CHADEMA wakataa kushiriki mchakato wa Katiba; Waunda tume kukutana na Kikwete

Jamii Africa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hakitokuwa tayari kushiriki katika mjadala wa kukusanya maoni kuhusiana na Katiba Mpya chini ya Tume ya Rais endapo sheria iliyopitishwa na Bunge kusimamia mchakato huo haitafanyiwa mabadiliko makubwa. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Freeman Mbowe katika tamko la Kamati Kuu ya CDM iliyotolewa mapema leo.

Katika taarifa yake kwa umma Bw. Mbowe amesema kuwa “ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo”

Pamoja na uamuzi huo Bw. Mbowe aliendelea kuonesha kuwa mswada mzima ambao wabunge wake waliupinga Bungeni umejaa mambo ambayo yanaonesha kuwa mchakato mzima wa kupata katiba mpya utakuwa unasimamiwa na kuipendelea CCM. “Sheria inaunda Bunge la Katiba ambalo litakuwa na Wajumbe hadi 400 wa CCM kati ya wajumbe 545 wa Bunge la Katiba. Idadi hii ya wajumbe itaiwezesha CCM kupata theluthi mbili ya wajumbe wanaohitajika chini ya Sheria hii ili kupitisha jambo lolote katika Bunge la Katiba na kwa hiyo Katiba Mpya itakuwa ni ile inayolingana na matakwa na maslahi ya CCM na itakuwa mpya kwa jina tu” imesema taarifa hiyo ya Mbowe.

Pamoja na hilo CDM imedai kuwa mswada uliopitishwa ili uwe sheria “unampa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mamlaka makubwa ya kuunda Tume ya Katiba na Sekretarieti yake ambayo sio tu itakusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti, bali pia ndiyo itakayoandaa na kuandika Rasimu ya Katiba Mpya na kusimamia mchakato wote wa wananchi kuijadili na kuipitisha katika Bunge la Katiba”

Baadhi ya vitu vingine ambavyo vinakataliwa na CDM kuhusu mswada huo ni kuwa sheria hiyo “inampa Rais na Mwenyekiti wa CCM mamlaka makubwa sio tu ya kupokea ripoti ya Tume ya Katiba bali pia ya kuifanyia mabadiliko ambayo yeye na Serikali yake wataona yanafaa kwa kutumia taratibu za kiserikali za kutunga sheria”

CDM imedai pia kukosa imani na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo kwa mujibu wa sheria hii imepewa jukumu la kusimamia kura ya maoni kuhusu pendekezo la Katiba Mpya. Akionekana kukumbushia udhaifu wa tume hiyo wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge wa mwaka 2010 Bw. Mbowe amesema kuwa “sheria (iliyopitishwa) inaipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoteuliwa na Rais na Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kusimamia mchakato mzima wa kura ya maoni ya kuipa Katiba Mpya uhai wa kisheria. Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina uhuru na imeshindwa mara nyingi kusimamia chaguzi huru na haki katika nchi yetu na haiwezi kusimamia kura ya maoni kwa uhuru unaohitajika”

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimemlaumu Rais Kikwete moja kwa moja kwa kukoleza tofauti za kisiasa badala ya kujaribu kuwaleta Watanzania pamoja. “Kamati Kuu imeshangazwa na kusikitishwa na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kutozitumia fursa hizo na badala yake kujiingiza katika jalala la taka za upotoshaji uliofanywa na Wabunge wa chama chake juu ya misingi na maudhui ya Sheria hiyo. Kamati Kuu inaamini kwamba badala ya kuwaunganisha Watanzania na kujenga muafaka unaohitajika katika mchakato wa Katiba Mpya, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa CCM wa Dar es Salaam imezidi kuwagawa Watanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama badala ya kuwaunganisha kwa misingi ya utaifa” amesema Bw. Mbowe.

Pamoja na hayo yote CDM imesema kuwa itaendelea na kutoa elimu kwa wananchi kudai sheria bora na mfumo bora wa kukusanya maoni na vile vile kuendelea kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi. Hivyo “Kamati Kuu inawaagiza wabunge na viongozi wote wa chama katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi” imesema taarifa hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kufuatia mkutano wa Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika siku ya Jumapili kwenye hoteli ya Mbezi Garden Jijini Dar-es-Salaam.

Vile vile kamati imelaani vikali uamuzi wa jeshi la polisi kupiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa ikidai kuwa jeshi limeingilia na kuondoa uhuru wa wananchi. “Kamati Kuu inasikitishwa na msimamo huu wa Serikali ya CCM kwani unashindwa kutambua ukweli kuwa matumizi ya nguvu za dola hayajawahi kuokoa serikali za kidikteta kuondolewa madarakani na Katiba Mpya kupatikana katika nchi mbali mbali duniani na katika Bara la Afrika”

Katika hitimisho lake Bw. Mbowe amesema kuwa “Kamati Kuu inasisitiza kwamba CHADEMA itaendelea kutumia njia zote za amani, ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoainishwa na Katiba na sheria husika za nchi yetu kuunganisha nguvu ya umma kupinga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mchakato wake utakaopelekea Tanzania kutopata Katiba Mpya na bora”

Wakati huo huo Kamati Kuu ya CDM imeunda kamati ndogo ya viongozi wa CDM ambao watatafuta nafasi ya kukutana na Rais Kikwete ili kumpatia mapendekezo yao ya nini cha kufanyika. Kwa mujibu wa Mbowe tume hiyo itapeleka mapendekezo kwa Rais na kama Rais na siyo mwenyekiti wa CCM na endapo atakubali mapendekezo hayo basi watashiriki mjadala huo lakini kama atakaa basi watarudi kwa wananchi.

 

Na. M. M. Mwanakijiji

VIDEO

TAMKO LA CHADEMA NOV 21, 2011

1 Comment
  • mbowe tuliza ball sisi CCM tukuandalie katiba hata kama ungekuwa wewe unatawala ungekubali ccm wakuandalie katiba tuwe wakweli tu kikwete kaza buti achana na akina mbowe hawa wanataka kututawala wakati hawakushinda urais wasubiri wakati wao kwa sasa tuwaandalie katiba tunayoitaka sisi wana ccm

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *