Lowassa kuongoza Harambee ya Kanisa Nyakato Mwanza

Jamii Africa

WAZIRI Mkuu Msitaafu, Edward Lowassa, wiki hii anatarajiwa kuzuru Jijini Mwanza kwa lengo la kuongoza harambee ya kuchangisha zaidi ya sh. milioni 150 katika Kanisa la Romani Katoriki, Parokia ya Nyakato, Jimbo Kuu la Mwanza; Mtandao huu umethibitishiwa.  Katika harambee hiyo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli Mkoani Arusha (CCM), na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ataungana na wageni wengine waarikwa zaidi ya 300, na kwamba zaidi ya sh. milioni 150 zinahitajika ili kuezeka paa la kanisa hilo la RC Nyakato, ambalo ni kubwa kuliko yote Kanda ya Ziwa Victoria.

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa

Akizungumza leo ofisini kwake jijini Mwanza kuhusu ujio wa Lowassa, mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo Parokia ya Nyakato, Pastory Masota (pichani chini), alisema, harambee hiyo itafanyika Jumapili wiki hii.  “Tumemwalika Lowassa katika kufanikisha harambee yetu hii, maana ni mtu mwenye mahusiano mazuri sana na jamii yote. Harambee hii itakuwa Jumapili wiki hii pale kanisani Nyakato National.

 

Pastory Masota

“Ukitaka kufanikisha jambo lazima utafute mtu anayependa ushirikiano na maendeleo kwa ujumla. Lowassa amekubali mwaliko wetu na atakuja, na kanisa letu hili ni kubwa kuliko yote Kanda hii ya Ziwa Victoria linalochukuwa waumini 1,350 kwa wakati mmoja”, alisema Masota.

Hata hivyo, ujio wa Lowassa jijini Mwanza, umeonekana kuwafurahisha watu wengi na wa kada mbali mbali mkoani hapa, na kwamba wanamsubiri kwa hamu ili waungane naye katika kufanikisha shughuli zote za kimaendeleo ndani na nje ya kanisa hilo.

Akifafanua zaidi kuhusu ujio wa kiongozi huyo na mwanasiasa aliyebobea, Masota alisema, harambee hiyo kubwa na ya aina yake, itatanguliwa na misa takatifu kuanzia saa 4:30 hadi saa 5 asubuhi, na wageni mbali mbali wa Serikali wamealikwa kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Arusha na Dar es Salaam.

Alisema, anaamini siku hiyo ya harambee kanisa litafanikiwa kufikia malengo yake kutokana na ushawishi mzuri unaokubalika kutoka kwa kiongozi huyo, ambaye alijiuzulu nafasi yake ya Uwaziri Mkuu kutokana na kuandamwa na shutuma alizoziita za uongo zisizo na chembe ya ukweli ndani yake.

Taarifa zilizopatikana jijini Mwanza zinaeleza kwamba, mbali na mambo mengine atatumia fursa hiyo kuhamasisha shughuli mbali mbali za maendeleo ndani na nje ya mkoa wa Mwanza, ikiwa ni lengo la kuwatoa Watanzania katika lindi la umasikini wa vipato.

Kwa mujibu wa Masota, hadi sasa kanisa hilo la Romani Katoliki Parokia ya Nyakato, Jimbo Kuu la Mwanza, limetumia zaidi ya sh. milioni 170, na kwamba harambee hiyo itakayoongozwa na Lowassa itafanikisha kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo ambalo ni la kwanza kwa ukubwa kujengwa bila ufadhili kutoka nje ya nchi.

Mwisho.

Na Sitta Tumma

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *