Benki ya Dunia yatoa Ofa barabara ya Serengeti

Jamii Africa

Benki ya Dunia imetoa ofa nzito kwa serikali ya Rais Kikwete of ambayo itakuwa ni vigumu serikali kuikataa. Ofa hiyo ni katika kuitika serikali kusitisha mpango wa kujenga barabara ya changarawe ndani ya mbuga za Serengeti na badala yake benki hiyo iko tayari kugharimia ujenzi wa barabara nyingine itakayopita pembezoni mwa hifadhi hiyo maarufu zaidi nchini.

Habari za pendekezo hilo zimeripotiwa na jarida mashuhuri la mazingira la The Ecologist duniani siku ya Alhamisi ambapo jarida hilo lilisema kuwa Benki ya Dunia imetaka serikali kusikiliza malalamiko ya wadau mbalimbali wa mazingira ambao wanaona njia ya sasa ya barabara hiyo inatishia uhamaji maarufu wa pofu, digidigi na pundamilia kutoka Tanzania kwenda Kenya kila mwaka na kuonekana kama mojawapo ya vivutio vikubwa vya asili vya utalii.

Kila mwaka wanyama kwa maelfu yao huama kutoka mbuga ya Serengeti iliyoko Tanzania na kwenda mbuga ya Masai Mara ya Kenya wakifuata majani na maji na baadaye kurudi. Wanamazingira mbalimbali duniani wamekuwa wakiendesha kampeni kali ya kuzuia barabara mpya ndani ya mbuga hiyo ambayo ingefupisha safari ya magari ndani ya mbuga hiyo na kurahisisha usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma mbalimbali kutoka upande mmoja wa jamii zinazozunguka mbuga hiyo kwenda upande mwingine.

Chama cha Mambo ya Mbuga cha Frankfurt (Frankfurt Zoological Society) kimedai kuwa endapo barabara hiyo iliyopendekezwa na serikali itajengwa kama ilivyokusudiwa kiasi cha pofu milioni 1.3 wanaohama kila mwaka watapungua na kufikia idadi ya pofu laki mbili tu. Chama hicho na wadau wengine wamekuwa wakidai kuwa barabara ambayo imependekezwa na serikali na ambayo Rais Kikwete aliapa kuwa ni muhimu kujengwa kwani itaharakisha maendeleo kwa wananchi wanaoishi kaskazini mwa mbuga hiyo.

Kwa mujibu wa jarida hilo barua ya Benki ya Dunia inanukuu sehemu ya tamko lililotolewa na benki hiyo ambapo ilitoa ahadi kuwa iko tayari “kusaidia Tanzania katika kuchagua na pale ikifaa, kutoa fedha ambazo zitasaidia kufanikisha mbadala wa njia ya kaskazini ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya Kaskazini mwa Tanzania huku wakati huo huo kulinda hali ya kipekee ya mbuga ya Serengeti”.

Barabara inayopendekezwa na serikali na ambayo itakuwa na urefu wa karibu kilomita 480 itaanzia eneo la Mto wa Mbu, Engaruka, ufukwe wa Ziwa Natron, Loliondo, Serengeti na kuishia Musoma. Hata hivyo sehemu inayolalamikiwa na wanaharakati wa mazingira na mambo ya wanyama pori ni kiasi cha zaidi ya kilomita 55 ambazo zitakatiza ndani ya Serengeti.

Katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Bi. Ngozi Ikonjo-Iweala huko Davos mapema mwaka huu Rais Kikwete alisema kuwa ujenzi wa barababa hiyo utafanyika na utakuwa na manufaa makubwa. Rais Kikwete alitoa angalizo kuwa tayari kuna barabara ya urefu wa kilomita 220 ambayo inapita Serengeti kwa hiyo kupitisha sehemu ndogo ya kilomita 55 hivi halitakuwa jambo geni au kubwa kiasi hicho. Rais Kikwete alizihakikishia taasisi za kimataifa kuwa “Tuna wajibu kwa watu wetu, wanahitaji barabara na tutawapatia huku wakati huo huo tukilinda mbuga zetu za Serengeti”.

Hata hivyo, hadi hivi sasa haijajulikana kama Serikali ya Tanzania iko tayari kufanyia kazi na kukubali pendekezo hilo jipya la Benki ya Dunia hasa baada ya viongozi wa kitaifa kusisitiza kuwa barabara hiyo itajengwa kama ilivyokusudiwa na serikali.

1 Comment
  • jamani msipotoshe hii barabara haijengwe ndani ya hifadhi ya taifa ya serengeti tujaribu kuwa wakweli

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *