Wakunga wa jadi nusura ya wajawazito Bunda

Gordon Kalulunga

HATIMA ya wajawazito wilayani Bunda mkoani Mara ipo mikononi mwa wakunga wa jadi na kujifungulia nyumbani bila msaada wa wataalam. Wilaya hiyo ina upungufu wa asilimia 42 ya watumishi wa afya wenye sifa.

Hakuna dawa zinazotengwa moja kwa moja kwa ajili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano. Lakini serikali inasema kuwa makundi hayo yanapaswa kutibiwa bure. Kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto zinauzwa 500 ingawa zimeandikwa haziuzwi.

Bohari ya dawa ya serikali (MSD) hata wakilipwa pesa na halmashauri hawapeleki dawa zote zinazohitajika kwa wakati kutokana na mahitaji yanayotumwa, lakini kibaya zaidi hawatoi taarifa zozote za kukosekana dawa hizo wakati tayari wanakuwa wamelipwa!

Mfumo wa manunuzi ya dawa ni mbovu na una mianya mingi ya ‘’rushwa halali’’ ambapo wahusika wanatumia taaluma zao kuongeza hesabu kwenye stakabadhi.

Mjamzito Agnes Baraka (23) mkazi wa kitongoji cha Kambubu kata ya Nyamang’uta anasema kuwa kama mimba yake itaendelea vizuri bila kupata au kuhisi matatizo basi yeye atajifungulia nyumbani badala ya kituo cha afya au hospitali.

‘’Ukiwa nyumbani unapata msada hata wa mzazi au mtu mwingine yeyote lakini hospitali hakuna msaada. Ni bora kwa wakunga wa jadi. Mtoto wangu wa kwanza nilijifungulia nyumbani na hii ni mimba yangu ya nne, moja iliharibika na moja mtoto alikufa kwa uzembe wa wataalam wa afya’’ anasema Agnes.

Maeneo maalum yenye viwango vya juu vya vifo katika wilaya hiyo ni pamoja na Hunyali, Guta, Mariwanda ambako kuna vifo zaidi.

Utafiti unaonesha kuwa katika eneo la Hunyari, wanawake wengi wanajifungulia nyumbani na baadhi yao wanapoteza maisha na hii ni kata inayoongoza wilayani humo kwa wajawazito kujifungulia nyumbani ikifuatiwa na kata ya Guta.

Katika kata hiyo mwaka 2009 wanawake 238 walijifungua na kati ya hao wanawake 148 walijifungulia nyumbani na watatu kati yao walifariki dunia.

Kata ya Guta mwaka 2009 jumla ya wanawake 183 walijifungua na kati yao 111 walijifungulia nyumbani ambapo wanawake wawili walipoteza maisha.

Katika eneo la Mariwanda jumla ya wanawake 141 walijifungulia nyumbani mwaka 2008 na kifo kimoja kilitokea.

Katika eneo la Mugara kuna zahanati ambapo akina mama 256 walijifungua na kati ya 206 akina mama 185 walijifungulia kwa wakunga wa jadi waliopata mafunzo.

Akina mama 71 walijifungulia kwenye zahanati ya Mugara ambapo utafiti umebaini kuwa kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya na kwa wakunga wa jadi waliopata mafunzo kumepunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Rainer Kapinga anasema kuwa kwa sasa uwiano wa vifo vya wajawazito kwa mwaka 2007 ilikuwa ni vifo 370 kati ya vizazi hai 100,000 na mwaka 2011-2012 vifo vilikuwa 77 kati ya 100,000.

Anasema bajeti ya afya kwa wilaya hiyo ni milioni 800 ambapo katika eneo la afya ya mama na mtoto ni Milioni 200 fedha ambayo inaisha kwa miezi minne tu badala ya mwaka mzima.

‘’Serikali imeweka kipaumbele katika upande wa afya ambapo kipaumbele cha kwanza ni dawa na vifaa na namba mbili ni suala la mama na mtoto’’ anasema Dr. Kapinga.

Kwa upande wake mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani Bunda Daines Limo anasema kuwa kutokana na upungufu wa watumishi na jamii kuwaamini zaidi wakunga wa jadi, nao wanawaruhusu wakunga kutoa huduma za kuzalisha wajawazito.

‘’Jamii inawaamini wakunga sasa sisi tukiwadharau tutakuwa hatutendi haki na hatutafikia malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano’’ anasema Daines Limo.

Anasema wanawatambua wakunga hao wa jadi kwa kuwapa mafunzo na kila kijiji kilichopo ndani ya wilaya ya Bunda kuna wakunga wawili ambapo wilaya hiyo ina vijiji 106 hivyo kufanya idadi ya wakunga wanaotambulika kufikia 202.

Kuhusu uzazi wa mpango anasema kuwa hali si nzuri ambapo wanawake wanaotumia huduma hizo ni kati ya asilimia 13-23 na kwamba wastani wa kuzaa kwa mwanamke katika wilaya hiyo ni watoto 9-13.

Utafiti unaonesha kuwa sababu zinazochangia akina mama wajawazito kutotumia vituo vya huduma za afya wakati wa kujifungua kama zilivyotolewa na wananchi wa maeneo yaliyoathirika na vifo ni pamoja na vitongoji kuwa mbali na vituo vya kutolea huduma.

Sababu zingine ambazo wananchi wameeleza ni pamoja na dhana ya baadhi ya akina mama kudhani kuwa kujifungulia nyumbani ni ujasiri, kauli mbaya kutoka kwa baadhi ya watumishi wa afya na umasikini uliokubuhu.

Imani, mila na desturi. Miundombinu duni. Uhaba wa vitendea kazi kwa watumishi wa afya, ukoseph wa maji, hakuna sehemu ya kupumzika kabla na baada ya kujifungua hasa kwenye zahanati.

Elimu ya uzazi kutotolewa kwa jinsi zote yaani mwanaume na mwanamke na kutotiliwa maanani na walengwa, mimba za utotoni, baadhi ya wahudumu kuishi nje ya vituo mfano katika eneo la Mugara ambako mganga anaishi Bunda mjini na muuguzi anaishi Isanju, mhudumu wa afya ndiye anaishi kituoni.

Aidha sababu nyingine ni pamoja na imani potofu ambapo mwaka 2008 na mwaka 2009 imeelezwa kuwa kulitokea vifo viwili kutokana na waazi kukaidi kutumia hudum za afya na badala yake wakaenda kuombewa.

Lengo la utafiti huu ilikuwa kutafuta kwa nini wilaya ya Bunda ina kiwango cha juu cha vifo vya akina mama vinavyotokea na uzazi.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *