NBS yashauriwa kuondoa utata wa takwimu za uchumi nchini

Jamii Africa

Wataalamu wa Shirika la Kimataifa la fedha (IMF) wameishauri Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia na kuondoa utata wa takwimu za ukuaji wa uchumi ilizozitoa hivi karibuni ambazo zimeibua mjadala katika jamii.

Takwimu hizo ni zile zinazohusu kuimarika kwa uchumi wa Tanzania ambapo katika nusu ya kwanza ya 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.8. Lakini kutolewa kwa takwimu hizo kuliwaibua wananchi na wanasiasa akiwemo Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini aliyetofautiana nazo na kudai kuwa uchumi wa Tanzania unasinyaa.

Wataalamu hao wa IMF wakiongozwa na kiongozi wao, Mauricio Villafuerte walifanya ziara ya kikazi nchini kuanzia Novemba 30 hadi Disemba 12 mwaka huu na kukutana na watendaji wa serikali chini ya Programu yenye dhima ya kusimamia Sera za Kiuchumi (PSI) na mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa taasisi za fedha ili kufikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Katika taarifa iliyotelwa na IMF, Mtaalamu Villafuarte amesema data za awali zinaonyesha uchumi umeimarika kwa asilimilia 6.8 lakini changamoto inajitokeza ni matumizi ya serikali yasiyoendana na makusanyajo ya kodi, kushuka kwa utendaji wa sekta binafsi na kuyumba kwa mikopo inayotolewa na benki za biashara.

Amesema viashiria hivyo vya kiuchumi vinaweza kuathiri mwenendo wa uchumi na kusababisha kushuka kwa kiwango hicho hatua zisipochukuliwa.

“Mavuno mazuri yaliyopatikana mwaka huu yameongeza upatikanaji wa chakula, yamepunguza mfumuko wa bei ya mazao na kushusha kiwango cha mfumuko kwa asilimia 4.4 mwezi Novemba kikiwa chini ya asilimia 5 ya mamlaka za fedha ambazo zinakusudiwa kuwa na uchumi wa kati", amesema.

Amebainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania izisaidie benki ambazo zinashindwa kujiendesha ili ziweze kukopesha sekta binafsi ambayo inategemea mikopo kama dhamana ya kuzalisha bidhaa mbalimbali.

                          Rais John Magufuli (mwenye shati jeusi) alopotembelea kiwanda cha Mfanyabiashara Said Bakhresa hivi karibuni.

Kwa nyakati tofauti wadau wa sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia serikali juu ya mlundikano wa kodi ambazo hauendani na gharama za uzalishaji kwani umekuwa ukiathiri soko na mitaji ya sekta hiyo.

Hali hiyo imechangia kuyumba kwa utolewaji wa mikopo ya benki kufuatia kupanda kwa gharama za uendeshaji wa shughuli za taasisi za fedha ambazo hutegemea mapato ya riba za mikopo na kuhifadhi fedha.

Ili kuokoa uchumi wa nchi, sekta binafsi inaendelea na mazungumzo na serikali ili kutafuta namna nzuri ya kufanya biashara itakayozifaidisha pande zote mbili.

Hata hivyo, serikali imesema benki zote ambazo hazifanyi vizuri zinapaswa kufungwa. Msimamo huo unayofautiana na ushauri uliotolewa na IMF wa kuziwezesha benki za biashara kuendesha shughuli zake ili kuinufaisha sekta binafsi.

Kauli ya Rais Magufuli

Akifungua tawi la benki ya CRDB mjini Dodoma, rais John Magufuli ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuzifungia benki zote zilizoshindwa kujiendesha na kubaki na benki chache ambazo zinaweza kuhimili ushindani wa soko.

"Niwaombe BoT, Mabenki ambayo hayafanyi vizuri msisisite kuyafungia na kuacha mambo ya kubebanabebana. Ni bora kubaki na Benki 5 zinazofanya vizuri kuliko kuwa na Benki nyingi zisizo na tija", amesema Rais. 

Pia emeitaka BOT kukamilisha Sera ya riba ili taasisi zote fedha ziwe na riba zinazolingana na kutafuta namna ya kuongeza ushirika na benki zinazofanya vizuri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *