TAHADHARI: Mafuta ya lavenda, chai huchochea wanaume kuota matiti

Jamii Africa

Pamoja na kukosekana kwa idadi kamili, lakini ukweli ni kuwa Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zingine, kumekuwepo ongezeko la wavulana na hata wanaume, kuonekana kuwa na matiti makubwa.

Kawaida, maumbile ya wanaume hayaruhusu kuwa na matiti makubwa. Kwanza yawepo kwa ajili gani?

Matiti makubwa ni maumbile ya wanawake, wanapopevuka na hii hutokea kwa sababu maalum, kwamba msichana anakuwa tayari amebalehe.

Kubalehe kwa msichana na kuanza kujenga dalili za kuwa mama, basi mwili wake hubadilika, ikiwamo kuota matiti ambayo ni ‘kiwanda’ cha maziwa kwa ajili ya kunyonyesha mtoto.

Sababu za wanaume kuota matiti zimekuwa zikikanganya; watu wa kawaida na hata wanasayansi,  hata hivyo katika siku za hivi karibuni, matokeo ya utafiti ulifanywa Marekani yamekuja na sababu ya kisayansi.

Utafiti huo unaonesha kuwa wanaume kuota matiti huchochewa zaidi na matumizi ya mafuta ya mti na hata maua ya lavenda pamoja na mti wa chai.

                   

Mmea wa Lavenda unaotajwa kuchochea uotaji wa matiti kwa wanaume

 

Taasisi ya Mazingira ya Sayansi ya Afya ya Marekani (NIEHS) katika utafiti wake imebaini kuwa kemikali katika mafuta hayo huchochea ongezeko la homoni za kike na kuharibu homoni za kiume kwa wanaotumia.

Uhusiano kati ya ukuaji wa matiti kwa wanaume na matumizi wa mafuta ya mti wa lavenda na ule wa chai, unaonesha kuwa kemikali nane zinazopatikana katika mafuta ya miti hiyo uharibu kazi za homoni za kiume.

Mafuta ya mimea hiyo hupatikana katika bidhaa tofauti kama vile sabuni, mafuta ya kujipaka, mafuta ya kuosha nywele pamoja na bidhaa za kutengeza nywele za bandia.

Kemikali hizo zilichunguzwa maabara kwa kuwekwa ndani ya mwili wa binadamu ili kuona ni kwa kiasi gani zinathiri homoni za ‘estrojeni’ na ‘testosteroni.’

Watafiti walibaini kwamba mafuta hayo yamekuwa yakichochea ongezeko la homoni za kike na kuharibu zile za kiume.

Watafiti kutoka NIEHS kwa mara ya kwanza waligundua ushahidi wa madai haya mwaka 2007 ambapo walifanya utafiti wao kwa watoto wa kiume watatu ambao walikuwa wameanza kuota matiti kabla ya kufika kwenye kipindi cha kubalehe.

Watoto hao hawakuwa na matatizo yoyote kiafya, lakini wote walikuwa wakitumia mafuta au bidhaa zenye mafuta ya lavenda na mchai ndani yake. Na pale walipopewa maelekezo ya kuacha kutumia mafuta hayo, ukuaji wa matiti yao ulikoma. 

Hivyo matokea ya utafiti yakahitimishwa kwamba kemikali ndani ya mafuta hayo huharibu homoni mwilini ambapo huongeza homoni ya estrojeni na kupunguza kiwango cha testosteroni na hali hiyo huchochea matiti kukua.

Daktari Tyler Ramsey kutoka taasisi ya NIEHS katika jimbo la Carolina Kaskazini, amewatahadharisha wananchi kuhusu matumizi makubwa ya mafuta ya lavenda na chai, ili kupunguza madhara ya kuota kwa matiti kwa wanaume.

''Jamii yetu huona mafuta hayo ya asilia kuwa yako salama. Hata hivyo, yana kiwango kikubwa cha kemikali, ni sharti yatumiwe kwa tahadhari kwa kuwa husababisha uharibifu wa homoni.''

                               Mti wa chai nao watajwa kuwa na kemikali zinaweza kusababisha uotaji wa matiti kwa wanaume usio wa kawaida

Prof. Ieuan Hughes, ambaye ni profesa wa magonjwa ya watoto katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza alisema kuwa matokeo hayo yamethibitisha ni kwanini mtu binafsi anayetumia mafuta hayo yalio na kemikali hizo huota matiti.

Madhara dhidi ya homoni za kiume huwa hayatarajiwi na haiwezekani kuyazungumzia bila kuwa na matokeo ya utafiti wa kisayansi.

“Ni kweli kwamba siyo watu wote wanaotumia mafuta hayo huathirika, hivyo basi ni wazi kwamba kuna watu ambao ni rahisi kuathiriwa na kemikali za mafuta hayo, ama pengine wanatumia bidhaa hiyo kupitia kiasi”.

Hata hivyo, bado utafiti zaidi unahitajika kuhusu matokeo hayo kutokana na kuwa baadhi ya wataalamu bado hawazikubali na kudai kwamba ni matokeo ambayo yamezushwa, kwani idadi ya watu waliofanyiwa utafiti ni ndogo sana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *