Wakulima wa chai Kagera wamkalia kooni mwekezaji kuboresha maslahi yao

Jamii Africa

Serikali imesema kuwa haitasitisha mkataba na Mwekezaji wa Kampuni ya Chai Maruku, iliyoko mkoani Kagera, kwa sababu mgogoro wa malipo uliopo baina ya  kampuni hiyo na wakulima pamoja na wafanyakazi wake unaelekea kutatuliwa.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji , alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Jason Rweikiza (CCM), aliyetaka kujua sababu za Serikali kutovunja mkataba na mwekezaji huyo na kurejesha umiliki kwa Serikali au kwa mwekezaji mwingine atakayejali maslahi ya wakulima na wafanyakazi.

Katika swali lake la msingi, Mhe.   Rweikiza alisema kuwa tangu Kampuni hiyo ibinafsishwe kwa mwekezaji, kumekuwa na malalamiko ya wakulima kutolipwa  fedha za mauzo ya chai kwa wakati na wafanyakazi kutolipwa  mishahara na stahiki zao ipasavyo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, katika kutatua mgogoro huo Serikali kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utendaji na uendeshaji wa Kampuni hiyo kwa kufanya vikao kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai (TASHTIDA).

Alisema kuwa katika vikao hivyo haki ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala la haki za wafanyakazi pamoja na madai ya wakulima, ambapo mpaka sasa mwekezaji amekubali kulipa madai ya wakulima kiasi cha Sh. milioni 12 huku wakiendelea kujadili namna ya kutatua suala la madai ya wafanyakazi.

Dkt. Kijaji aliahidi kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha haki za wakulima na wafanyakazi hazipotei. Pia wakulima kulima kilimo bora cha chai kitakachowanufaisha kiuchumi na kijamii.

                        Wakulima wakivuna chai

 

Chai na changamoto zake

Utafiti iliofanywa na watafiti mbalimbali kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania kwa ushirikiano na Jumuiya ya Ulaya (EU) mwaka 2012  katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ulibaini kuwa wakulima wanatakiwa kuelimishwa zaidi  juu ya njia bora za kulima zao hilo ili kuongeza uzalishaji na faida.

Katika utafiti wao waliwaelimisha wakulima katika kutambua na kukabiliana na changamoto mbalimbali, ambapo pia walikiri  kuwa zao la  chai endapo likilimwa, kuhudumiwa na kuuzwa katika soko sahihi litawakomboa wananchi na kuliingizia taifa kipato.

Kabla ya utafiti huo, wakulima wengi katika wilaya hiyo walikata tamaa kutokana na kupata hasara baada ya kuuza chai kwa bei ndogo.

Mtafiti wa zao la Chai katika wilaya ya Mufindi, Prof.  Bruno Ndunguru akizungumzia hali halisi ya kilimo cha chai alisema walibaini kuwa udongo kukosa rutuba mbadala kwa zao la chai, ambapo wakulima hao walitumia mbolea ya kupandia na kukuzia, swala ambalo lilipelekea kuharibika kwa ardhi na hatimaye kukosa kabisa rutuba kwa zao la chai.

Prof. Ndunguru alisema katika hatua za kwanza, EU ilisaidia kujenga majengo mapya ya ofisi ambazo zitatumika na watafiti wa kilimo hicho na wakulima wadogo wadogo wa Mufindi.

” Utafiti wetu ulihusisha zao la chai kwa kutafuta aina mpya ya mbegu na miche ya kupandwa, uwezo wa kusambaza maji katika mashamba ya chai, rutuba sahihi ya ardhi na kujenga ofisi za kutosha kwa ajili ya kazi nzima ya utafiti,” alisema Prof. Bruno.

Alibainisha kuwa katika kufanya kazi ya kutafiti udongo na ardhi sahihi kwa kilimo cha chai wamehakikisha unapimwa katika maabara za kilimo, kutoa ushauri wa matumizi sahihi ya ardhi kwa wakulima wa chai, kutoa taarifa za maeneo ambayo wakulima walitumia mbolea za chumvi pamoja na kuhamasisha masoko yanayonunua chai.

Katika mwaka wa 2001 hadi 2004 mradi wa utafiti uliwahusisha wakulima wa chai 4,350,364 ambapo katika mwaka wa 2005 hadi 2008 wakulima walikuwa 13,987,901 na kuanzia mwaka 2009 hadi 2012  idadi ya wakulima iliongezeka maradufu,  hali ambayo inahamasisha EU waendelee kutoa misaada zaidi ya pesa kuwakomboa wakulima wa chai.

Mkulima wa chai katika wilaya hiyo, Emmanuel Lugano, alisema kutokana na kulima kilimo cha kisasa baada ya watafiti kufanya utafiti wa chai sasa wanaweza kuwa na uhakika wa maisha ikiwemo kusomesha watoto na kuboresha maisha yao.

“Awali sisi wakulima tulikata tamaa kabisa kuendelea kulima chai, utafiti uliofanywa na watafiti hawa, umetukomboa kutokana na sasa tunalima kilimo bora, tunapata soko la uhakika na tunaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kiuchumi tofauti kabisa na hapo awali tukipata hasara”, amesema Lugano.

                                         Chai inapitia mchakato mrefu katika usindikaji

 

Asili ya Chai

Asili ya chai bado haijajulikana hasa ni wapi japokuwa inaaminika chimbuko lake ni China. Nchi  zinazozalisha chai kwa wingi kwa sasa ni China, Japan, Indonesia na Kenya ikiwa nchi ya tatu kwa uzalishaji baada ya India na Sri  Lanka.

Kwa upande wa Afrika, Tanzania ni nchi ya nne baada ya Kenya, Malawi na Uganda ambapo inalimwa katika mikoa ya Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Njombe na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga. Inakadiriwa kuwa Tanzania huzalisha tani 32, 000 kwa mwaka ambapo husindikwa katika viwanda vilivyomo nchini na nyingine husafirishwa nje ya nchi.

Kuna aina mbili za chai ambazo ni China Tea (Camellia Sinensis) na Assam Tea ambazo hustawi katika maeneo tofauti kulingana na hali ya hewa ya eneo husika. Chai hustawi vizuri  katika maeneo yenye mvua za wastani (1500- 2500mm) lakini inaweza kukua pia katika maeneo ambapo hakuna mvua  kubwa sana yaani milimita 1200 na joto lidi la 18 – 20°C .

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *