Kanuni mpya za Madini kushusha uzalishaji wa dhahabu hadi 0% ifikapo 2027

Jamii Africa

Kuanza kutumika kwa sheria Mpya za madini, kanuni na ukaguzi wa kampuni za madini kunatajwa kupunguza uzalishaji wa madini ya dhahabu na uwekezaji nchini.

Kwa mujibu wa shirika la utafiti BMI linatabiri kuwa wastani wa uzalishaji wa dhahabu kwa mwaka utashuka hadi asilimia sifuri (0) katika ya 2018 na 2027, kutoka 2.4% ya kipindi kilichopita.

Wanatabiri kuwa kiwango cha ukuaji wa sekta ya madini hakitakuwa cha kuridhisha kwa miaka ijayo kutokana na Serikali kufanya mabadiliko ya sheria na kanuni za uchimbaji madini ambazo zinadaiwa  kudhoofisha mazingira ya utendaji wa sekta hiyo, kuzuia uwekezaji wa sasa na baadaye.

Mnamo Februari 20 mwaka huu, Serikali ilitangaza kuweka vikwazo kwa benki za kigeni, kampuni za bima na sheria zinazimamia na kufadhili sekta ya madini.

Kwa kutumia kanuni hizo mpya itakuwa ni lazima kwa kampuni yoyote ya madini kufanya kazi na benki za ndani ambazo kwa sehemu kubwa zinamilikiwa na watanzania; na kampuni za bima na uwakili (sheria) kama sehemu ya malengo ya Serikali kuchochea ukuaji wa sekta zilizopo nchini.

Vikwazo hivyo vimekuja baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya madini mwaka jana ambayo inazuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu na serikali kufanya mazungumzo juu ya mikataba iliyoingia na makampuni ya madini; kwasababu Rais John Magufuli amedhamiria kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Ndani la Taifa (GDP) kwa asilimia 10 ifikapo 2025.

 

 

Hali halisi ya uzalishaji wa dhahabu…

Kulingana na jalida la Further Africa ambalo limejikita katika uchambuzi wa sekta ya madini katika nchi za Afrika, linaeleza kuwa utafiti wa BMI umetoa utabiri wake kwasababu ya viashiria vinavyojitokeza kwenye uzalishaji wa dhahabu ambavyo ni matokeo ya maamuzi ya baadhi ya kampuni za madini nchini kuanza mchakato wa kuuza mali na hisa zao kufuata masharti mapya yaliyowekwa na Serikali ambayo yanadaiwa kutokuakisi mazingira mazuri ya uwekezaji.

Mathalani, kampuni ya madini ya Acacia, mzalishaji mkubwa wa dhahabu nchini, ambayo mwanzoni mwa mwezi Machi, 2018 ilitangaza kuingia ubia na wawekezaji wengine kwa kuuza baadhi au sehemu yote ya shughuli zake nchini Tanzania.

Acacia ilifikia uamuzi huo kutokana na matokeo ya awali yaliyoshuhudiwa mwanzoni mwa mwaka huu ambapo ilitangaza kupata hasara ya Dola za Marekani milioni 707 kwa mwaka 2017, kwasababu Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini Machi, 2017 kupisha uchunguzi uliogundua kuwa kuna upotevu mkubwa wa mapato unaotokana na kukwepa kodi.

Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo ili kutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara lakini wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa Acacia hawajakubaliana na matakwa ya Tanzania ambayo yanadaiwa kuididimiza kampuni hiyo.

Inaelezwa kuwa kampuni za madini ya dhahabu ya Shandong na Zijing Mining zinafanya mazungumzo ya kuingia ubia na Acacia au kununua mali zote za kampuni hiyo zilizopo Tanzania.

Hata kama Acacia ikiuza sehemu ya mali zake haitaathiri moja kwa moja uzalishaji wa ndani wa madini lakini kitakachotokea ni kuyumba kwa usambazaji wa madini kwasababu ya mabadiliko ya umiliki wa makampuni.

Jambo ambalo si ishara nzuri kwa Tanzania ni kuwa, maamuzi ya Acacia yanaweza kuathiri sekta ya uwekezaji nchini kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa dhahabu unachukua asilimia 90 ya sekta madini.

Kwa upande wake, Kampuni ya madini ya Anglogold inayomiliki mgodi wa  dhahabu wa Geita inatarajia kufanya mazungumzo na Serikali ili kuelezea ni kwa kiasi gani sheria za madini zitakavyoathiri utendaji wa kampuni hiyo siku zijazo.

Taarifa zilizopo ni kwamba Anglogold tayari imewasilisha malalamiko yake kwa mabaraza ya usuluhishi ya kimataifa juu ya kanuni hizo mpya ambazo zimetungwa na kuanza kutumika wakati kampuni za madini ziliingia makubaliano na sheria za zamani. Na kuna hatari kubwa ya kampuni hiyo kuondoka nchini ikiwa haitakubaliana na Serikali juu ya masharti mapya.

Zaidi ya hapo, kampuni ya dhahabu ya Katoro inayoendesha miradi ya uchimbaji wa dhahabu katika maeneo ya Imweru na Lubando yaliyopo nje kidogo ya jiji la Mwanza, Machi mwaka huu ilitangaza kusimamisha shughuli zake kwenye mradi wa Imweru ili kufanya tathmini ya kiuchumi na uwekezaji kutokana na ujio wa kanuni mpya za madini.

Matokeo yake, utafiti wa BMI unatabiri kuwa uzalishaji wa dhahabu nchini Tanzania, ambao ni asilimia 90 ya sekta yote ya madini, utashuhudia anguko la ukuaji kwa wastani asilimia sifuri (zero average groth rate) katika ya 2018 na 2027, kutoka 2.4% ya awali.

Serikali imetakiwa kutathmini maamuzi yake na kuzipitia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya madini ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa kwenye pato la taifa na ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa kurekebisha hali iliyopo sasa inaweza kuathiri mfumo wa ukusanyaji mapato na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

1 Comment
  • Ni vema tu yakapungua kuchimbwa kuliko kuchimbwa kwa hasara. Madini hayaozi. Utafika wakati tutayachimba kwa faida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *