Shule ya msingi Darpori: Kitabu kimoja, darasa zima

Albano Midelo

ELIMU bora kwa watanzania wote wa mjini na wale wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini  ni moja ya malengo ya millennia ya serikali ya chama tawala  ndiyo maana ulianzishwa mpango wa kuboresha elimu ya msingi MEM na kuboresha elimu ya sekondari MES.

Hata hivyo mpango wa kuboresha elimu bora kwa watanzania unaonekana kukabiliwa na changamoto nyingi katika baadhi ya maeneo yenye mazingira magumu kama hali ilivyo katika shule ya msingi Darpori iliyopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma. Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule anasema kijiji hicho chenye utajiri wa madini ya dhahabu kina watu karibu 10,000 kilianza rasmi mwaka 2004, kina karibu makabila yote 120 yaliopo nchini pamoja raia kutoka nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

Kijiji cha Darpori kilichopo katika kata ya Tingi  kinaundwa na vitongoji vinne ambavyo ni Songeapori,Lunyere, Tanzania One na Njarambe, kijiji kina shule moja ya msingi ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazochangia kushusha elimu kwa wanafunzi.

Andrew Kayuni ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Darpori  anazitaja changamoto ambazo zinaikabili shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 ikiwa na jumla ya wanafunzi 143 kati yao wavulana 72 na wasichana71 kuwa ni pamoja na shule kuwa na vyumba vinne tu vya madarasa kati ya saba vinavyohitajika hali ambayo inasababisha darasa la tatu na nne pamoja na darasa la sita na la saba kusoma katika chumba kimoja.

“Mwalimu wa darasa la tatu akiingia wanafunzi wa darasa la nne wanabaki darasani kimya wakimsubiri mwalimu wao pia katika chumba cha darasa la saba mwalimu mmoja anapoingia anafundisha darasa linalohusika na wale ambao hawahusiki ingawa wapo darasani wanakuwa kimya hali hii inavuruga ratiba ya masomo na kuleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi na walimu katika ufundishaji’’, anasisitiza mwalimu Kayuni.

Changamoto nyingine anazitaja kuwa ni shule ina walimu watano tu kati ya mahitaji ya walimu wanane,walimu hawana choo pamoja na upungufu mkubwa wa samani za shule yakiwemo madawati hali ambayo inasababisha dawati moja kukalia watoto watano hadi sita badala ya dawati hilo kukaliwa na watoto  wawili hadi watatu.

Changamoto nyingine kubwa ambayo inawadharirisha walimu katika shule hiyo ni familia mbili za walimu wenye familia ya watu 16 hadi 18 kuishi katika nyumba moja ya shule yenye vyumba viwili hali ambayo imesababisha walimu kuishi katika mazingira magumu ya kazi.

“Shule yetu ina nyumba mbili tu za walimu, nyumba hizi zina vyumba viwili pamoja na sebule, hapa shuleni kuna walimu watano, katika nyumba hizi mbili kila nyumba moja zinaishi familia mbili za watu kati ya 16 hadi 18, mwalimu mmoja hana nyumba amepanga katika nyumba za wachimba madini ambazo analipa pesa nyingi sana  tunaomba  serikali isaidie kuleta fedha za ujenzi wa nyumba za walimu’’,alisema.

Pamoja na changamoto hizi mkuu huyo wa shule hiyo anasema shule hiyo licha ya kukabiliwa na  mazingira magumu ya kazi   kitaaluma inajitahidi kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa ya darasa la saba karibu kila mwaka ambapo mwaka 2008 wanafunzi watano walifaulu kati yao wavulana watatu na wasichana wawili ,mwaka 2009 jumla ya wanafunzi saba walifaulu kati yao wavulana watatu na wasichana wanne na mwaka 2010 wanafunzi 12 walifaulu kati yao wavulana watano na wasichana saba.

Ametoa mwito maalum kwa serikali kuwatazama kwa macho ya huruma walimu wote nchini ambao wanafanyakazi katika mazingira magumu kama ilivyo katika kijiji cha Darpori ambako mazingira na maisha ya walimu ni magumu hali ambayo inasababisha mishahara wanayopata kuishia kulipa nauli,kulala katika nyumba za wageni wakati wanafuatailia mishahara pamoja na kununua bidhaa kwa bei mbaya.

Godfrid Nchimbi ni mwalimu wa shule ya msingi Darpori anasisitiza kuwa maisha na mazingira ya kufundishia katika shule hiyo ni magumu  kwa mfano wakati wa kwenda kuchukua mshahara wanatumia magari ya machimbo ya dhahabu ambapo wakati wa masika kutokana na ubovu wa barabara inatakiwa mwalimu aombe ruhusa ya wiki moja   na kulipa nauli ni shilingi 80,000 kwenda na kurudi, licha ya kulipa nauli hiyo abiria anawekwa juu ya bodi la gari au kushika bomba kwa nje  umbali wa kilometa 82.

Bidhaa na vyakula katika kijiji hiki cha machimbo ya dhahabu yapo juu kwa kuwa idadi kubwa ya wakazi wa kijiji hiki wanajishughulisha na uchimbaji wa madini kwa mfano vocha ya simu ni shilingi 1500 badala ya 1000, soda shilingi 1500 hadi 2000, bei ya petroli ni  kati ya shilingi 5000 hadi 8000 kwa lita moja walimu wenye pikipiki tunaingia gharama kubwa ya mafuta’’, alisema.

Anusiata Mbunda amefundisha katika shule ya msingi Darpori kwa miaka minne sasa, anasema kutokana na mazingira magumu ya kufundishia miaka miwili iliyopita alitamani kuacha kazi lakini anaendelea kuvumilia ili kuwasaidia watoto wa kijiji hicho ambao anasema wanahitaji elimu kama ilivyo kwa watoto wengine wanaoishi katika mazingira bora ya kujifunzia na hivyo ametoa wito kwa serikali kutafutia ufumbuzi wa baadhi ya changamoto.

“Ndugu mwandishi umefanya vema kuja kututembelea na kuona matatizo yetu hebu fikiria kuna baadhi ya masomo hapa kitabu kimoja wanasoma  darasa zima sasa katika mazingira kama haya kweli elimu bora itatolewa? Wanafunzi katika dawati moja wanakaa sita, chumba kimoja cha darasa yanasomea madarasa mawili kwa wakati mmoja hii ni aibu na udharirishaji wa wanafunzi na walimu’’, alisema.

Uchunguzi umebaini kuwa shule ya msingi Darpori ina vitabu vichache vya kufundishia na kujifunzia kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaosoma wasiozidi 140 hali ambayo inasababisha kupata shilingi 7000 tu   zinazotolewa na idara ya elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika mpango wa kuboresha elimu yaani MEM  kwa ajili ya ununuzi wa vitabu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule amekiri kuwa mazingira ya shule hiyo hayaridhishi na kwamba baadhi yake zimeanza kutafutiwa ufumbuzi   ikiwemo ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na kujenga choo cha walimu na kusisitiza kuwa hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu wanatarajia vyumba hivyo vitakuwa vimekamilika.

1 Comment
  • tunaiomba serikali kupitia wizara ya elimu Ione umuhimu wa kuisaidia shule yetu kwani viwango vya ufahuru vya watoto wetu vinashuka siku hadi siku walimu wachache,vitabu vichache ,mazingira,miundombinu haikizi matakwa ya walimu na wanafunzi je taifa hili la watoto wajinga tutalipeleka wapi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *