UCHUMI WA VIWANDA: Dhana, maana na uzoefu wa wasomi wetu

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa ukosekana kwa sera, mipango na mikakati inayotafsiri dhana ya uchumi wa viwanda kunaweza kuikwamisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Ikumbukwe kuwa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ilipoingia madarakani mwaka 2015 ilibeba kaulimbiu ya kujenga uchumi wa viwanda jumuishi ili kuongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi.

Lakini kumekuwa na tafsiri, utata na uelewa tofauti wa dhana ya uchumi wa viwanda ambayo serikali inaitekeleza. Kutokana na hali hiyo, Kavazi la Mwalimu Nyerere liliandaa mjadala wa wasomi ili kubadilishana uzoefu wa kihistoria ya Tanzania ya ujenzi wa viwanda.

Akizungumza katika mjadala huo, Prof. Severine Rugumamu amesema kuwa nchi imekosa dira jumuishi ya kujenga uchumi wa viwanda ambapo wananchi hawajaelimishwa na kujulishwa dhana nzima ya viwanda na misingi yake katika kukuza uchumi wa nchi matokeo yake wanajengewa matumaini hewa.

“Tunaendelea kuwa na matumaini hewa, pamoja na viwango vya ukuaji wa uchumi,hatuna sera, mipango na mikakati jumuishi ya kujenga uchumi wa viwanda”, amesema Prof. Rugumamu.

Ameeleza kuwa uzoefu alionao juu ya maendeleo ya viwanda duniani, hatua ya kwanza ni kuwaunganisha wananchi wote wawe katika mwelekeo unaofanana kama alivyofanya Mwalimu Nyerere wakati wa utekelezaji wa sera ya Ujamaa ambapo aliweza kuwaunganisha wananchi wote katika mapambano dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi.

“Mwalimu Nyerere alifanikiwa kupinga ujinga, umasikini na maradhi kwasababu aliwaunganisha wananchi wote kuboresha maisha yao. Kukua kwa uchumi wa viwanda kunawezesha ukuaji wa uzalishaji katika sekta ya kilimo na pato la nchi lakini tumeshuhudia ukuaji wa viwanda kwa asilimia 2 mwaka 1961 lakini miaka 20 iliyofuata ukuaji huo ulifikia 5%”.

Amefafanua kuwa kukosekana kwa dira ya kitaifa ya viwanda ni matokeo hafifu ya utashi wa kisiasa wa viongozi ambao wamekosa maono na nadharia tunayopaswa kuifuta kama nchi katika fungamano la sekta mbalimbali ambazo zinaweza kuchangia ukuaji wa viwanda vya ndani ili kupata soko la uhakika la bidhaa zitakazozalishwa.

Ameongeza kuwa changamoto inayowezwa kutukwamisha kwenye safari ya uchumi wa viwanda ni msisitizo uliowekwa wa kuzalisha bidhaa zitakazouzwa katika soko la ndani na kusahau soko la nje ambalo ni kubwa zaidi na lina manufaa ikiwa litawekewa mikakati mizuri ya kidiplomasia. 

Akitolea mfano wa Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025) ambayo moja ya lengo lake ni kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati, amesema dira hiyo haina nguvu ya kisiasa ya utekelezaji kufikia kule tunakotaka kufika.

“Dira ipewe kipaumbele cha usalama wa taifa sio tu kupunguza umasikini. Mageuzi ya kiuchumi ni jukumu la kisiasa na taasisi za serikali ndizo zina mamlaka ya kusimamia sera na utekelezaji wake”, amesema Prof. Rugumamu.

Kutoeleweka vizuri kwa sera na mipango iliyopo ya viwanda kumeifanya serikali kushindwa kusimamia jukumu lake la kukuza uchumi wa viwanda na kuiachia sekta binafsi kutawala soko na kujipatia faida mara dufu.

Amehitimisha kwa kusema msingi  wa serikali kuhusika moja kwa moja katika dhana ya viwanda lazima ujikite kwenye kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, nishati na kujenga viwanda mama vitakavyozalisha malighafi na nyenzo za kuzalisha bidhaa zingine za viwandani.

                               Fungamano la kilimo na viwanda; njenzo muhimu kuelekea uchumi wa viwanda

 

Wasomi watoa neno

Akichangia katika mjadala huo wa uchumi wa viwanda, Mwenyekiti mstaafu wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Prof. Isaa Shivji amesema, changamoto zinazojitokeza kwenye sera ya viwanda ni kutokuwepo kwa uwajibikaji na uwazi wa wanaobeba gurudumu la maendeleo ya taifa.

Amesema wakati wa Azimio la Arusha, wananchi wote walihusishwa kwenye utekelezaji wake na kila mtu alifahamu wazi majukumu yake ambapo wakulima na wafanyakazi walipewa kipaumbele kwenye kutengeneza mustakabali wa taifa.

Ameongeza kuwa mjumuiko huo uliwezesha kuwa na fungamano thabiti la sekta za kilimo na viwanda ambazo zilikuwa zinategemeana katika uzalishaji na kukuza pato la taifa.

Kwa upande wake, Prof. Wole Soyinka amesema uelewa hafifu wa sera na mikakati ya kuendesha viwanda miongoni mwa viongozi na wananchi ni changamoto nyingine inayokwamisha dira inayoongoza uchumi wa viwanda.

Washiriki wa mjadala huo wamesisitiza mambo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa itikadi, kuimarisha sekta ya umma, kuongeza wataalamu, ushirikishwaji wa wadau wote wa maendeleo na dira moja ya maendeleo ya viwanda.

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu ch Dar es Salaam (UDSM), Prof. Humphrey Moshi amesema mafanikio ya viwanda lazima yaendeshwe na itikadi moja inayoeleweka kwa wananchi wote ikizingatiwa kuwa Tanzania hatuna itikadi inayoeleweka maana kwa upande mmoja tunafuata sera za ujamaa na wakati huohuo tunatekeleza matakwa ya ubepari.

“Tutengeneze itikadi na falsafa ya kuongoza uchumi wa viwanda. Serikali iingie na kusimamia vizuri sekta ya umma na binafsi ili kujenga msingi mzuri wa viwanda”, amesema Prof. Moshi.

Naye, Mhadhiri wa zamani wa UDSM, Prof. Samuel Wangwe amesema ukuaji wa viwanda unategemea maendeleo mazuri ya kilimo ambapo ameishauri serikali kuimarisha mfumo wa utendaji wa kilimo na kukuza teknolojia ya uzalishaji zana na bidhaa za viwandani.

Akihitimisha mjadala huo, Prof. Rugumamu amesema sera, mipango na mikakati ipewe kipaumbele ili kukuza uelewa wa wananchi kuelekea uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *