 ya pesa za bajeti ambazo ni sawa na sh. milioni 20, pesa hizo zitasaidia kutoa dawa za minyonyoo na kuwahamasisha wanajamii wa jimbo la Mwibara kulima kilomo cha bustani za mboga za majani pamoja na kufuga.

Pia wanapewa ushirikiana na shirika lisilo la kiserikali PSI, kwa kutoa elimu sehemu mbalimbali za vijijini juu ya umuhimu wa chakula bora kwa watoto pamoja kuwasaidia kutoa dawa za ugonjwa wa minyonyoo kwa watoto wa shule ya awali na msingi.

Kwimba Masunga ni mama wenye watoto watatu kati ya hao mmoja anaumwa ugonjwa wa utapiamlo, mama huyu anatokea katika kata ya Kisori huko anakoishi hawezi kulima kwa sababu ya hali ya ukame na maisha yake yote anategemea kununua chakula dukani.

utapiamlo-mgonjwa

"Nashindwa kulima kwa sababu ya ukame katika kata ya Kisori, hata kufuga pia ni tatizo kubwa kwa sababu ukifuga ng'ombe zinakufa kwa njaa kwa kukosa kula majani na maji ya kunywa, basi maisha yangu kwa sasa nategemea kununua dukani tuu,"alisema Masunga.

Masunga alisema kuwa mtoto wake anayeumwa utapiamlo anamwaka mmoja na miezi saba, alianza kuugua homa za mara kwa mara akiwa na miezi saba, alijitahidi kumpeleka zahanati na kupatiwa dawa za malaria lakini hakupona na kila siku anazidi kuzoofika, mpaka sasa ana mwaka mmoja anumwa na ndio yupo katika hali hiyo.

"Najitahidi kumlisha chakula lakini hataki kula yeye analia tuu hata kula kwake ni shinda sana, madawa nimemaliza lakini mtoto bado anaendelea kuumwa tuu, ndio leo nimemleta katika kituo hiki cha afya ndio wananiambia mtoto wangu anaumwa utapiamlo kwa sababu ya kukosa lishe, ndio inawezekana kwa sababu chakula ni shinda nyumbani," alisema huku akimwangalia mtoto wake na machozi yakitiririka shavuni.

utapiamlo-bunda

Tunaiomba serikali kutusaidia chakula maana hali ni mbaya sana hasa kwa kipindi hiki cha kilimo chakula kinapatikana kwa shinda sana pale kijijini kwetu, Mbunge wetu basi atusaidie kutuombea chakula katika wilaya za jirani ili watoto wasife kwa kukosa chakula.

Tatizo kubwa la jimbo hilo kuathirika na ugonjwa wa utapiamlo ni kwa sababu ya kukosa mvua za masika na vuli ambazo zingewasaidia kulima kilimo cha muda mfupi kama mahindi, maharege, mboga mboga, mtama na mihogo, lakini magonjwa ya mazao kama batobato yameharibu zao la mhogo katika jimbo hilo.

1 Comment
  • Jamani, samaki, na ng'ombe kwa ajili ya maziwa huko si ndo kwenyewe? Inakuwaje tena utipiamlo?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *