Jairo, Luhango na Ngeleja wabanikwa Bungeni!

Jamii Africa
Spika Makinda

Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata la malipo ya mamilioni ya shilingi kwa watendaji wa Wizara ya Nishati ili kusaidia bajeti ya wizara hiyo ipite katikati ya mwaka huu imewasilishwa Bungeni na kuonesha kuwa malipo hayo hayakuwa halali na ulaghai mkubwa umefanyika na hivyo kutaka wahusika wawajibishwe.

Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya kupitia ushahidi wote na kuwahoji watu mbalimbali imehitimisha kuwa “utaratibu wa uchangishaji wa fedha uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini haukuwa na uhalali wowote kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.” Ripoti hiyo pia ilimtuhumu Katibu Mkuu Bw. Luhanjo kutosema ukweli kuhusu utaratibu huo. “Kamati Teule imeridhika pia kwamba huo siyo utaratibu wa kawaida kama ilivyoelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi katika Taarifa yake kwa Umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu Uchunguzi wa Awali” imesema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa fedha zilizotumika kutekeleza agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo hazikutoka kwenye bajeti yoyote iliyowekwa kwa ajili hiyo bali zilichotwa kutoka katika akaunti mbalimbali zilizokuwa zimetengewa fedha. “Nyaraka za matumizi halisi zinaonyesha kuwa fedha zilizokusanywa zimetumika kwa ajili ya malipo ya posho ya kujikimu kwa watumishi 69 wa Wizara, posho ya vikao kwa watumishi 243 waliokuwa Dodoma, manunuzi ya chakula, manunuzi ya vifaa vya kuandikia, malipo ya Takrima kwa Waziri na Naibu Waziri na manunuzi ya mafuta kwa ajili ya magari, matumizi ambayo yangeweza kugharimiwa na kasma husika za Wizara bila kuhitaji kuchangisha” imebainisha ripoti hiyo.

Hata hivyo ripoti hiyo imeonesha kuwa kinyume na madai ya awali yaliyotolewa na Mbunge Beatrice Shelukindo kuwa fedha ziliingizwa kulainisha wabunge kamati imekuta kuwa hakuna fedha iliyotumika kama rushwa kwa wabunge. Hitimisho hilo hata hivyo linaweza kuwa na utata kwani kamati teule yote imeundwa na wabunge na walitakiwa kujichunguza wenyewe! Taarifa inasema kama kwa kupita tu kuwa “Nyaraka zilizowasilishwa hazikuonyesha kuwepo kwa malipo kwa Waheshimiwa Wabunge ambayo yangeashiria rushwa” na hivyo kuwasafisha wabunge.

 

Kinyume na ilivyodaiwa na watu wengine kamati teule imekuta kwamba kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi kumwajibisha Katibu Mkuu wa wizara ya nishati na madini kilikuwa ndani ya uwezo wake. “Kamati Teule imeridhika kwamba hatua ya kufanya Uchunguzi wa Awali iliyochukuliwa na Katibu Mkuu Kiongozi dhidi ya Ndugu David Kitundu Jairo ni sahihi kwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Makatibu Wakuu wote kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, 2002 na Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003″

 

Pamoja na mambo mengine Kamati hiyo teule imeona kile ambacho tayari kilionwa kwenye Kamati Teule ya Richmond iliyoongozwa na Dr. Harrison Mwakyembe kuwa kukosekana kwa sheria ya kuwalinda watoa taarifa nyeti (whistleblowers protection act) kunazia watu kutoa taarifa za siri ” kukosekana kwa Sheria ya kuwalinda watoa taarifa (Whistleblowers) kunalinyima Taifa fursa ya kubaini na kuyashughulikia maovu
hayo kwa wakati na kwa ufanisi” Hata hivyo kamati haijaonesha wabunge wana mpango gani wa kuhakikisha sheria hiyo inatungwa mara moja hasa ikizingatiwa kuwa kimekuwa ni kilio cha muda mrefu sasa na siyo kitu ambacho kinahitaji kuoneshwa na kamati baada ya kamati wakati wao wabunge ndio watunga sheria wenyewe!

 

Katika kitu cha kushangaza hata hivyo haieleweki ni kwanini kamati teule inaamini kuwa vijana watafanya kazi vizuri zaidi na kwa uadilifu kwani mojawapo ya mapendekezo yake yanaonekana kuwapigia debe viongozi vijana kana kwamba viongozi wote waliopo sasa walianza ajira zao wakiwa wazee. Kamati inasema “Vile vile vijana wenye sifa wapewe nafasi katika ajira mpya na wastaafu kwa upande wao waandaliwe na kuhamasishwa kuanzisha shughuli katika Sekta binafsi zitakazozalisha ajira.” Maoni ya baadhi ya watu yanaona kuwa pendekezo hilo lawezekana kuwa ni kujipigia debe kwa baadhi ya viongozi vijana ambao hawajaingizwa kwenye nafasi za juu za utumishi na wanajitahidi kuwaondoa viongozi waliokaa muda mrefu.

 

Kuhusu Bw. Jairo Kamati Teule imetoa pendekezo kuwa awajibishwe. “Kamati Teule inapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa
Ndugu David Kitundu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za Serikali kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Fedha za Umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za Umma” inasema kamati hiyo katika mapendekezo yake. Hata hivyo pendekezo hilo linaweza likawa na matatizo kwa sababu tayari Bw. Jairo ameshachukuliwa hatua na Katibu Mkuu kiongozi baada ya kuchunguzwa na kusafishwa. Kitendo cha kumwadhibu tena baada ya kuchunguzwa na chombo kingine juu ya suala lile lile laweza kuwa ni kuvunja kanuni ya double jeopardy. Katika kutuliza munkari wa wabunge hata hivyo Bw. Jairo anaweza kuwajibishwa au kulazimishwa kustaafu mapema.Kamati Teule hata hivyo haisemi nani amwajibishe Jairo zaidi ya kuitaka “serikali” kufanya hivyo.

 

Vile vile Kamati teule inataka watumishi mbalimbali walioshiriki katika mchakato mzima nao wawajibishwe. “Vile vile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa Sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye Taarifa hii kushiriki kwa namna mbalimbali katika mchakato wa uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za umma.” Vile vile Kamati Teule imeipendekezea “serikali” kumchukulia hatua zinazofaa Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja. “Kwa kuwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri Waziri ndiye Msimamizi Mkuu wa Wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye kufahamu, Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, (Mb.)” imependekeza kamati hiyo.Vile viel kamati teule imependekeza kuchukuliwa kwa hatua ‘zinazofaa’ dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Bw. Utouh pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi. Kamati haikuanisha hatua zinazofaa ni zipi.

 

Mapendekezo mengine yaliyotolewa na Kamati Teule yanahusiana na mjadala wa Katiba Mpya kwani ripoti hiyo ya Kamati Teule ikisomwa vizuri inaonekana wazi kuwa hakuna sheria hasa zilivunjwa wazi au makusudi au hakuna jambo lililofanywa ambalo halikuwa ndani ya uwezo wa wahusika. Madai makubwa ni kuwa kanuni mbalimbali za utawala bora hazikufuatwa kanuni ambazo hazikuwa na nguvu sana kama ambavyo ingestahili. Hivyo, Bunge limejijikuta kwa mara nyingine likigongomelea msumari wa udhaifu wa Katiba ya Sasa na hivyo kuonesha kuwa mjadala wa Katiba Mpya una nguvu na unatakiwa kuwa wa kina zaidi kuliko ambavyo iko hivi sasa.

 

Hata hivyo kamati teule inaonekana kurudisha uwajibikaji mkubwa kwa serikali badala ya wao Wabunge ambao ndio watunga sheria wa Tanzania. Katika mapendekezo yake mengi Kamati Teule inaonekana kuitegemea serikali kufanya mambo mbalimbali badala ya kulitaka Bunge lipitishe sheria ambazo serikali ingetakiwa kufuata. Kwa kufanya hivyo bunge linaonekana kukwepa wajibu wake wa kutengeneza sheria ambazo serikali inatakiwa kuzitii na kuzifuata, sheria ambazo zingeweza kuonesha adhabu ambazo zinaweza kuwapata watendaji ambao watazikiuka lakini kinyume chake Bunge limeirudishia serikali bila yenyewe kuwajibika. Kamati Teule haijaonesha makosa yoyote ya Bunge au wabunge katika sakata hili kwani inaonekana kutumia Ibara ya 100 ya Katiba kuwalinda hata kuwalinda kuwawajibisha wabunge.

 

Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Eng. Ramo Matala Makani (Mb). Kamati Teule iliundwa na Spika Anna Makinda Augusti 24, 2011 kufuatia mjadala mkali uliohusiana na madai ya  Beatrice Shelukindo MP (CCM Kilindi) ambaye Julai 18 ambaye aliweka Bungeni kile alichokiita ni barua iliyoonesha kuwa Bw. David Jairo kuwa ametumia madaraka. Katika maelezo yake Bi. Shelukindo alidai kuwa utaratibu uliotumika kukusanya fedha kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kwenda akaunti za GST Dodoma kuwa ulikuwa na walakini na kwa vile kiasi kilichodaiwa cha shilingi bilioni 50 kilisababisha maneno makali. Ni kutokana na hilo ndio uchunguzi wa awali ulifanyika ambapo Katibu Mkuu kiongozi alimsafisha Jairo ambaye alipokewa kwa mbwembe na Waziri wake pamoja na gari lake kusukumwa na watumishi ambao waliona kuwa ameonewa. Kitendo hicho kiliwaudhi zaidi wabunge ambao waliona kuwa wamedharauliwa na siku moja baadaye hoja ilitolewa ya kuundwa kwa Kamati Teule na matokeo yake baada ya uchunguzi walifikia hitimisho ambalo kwa wengi wao lilikuwa tayari limefikiwa kabla hata ya uchunguzi.

 

Sasa hivi mpira umepelekwa kwa “serikali” na haifahamiki ni hatua gani zitachukuliwa kwani Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora Bw. Mathias Chikawe ameliambia Bunge kuwa serikali itachukua hatua stahiki baada ya kupitia mapendekezo hayo na kama uchunguzi wa Richmond ni dalili ni wazi kuwa hatua kali zaidi haziwezi kuchukuliwa zaidi ya barua za maonyo au hatua nyingine za ndani za kinidhamu. Kwenye sakata la Richmond Kamati Teule ilitoa mapendekezo kama haya lakini serikali haikuchukua hatua kali kwani karibu watumishi wote waliotakiw akuwajibishwa wameendelea na nafasi zao baada ya kuitwa na kutoa maelezo pamoja na kuandikiwa barua za nidhamu na si zaidi ya hapo.

 

Kupata nakala ya Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata hili BONYEZA HAPA

 

Na. M. M. Mwanakijiji

 

 

 

 

2 Comments
  • Shida ya speaker wa Bunge nimoja anpotoa maoni ana base only on one side of CCM haya yote nikwamba anatetea kibarua chake.not knowing that She is working for Tanzanian but not only Kikwete and THE CCM MPS.

  • the problems iz baadhi ya viongoozi wa chama cha mafisadi ni kwamba they dont belive in GOD .ndo maana wanattenda hayo wayatendayo hawakumbuki hata kiapo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *