Uhaba wa dawa sababu ya kusingizia ugonjwa Rorya

Stella Mwaikusa

Katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya wakazi wa vijiji vinavyohudumiwa na kituo  cha afya cha Kinesi kilichopo kata ya Nyamunga wilaya ya Rorya wanasingizia ugonjwa ili kupata dawa za akiba.

Mganga mkuu msaidizi wa kituo hicho cha Kinesi Ngocho Marwa, anasema kutokana na hali ya kukosekana kwa dawa za magonjwa mbalimbali katika kituo hicho, kumewafanya baadhi ya wagonjwa kusingizia ugonjwa ili kupata dawa pale wanaposikia dawa zimekuja katika kituo hicho.

Anasema taarifa za  kuwepo kwa dawa zinawafikia wakazi wa mji huo kutokana na kamati ya afya ya kijiji kupewa taarifa hizo, na pale wanapopata taarifa basi mtu huja na watoto wake wote kila mtu akitaja ugonjwa wake ili tu wapate dawa nyingi kwa ajili ya akiba.

Anasema kukosekana kwa dawa katika kituo hicho kunatokana na Bohari ya dawa ya taifa (MSD), kuleta kiasi kidogo cha dawa kuliko kilichoagizwa na kufanya hali iwe ngumu kwao.

Marwa anasema dawa zikifika kituoni hapo zinakaa kwa wiki moja tu na hazipatikani tena, mpaka baada ya miezi mitatu au sita, hali ambayo imewafanya wananchi kubuni mbinu za kusingizia ugonjwa.

kinesiii

Picha: Wahudumu wa afya wa kituo cha Kinesi

“Tumezungukwa na maji ya ziwa victoria kuna mmbu wengi pamoja na magonjwa ya kichocho lakini ni miezi sita sasa hakuna dawa ya malaria wala kichocho .” anaeleza Marwa.

Anasema waligundua kwamba baadhi ya wakazi wanasingizia ugonjwa kwani dawa zikiisha hawaonekani, vile vile mtoto anafika hapa unamuuliza anaumwa nini hata hasemi huku mzazi wake akitaja ugonjwa mwingine tofauti na ule aliotaja mwanzo.

“Mtu anakuja na watoto nane au tisa  na kila mtu anatakiwa kupewa dawa na dawa zenyewe zinakuja chache basi hiyo ni changamoto kubwa kwetu” anaeleza Marwa.

2 Comments
  • Sasa Stella usipokuwa mbunifu na bajeti inayotoka kwa huduma ya afya ni finyu na unafamilia kubwa, mchakato ndio huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *