Yaliyotokea Mtwara: Wanasiasa, serikali walipotoka!

Jamii Africa

Mtazamo na msimamo wa sisi wapiganaji wa kudumisha fikra za Baba wa Taifa, kuhusu yaliyojitokeza katika uchangiaji wa usafirishaji wa Gesi Asilia kutoka Mtwara ni kwamba upungufu uliojitokeza ni kwamba hoja zinazotolewa kwa pande zote husika sio sahihi kwa sababu hoja zao hazizingatii uchumi, hali ya nchi kiuchumi na mslahi ya Taifa kwa ujumla.

Mambo yaliyodhihirika katika suala hili na kama kama yafuatayo:-

1. Pamoja na kwamba wapiganaji wanaungana na wale wanaopinga usafirishaji wa gesi Asilia kutoka Mtwara, jambo lililodhihirika ni kwamba hoja za wale wote wanaopinga mradi huo sio sahihi. Hoja za Mtwara zimetawaliwa na ubinafsi, ukabila na uelewa mdogo wa umiliki wa Raslimali za Taifa na matumizi ya matunda yatokanayo na raslimali za Taifa.

2. Kwakuwa wenyeji wa Mtwara wana idadi kubwa ya wapiga kura katika chaguzi za kisiasa, Wanasiasa wamevamia sakata hili bila kujali maslahi na mustakabali wa kitaifa, kama:

(a) Nukuu kutoka Tanzania Daima toleo No. 2959 la 08/01/2013:- Dk. Slaa: Gesi ni mali ya wananchi! Adai hawatafuti umaarufu bali wanapinga dhuluma. Wananchi wa Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu, wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai wanufaike nayo ili nao wapate viwanda, shule na hospitali nzuri”. Ameendelea kusema kwamba  nukuu: wanaoendeleza mgogoro katika sakata hili ni wale waliofilisika kifikra, hawajui katiba na hawajui kuwa wananchi ndio walinzi wa kwanza wa raslimali zao…..”

Hoja yangu:

Hivi Dr. Slaa hajafilisika kisiasa kudai kwamba gesi ni mali ya watu wa Mtwara tu?. Ni kweli umasikini uko Mtwara tu, au Watanzania wote ni masikini? Je, hajui kwamba ukitoa upendeleo kwa baadhi ya watu, watu hao waliopendelewa wanakuwa wanawanyonya wananchi wengine? Je, Raslimali za Taifa sio kwa Watanzania wote? Je, tukubali Raslimali za Taifa zimilikiwe na watu wa mahali zinapopatikana? Je, watu wa asili hiyo hawafaidi mfuko wa hazina itokanayo katika sehemu nyingine za Watanzania? Aliyewakopa watu wa Mtwara korosho ni nani?. Dr. Slaa ameshindwa kujenga hoja za kiuchumi za kuwawezesha Watanzania wote kwa ujumla wetu tufaidike kutokana na  miradi ya Gesi Asilia?

3. Baya zaidi, hata viongozi wa dini wamekurupuka kutumia heshima yao wanayopewa na watanzania bila kujali kwamba mchango wao unaweza kuongeza tofauti za kidini! Ni vema viongozi wa dini wajiepushe kuingilia migongano ya wanasiasa na hasa pale mtazamo wao unatofautiana na Serikali iliyoko madarakani. Wana jukumu kubwa la kujenga taifa la Tanzania lenye maadili mema bila kuingilia shughuli za Serikali. Haki yao kikatiba ya kutoa mawazo inaheshimika, lakini ni vema watoe mawazo yao binafsi bila kuhusisha taasisi za kidini wanazozongoza.

4.  Pamoja na kwamba maelezo  ya Serikali ni kwamba Maliasili zote nchini bila kujali wapi zinapopatikana ni mali ya Taifa zima, na matunda yake ni kwa maslahi ya umma wote wa Tanzania maelezo kuhusu mradi huo, yana kasoro nyingi kiuchumi na kimazingira. Maelezo ya Serikali ni sahihi kwamba hoja nyingi za wanasiasa za kupinga mradi huo zimetolewa kisiasa na sio za kiuchumi. Mfano ninukuu maelezo potofu ya Dr. Slaa katika Tanzania Daima toleo No. 2959 la tarehe 08/01/2013:- Wananchi wa Mtwara ni Masikini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu, wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi wanayo haki ya kudai wanufaike nayo ili nao wapate viwanda, shule, na hospitali nzuri. Katiba anayonukuu ni vema aisome vizuri.  Gesi kama maliasili nyinginezo ni ya watanzania wote, Watanzania wote ni masikini, huduma za jamii ni wajibu hata kama gesi haikupatikana. Hapa Dr. Slaa anataka kuhalalalisha ubaguzi na ukabila. Kuna sehemu nyingi za Tanzania ambazo hawana hata maji. Kero anazozisema ndizo zinazojitokeza kwa nchi nzima kama ahadi katika ilani za uchaguzi za kila Chama cha siasa. Ni vema kutumia hoja za uchumi kuliko kutumia hoja za ukabila na ubinafsi.

mtwara-bango

5. Kwa maamuzi sahihi tunao uwezo wa kulitoa Taifa letu katika hali ya unyonge na kulitia katika hali ya nguvu. Tunaweza kuongoza vita vya wananchi watoke katika hali ya dhiki na kuwa katika hali ya neema.

6.  Kwa upande wa Serikali ni vigumu kuhalalisha kigezo cha maamuzi ya utekelezaji wa mradi huo kama ilivyo. Maelezo ya Serikali hayaridhishi, kuzingatia vigezo vya kiuchumi endelevu kwa nchi yenye dhamira ya kujitegemea kiuchumi, pamoja na hali ya uchumi tuliyonayo. Na wakati huo huo vigezo vya mazingira havikutumika. Maamuzi haya yanadhihirisha upungufu wa taaluma ya uchumi walionayo viongozi na watendaji katika ngazi za maamuzi. Mapungufu ya maamuzi kiuchumi yamesababisha uchumi wa nchi yetu kuzorota kiasi kwamba Mhe. Rais amewahi kutamka kwamba kuna haja ya wanataaluma wetu kwenda Malaysia kuona jinsi wanavyoendesha uchumi wao.

7. Vile vile maamuzi ya kuanzisha mradi huu haukutumia ushirikishwaji wa wadau kama ilivyo katika nchi inayofuata nadharia ya Ujamaa. Uongozi katika nchi ya Ujamaa si uongozi wa amri na utawala wa mabavu. Kiongozi huongoza kwa kuelimisha, kuelewesha, kushauri, kushawishi, kushirikisha na kuelekeza. Nguvu yake kubwa inatokana na kukubalika kwake na umma, na fikra yake sahihi inayolingana na maslahi ya Umma. Ili kutimiza jukumu lake la uongozi anahitaji kutumia nguvu ya hoja siyo hoja ya nguvu. Jambo lililodhihirika ni kwamba viongozi walioko madarakani wanaweza kufanya maamuzi bila kushirikisha wadau sawa na dikteta. Kwa jinsi hii demokrasia katika nchi yetu inaisha baada ya kupiga kura ya kutoa ridhaa  kwa viongozi kuwa na mamlaka kwa mfumo wa vyama vingi.

Mijadala kuhusu miradi mingi huwa inaibuka wakati miradi hiyo imo katika hatua za utekelezaji. hapa usafirishaji wa Gesi Asilia ni mfano hai, pamoja na mingine ni kama  ugawaji ardhi kiholela kwa wageni na uvunaji wa madini hatari ya urani.

UPUNGUFU WA MTAZAMO WA SERIKALI

 Hakuna ubishi kwamba kuna haja ya kuongeza uzalishaji ya umeme.

  • Hakuna Ubishi kwamba gesi inahitajika kama nishati mbadala na wakati huo huo hakuna ubishi kwamba gesi inaweza kuuzwa katika nchi jirani na nchi za nje.
  • Hakuna ubishi kwamba Watanzania ni masikini na adui wetu mkubwa ni umasikini lau kama ujinga unatuongezea umasikini, na umasikini unatugharimu kupambana na adui ujinga na adui Maradhi. Umasikini umewezesha ghiliba za vibepari na vibwanyenye kubabaisha viongozi wetu na kusababisha kupanua ubepari.
  • Hakuna ubishi kwamba nchi yetu kama nchi inayoendelea ina changamoto nyingi za maendeleo ambazo ufumbuzi wake unategemea utekelezaji wa miradi mbali mbali ambayo kiwango chake ni kikukubwa kulingana na akiba tuliyo nayo.
  • Hakuna ubishi kwamba Serikali hupata fedha zake za matumizi kutokana na kodi. Na kodi hupatikana kutoka katika kile wananchi wanachokipata. Kama kodi  inayopatikana ni ndogo maana yake watu ni masikini kipato chao ni kidogo. Wenye kipato kikubwa watalipa kiwango kikubwa cha kodi.
  • Serikali inapokiri kwamba asilimia 80% ya kodi inakusanywa kutoka Dar es Salaam, tafsiri yake ni kwamba Dar es Salaam wanahodhi asilimia 80% ya uchumi wa nchi nzima. Huko bara Mabepari watakuwa wanahodhi zaidi ya asilimia 15% ya uchumi uliobaki, Kwa hiyo Watanzania wanamiliki chini ya asilimi 5% ya uchumi wa Taifa lao wenyewe. Hoja hii dhaifu ambayo inajenga taswira kwamba mgawanyo waq keki ya Taifa sio sawia, ndiyo inayowapotosha watu wa Mtwara hadi kuandamana wakijenga fikra potofu kwamba gesi ni ya Mtwara na Mtwara watafaidika nayo endapo haitasafirishwa kwenda Dar es Salaam kutoka Mtwara.
  • Hakuna ubishi kwamba Tanzania ina raslimali nyingi za kutuwezesha kuwa Taifa Tajiri duniani. Uchumi tunao lakini tumeukalia. Hakuna ubishi kwamba Mabepari ambao ni Wakoloni Mamboleo ndio hivi sasa ndio wanaofaidi raslimali na utajiri wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa.Hivi sasa wanatubeza kwa msemo waliouapata Tarawanda Mkoa wa Pwani usemao “milango ya Tanzania ni milango ya Bagaza habule kofuli”. Milango ya Tanzania haina kufuli, Mabepari wanaingia na kusomba raslimali zetu watakavyo na kuzifaidi kwa jina la ‘Wawekezaji’.

Je, tunamuenzi Baba wa Taifa kwa kupuuza mafundisho yake kwamba Ubepari ni Unyama? Au tunafuata ni methali ya waarabu isemayo “wamaa yadhakaru ilal ul albabi”. Hawakumbuki ila wenye akili.

  • Tupige vita kuifanya nchi yetu kugeuzwa kuwa Pango la Wanyonyaji na hali ya kwamba tunajua kwamba mabepari na makabaila wana hulka ya unyonyaji na ubeberu, na ubepari ni unyama. Yes we can! Mwalimu kasema “It can be done play your part!” Obama anasema ‘Yes we can!’
  • Hakuna ubishi kwamba ufisadi na rushwa iliokithiri katika nchi yetu imeongezewa kasi na wawekezaji. Hakuna ubishi kwamba nchi zote duniani zinakabiliwa na changamoto la uchumi, idadi ya watu, ardhi na fursa za kuwekeza. Hakuna ubishi kwamba nchi hizo zinaboresha sera zao za kunyonya nchi maskini kwa msemo wao usemao “wajinga ndio waliwao”. Hakuna ubishi kwamba wahenga walisema kwamba ukitaka kula cha mwenzio sharti na wewe uliwe. (Je Watanzania tuko tayari kuliwa?). Hakuna ubishi kwamba Tanzania tulionewa kiasi cha kutosha, trulinyonywa kiasi cha kutosha, tulidharauliwa kiasi cha kutosha na tulipuuzwa kiasi cha kutosha.
  • Dhamira ya kupigania uhuru ilikuwa ni kujenga Taifa ambalo hatutanyonywa tena, hatutaonewa tena, hatutapuuzwa tena wala hatutadharauliwa tena. Hakuna shaka kwamba umoja ni nguvu na utedgano ni udhaifu.) Waingereza wana msema wao usemao “Amlipaye mwimbaji ndiye huchagua wimbo.” Tutawezaje kutegemea nchi za kigeni na Makampuni ya kigeni kwa sehemu kubwa ya maendeleo yetu bila kuzipa nchi hizo na Makampuni hayo sehemu kubwa ya uhuru wetu wa kutenda wapendavyo? Ukweli ni kwamba hatuwezi. Kwa taswira hii tuliamini kwamba Taifa haliwezi kuwa huru kama haliwezi kujitegemea.  Kwa jinsi hii tuliamua kufuata siasa ya nadharia ya Ujamaa na kujitegemea. Miaka mitano ya kwanza iliyofuatia uhuru ilikuwa kipindi kigumu kwa Serikali changa. TANU yenyewe ilibidi iondokane na hali ya kuwa Chama cha kupigania uhuru na kuwa Chama cha kulinda uhuru na kujenga Taifa linalojitawala. Katika hali ambayo changamoto za kukabiliano nazo zinakuwa nyingi, wachumi hutumia falsafa  yao inayowaongoza kiuchumi iitwayo  ‘Scale of Preference”, ambayo Waswahili wanaiita kipaumbele endapo kuna miradi mingi inayolazimika kutekelezwa.

Kwa hiyo Mapungufu katika maamuzi yaliyodhihirika ni kwamba hayakuzingatia falsafa za uchumi na tahadhari za mazingira kama ifuatavyo:-

Serikali haikuwa sahihi katika kuchagua kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara kuipeleka Dar es Salaam kuwa kipaumbele kutokana na udhaifu wa uchumi tulionao na changamoto muhimu tulizo nazo i.e. ‘Scale of Preference”, au kipaumbele.

Jambo lililodhihirika vile vile ni kwamba sisi wenyewe kama Taifa hatukutumia kwa kiasi cha kutosha nguvu za Serikali na za wananchi katika kufanya maamuzi sahihi ambayo ufumbuzi wake tuna uwezo nao. Hapa ni pamoja na kutambua na kuwashirikisha wachumi wa kweli walio wazalendo na wenye nadharia ya Ujamaa na Kujitegemea. Pamoja na Mheshimiwa Rais kuwa na dhamira ya kuchukua mfumo wa Malaysia katika uendeshaji wa uchumi wao, napenda kumhakikishia kuwa taasisi yetu inayo wataalamu wa uchumi ambao wanaweza kutoa mwelekeo sahihi. Mafanikio katika uchumi wa Malaysia, UAE, China, Indonesia, Taiwan, Korea yametokana na kutumia Fikra Sahihi za Baba wa Taifa kuendesha uchumi katika nchi zao. Napenda niwakumbushe kwamba katika makala zetu za awali tulieleza kwamba Baba wa taifa alikuwa mchumi lau kama hakutoboa siri ya taaluma yake. Fikra za Baba wa Taifa ni Falsafa Sahihi za Ubhumi na utawala bora.

Ufumbuzi wa uvunaji wa raslimali za Taifa na uendelezaji wa miradi mbali mbali katika nchi yetu tumeueleza kwa kirefu katika taarifa ya mdahalo wetu wa miaka 50 ya uhuru. Tunaweza kumiliki viwanda, na tunaweza kupata fedha, lakini msingi wake ni WANANCHI na JUHUDI yao na sio wageni kutoka ng’ambo. Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe wenye moyo na hasa walio wazalendo. Hii ndiyo maana ya kujitegemea.

Gesi asilia tunayo, watu tunao; kwa hiyo basi, ufumbuzi wa mgongano kaatika uvunaji na usafirishaji wa gesi toka Mtwara ni:-

(a)     Siasa safi (Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea), na

(b)     Uongozi bora

Tuwe makini katika kuchagua silaha ya mapinduzi tunayoyataka. Tunataka kuondoa unyonge wetu kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo hatuna. Ni dhahiri kwamba tumefanya makosa kuchagua fedha kama silaha yetu.

Ni fikra porofu kuchagua fedha kuwa ndiyo silaha yetu kubwa ya maendeleo hali tunajua kuwa nchi yetu ni masikini. Mnyonge hapigani kwa fedha!

Vile vile ni fikra potofu kuamini kuwa tutaweza kuondoa hali hii ya unyonge wetu kwa kutegemea fedha za wageni kutoka ng’ambo badala ya fedha zetu wenyewe. Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe wenye moyo na hasa walio wazalendo.

Taarifa ya wizara ya nishati inaonyesha kwamba TPDC inatumia fedha za walipa kodi kuwezesha wawekezaji kuvuna gesi na kupata faida kupeleka katika nchi zao

Tumejenga matumaini ya kupata fedha za maendeleo mbali mbali kwa kutumia njia potofu ya kualika msululu wa mabapari kuja kumiliki raslimali zetu na kuhodhi uchumi wetu. Lakini hatuwezi kupata za kutosha. Nia yetu na matumaini yetu ni kuwafanya wenye raslimali zao katika nchi za nje waone kwamba Tanzania ni nchi inayofaa kuingiza raslimali zao, kwani raslimali yao itakuwa salama, italeta faida, na faida hiyo wenyewe wataweza kuiondoa bila vipingamizi.. Je ni vyema kukubali kuacha uchumi wetu wote uwe mikononi mwa wageni kwa ajili ya kupata faida na kuipeleka katika nchi zao. Huu Ujamaa tunaosema kuwa ndiyo shabaha yetu, tutaujengaje? Hii ni ghiliba ya vibepari na vibwanyenye ambao ni adui wa Ujamaa wetu.

Siasa ya kualika msululu wa mabepari kuja kutunyonya na kupeleka fedha zetu za kigeni katika nchi zao utaacha uchumi wetu salama?  Madhara ya uwekezaji hayajaongeza kasi ya ufisadi, rushwa, kuongeza ukali wa maisha kwa mwananchi na kutupotosha katika utekelezaji wa siasa yetu ya Ujamaa? Je ni kweli tunaamini kwamba bila ubepari kwanza hatuwezi kujenga Ujamaa?

Je, kiongozi aliyeapa kulinda ujamaa, akipanua ubepari na kudhoofisha Ujamaa hajavunja katiba ya nchi ibara ya 9. Na kama kiongozi huyo ni mwanaCCM hajavunja katiba ya Chama chake kilichomuwezesha kupata ridhaa ya wananchi?

UVUNAJI WA GESI:-

(i)     Uwekezaji:-

Kwa hali ya kusikitisha taarifa ya wizara ya Nishati inaweka bayana Kwamba TPDC inatumia fedha ya walipa kodi kuwezesha wawekezaji kuvuna gesi asili ili wapate faida ya kupeleka kwao. Mwekezaji hatapeleka sarafu ya ki-Tanzania bali atapeleka fedha za kigeni. Kwa jinsi hii TPDC inawezesha uwekezaji wa mirija ya wawekezaji kunyonya fedha zetu za kigeni. Athari yake ni kudhoofisha thamani sarafu yetu ya ndani (Shillingi ya kitanzania) Thamani ya sarafu yetu ikidhoofika ukali wa maisha unaongezeka. Baya zaidi ni kodi zetu wenyewe zinatumika kuwezesha kuwekeza mirija ya kunyonya fedha zetu za kigeni isiyondosheka. Baba waTaifa alituusia tuwe na subira ya kuvuna madini mpaka tuelimishe vijana wetu. Lakini vile vile ili tufaidi raslimali zetu ni lazima tuzivune wenyewe.

Kama Serikali itakuwa na upungufu wa mtaji ni vema wauze hisa kupitia Dar es Salaam Stock exchange. Watanzania million 45 tunao uwezo kwa pamoja kumiliki uchumi wetu wenyewe. Taarifa ya Wizara ya Nishati inadai kwamba uchorongaji wa kusima kimoja cha gesi asilia nchi kavu ni dola za marekani Millioni 40. Watanzania Millioni 45 tunahitaji kununua hisa za wastaniwa dola moja kwa kila Mtanzania. Taarifa ya Waziri inaonyesha kwamba “Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia kila siku. Takribani Dola za Marekani Billioni Moja (sawa na Shillingi Trillion 1.6) kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini.  Taarifa hii inaonyesha kwamba Serikali inao uwezo wa kupata dola Million 40 kama wanao uwezo wa kutumia  Dola Billioni Moja kwa mafuta ya umeme tu.

Tukifanya maamuzi sahihi, kwa kutumia nguvu za Serikali na nguvu za wananchi tunaweza kumiliki uchumi wetu sisi wenyewe bila kualika msululu wa mabepari kuja kutunyonya. Ndugu zetu Mafisadi Watanzania hawatalazimika kuhamisha mitaji yao bali watapata fursa ya kusogeza badala ya kuzihamisha. Kwa jinsi hii thamani ya shillingi itabaki imara. Ili thamani ya shillingi yetu iwe imara inatubidi kukata mirija inayonyonya fedha zetu za kigeni.

Ushirikishwaji wa Wananchi katika uwekezaji kwa jinsi hii umetumika UAE. Watu wanaposikia kwamba UAE huwa wanawekewa fedha kwenye akaunti zao, ukweli ni kwamba huwa wanawekewa gawio la hisa zao katika miradi mbali mbali inayosimamiwa na serikali yao.

  • Ni vema Wizara itambue kwamba Gesi ina kiwango maalumu, ambacho hupungua kutokana na uvunaji. Kwa hiyo kuna siku gesi hiyo itakwisha. Nukuu ya Taarifa:- Kiasi cha wingi wa Gesi Asilia  iliyogunduliwa nchi kavu na baharini ni takribani Futi za ujazo trilioni 35.” Je hizi zinawatosha watanzania hadi siku ya kiyama? (mwisho wa dunia).
  • Kwa mtazamo wa matumizi ya maji ya mto Nile, ni kwamba hatutegemei Mto Nile (Kagera) kukauka pamoja na propaganda ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Kwa hiyo umeme kutokana na vyanzo vya mto Nile ungekuwa wa uhakika kwa muda mrefu.

(ii)    Usafirishaji:-

Kwa ujumla wetu, Watanzania wote tuna haki ya kugawana Keki ya Taifa sawia.

(a)  Pamoja na kodi ndogo kutoka Wilaya ya Ngara, mkazi wa Ngara analipa kodi zaidi ya mkazi wa Dar es Salaam. Bidhaa inaposafirishwa kutoka Dar kwenda Ngara inalipiwa VAT. Kodi hiyo ya ziada kutokana na usafirishaji kwa mithili ya VAT anailipa mkazi Ngara. Hata katika asilia 80% ya kodi iliyopatikana Dar, mkazi wa Ngara naye kachangia kwa namna moja au nyingine.Je inatajwa Ngara kujenga hoja ya kupuuza kuendeleza uzalishaji kwenye chanzo asili cha maji Omurusumo kwenye mto Nile (Kagera) kwa dhana kwamba Watanzania wa Ngara na karagwe watafaidi?

Matunda ya raslimali za kitaifa ni ya Watanzania wote. Lakini mkulima wa ngara analima Klahawa ambayo inaleta fedha za kigeni am,bazo Bepari mwekezaji atahamisha kupeleka kwao na kumuachia ukali wa maisha Vigezo vya uchumi havikuzingatiwa katika maamuzi ya kujenga bomba ya kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwende Dar es Salaam. Ukweli ni kwamba gharama ya kujenga bomba hilo ni kubwa sana.

Nchi yetu ni maskini na ina changamoto nyingi za kutatua. Ujenzi wa Bomba hilo sio kipaumbele. Kama ni uzalishaji wa umeme, ni ukweli kwamba gharama ya kuzalisha umeme lngekuwa rahisi kama mitambo ya Kinyerezi ingefungwa karibu na malghafi gesi inapopatikana (i.e. Mtwara) bila kuingia gharama ya kuisafirisha, na kuunganisha umeme huo kwenye gridi ya Taifa. Hata kama umeme utazalishwa Dar es Salaam, umeme huo vile vile utaunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

(b) Gesi ina hulka ya kuwaka moto. Kwa hiyo endapo bomba hilo litavuja, linaweza kuleta madhara ya maisha kwa watu wengi.

(c) Kinyerezi iko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa. Ndege za kimataifa zinaweza kususa kutua Dar es Salaam kwa tahadhari ya usalama, kufuatia madhara yatokanayo endapo gesi hiyo italipuka.

(d) Jiji la Dar es Salaam linapanuka kwa kasi kubwa. Kinyerezi ingetumika kwa makazi ya watu. Hapa udhaifu wa mipango miji umejitokeza, kama vile EPZ ilivyowekwa Mabibo External.

(e) Kwa ujumla tahadhari ya mazingira haikufanyiwa tathmini. Tunaiomba NEMC itoe taarifa ya Environmental impact Assessment.

(f) Hoja potofu ya ktgezo cha kodi ilipatikanayo kutoka Dar es Salaam kuwa asilimia 80% ni hoja dhaifu na inawaongezea watu wa Mtwara kuendelea kujenga hoja potofu ya kudai kwamba manufaa ya gesi yatakuwa ya watu wa Mtwara endapo gesi hiyo haitasafirishwa.

(g) Jambo linalodhihirika ni kwamba kama kweli Dar wanalipa asilimia 80% ya kodi na kodi inatokana na kiasi cha fedha kinachopatikana, tafsiri yake ni kwamba Dar es Salaam inamiliki asilimia 80%  ya uchumi wa Tanzania uliotokana na uwekezaji kutokana na raslimali za watanzania wote. Hii inajenga hofu kwamba kama kigezo ni kodi inayopatikana Dar basi kuna upendeleo maalum kwa Dar na Dar es salaam wanawanyonya Watanzania wenzao ambao hawaishi Dar es Salaam.  Hii inaongeza msongamano wa watu na magari Dar, na inasababisha Dar kutumia raslimali za umma kuboresha miundombinu ya Dar kuwawezesha wakazi wa Dar es salaam kuishi Dar kwa starehe.

Je, wakazi wa Dar ndio wanaolipa kodi hiyo. Walio wengi Dar hawashiriki katika uzalishaji. Ubabaishaji, uranguzi na ufisadi ndivyo vyanzo muhimu vya mapato ya wakazi walio wengi Dar es Salaam hadi jiji likaitwa Bongo. Watanzania walioko nje ya dar es Salaam walio wengi wanashiriki katika shughuli za uzalishaji. Upendeleo huu ni kukiuka katiba na huo ndio unyonyaji.

Itaendelea…

Mwandishi Dr. Kalokola Muzzammil ni mwanaharakati aliye katika ‘Mapambano ya kudumisha Fikra Sahihi za Baba wa Taifa’ anapatikana kwa namba hizi 0784 489 526 au 0713 330 633 na 0774 399 526

1 Comment
  • Safi, lakini sidhani kama unaweza kutaja majina ya watu wote waliochangia katika suala la Mtwara. Watu (mtu mmoja mmoja na makundi) waliochangia wako wengi mno. Kutaja Jina moja tu la kati ya wengiii waliotoa michango yao inaweza kuonesha kuwa unamchukia huyo mtu. Ni muhimu kujiepusha kutaja taja majina ya watu kama kweli unafanyia kazi katika taasisi fulani yenye wataamu wa kiuchumi kama Malyasia.

    Any way hiyo siyo hoja usijali umechangia vizuri, lakini hebu angalia mfano huu:

    Mkoani Rukwa ni wakulima hodari wa zao la mahindi na maharege, yakiwemo mazao mengine pia.

    Mwalimu Nyerere aliona busara wakulima hao wakawa na maghala ya kuhifadhia mazao yao katika vijiji. Alijitahidi vijiji vichache vilijengewa maghala kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo, nadhani ni wajerumani katika GTZ. Maghala hayo ya vijijini yalisaidia sana kusafirisha mahindi na kupelekwa kwemye maghala yaliyokuja kujengwa mjini Sumbawanga yaliyolenga kukusanyia na kuhifadhi akiba ya chakula katika mradi wa serikali wa usalama wa chakula (National Food Reserve).

    Tangu miaka hiyo, wakulima wa Rukwa wamekuwa wakishuhudia mahindi (yakiwa mbeki au punje zisizokobolewa) yao yakisafirishwa kwenda kusaidia mikoa yenye njaa.

    Mawazo Mgando ya serikali:

    Nyerere alianza vizuri na maghala ya kuhifadhi mahindi, nilidhani miaka ya awamu zilizofuata wangeenda hatua moja mbele zaidi ya kuongeza thamani ya mahindi hayo huko huko Rukwa na wakasafirisha unga. Serikali ingetoa maelekezo kwa shirika hilo la SGR kwa kipindi hicho kuwa ni marufuku kusafirisha mahindi au mbegu, kama shirika/serikali ingekuja na njia mbadala ya kuweka viwanda vya kusindika unga na vyakula vya mifugo. Hapo wakulima wa Rukwa wangeona umuhimu wa mahindi yao na vijana wengi wangebaki Rukwa badala ya kukimbilia ubungo. Sasa tunashuhudia mahindi/mbegu yanauzwa Tandale na machine za kukoboa na kusaga Dar es salaam halafu wanalalamika umeme hautoshi!

    Wananchi sasa wanaanza kuamka, wanaanza kukataa usafirishaji wa mali ghafi, wanataka ziongezewe thamani maeneo husika then zisafirishwe, nadhani ndiyo mawazo ya kisasa. Nadhani mashamba ya chai yameanza vizuri, sijui ni kwa sababu ya nature ya zao lenyewe au kwa nia njema. Kule Mbinga kulikuwa na Mbiku nadhani ni mifano mizuri.

    HALAFU VIONGOZI WETU WATAMBUE KUWA DAR ES SALAAM SIYO TANZANIA. ULE NI MKOA KAMA ILIVYO MIKOA MINGINE.

    TUWE MAKINI KATIKA DISTRIBUTION WAZEE

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *