Kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuibua upotevu mkubwa mapato Serikalini wa trilioni 1.5, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitokeza kutoa ufafanuzi na kudai fedha hizo hazijapotea bali ni mkanganyiko wa mahesabu ambao haujaeleweka kwa wananchi.
Hatua hiyo ya CCM inakuja siku chache baada ya Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kuitaka Serikali itoe maelezo ya kinakuhusu fedha hizo na kuzitaka Kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Bajeti kuchunguza upotevu huo ili waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Kauli hiyo ya Zitto aliyoitoa mwishoni mwa juma, imeibua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii ambapo wananchi wanaitaka Serikali itoe ufafanuzi wa fedha hizo zimetumikaje na nani alihusika kuidhinisha malipo hayo ambayo hayapo kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Mapema leo CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amejitokeza mbele ya wanahabari kujibu tuhuma hizo na kudai kuwa chama chake kinakubaliana na ripoti ya CAG na mapendekezo aliyoyatoa wanayafanyia kazi ili kuongeza uwajibikaji Serikalini.
“Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa ambao umejitokeza baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuwekwa hadharani. Ni utaratibu mzuri ambao Chama Cha Mapinduzi kimejiwekea na kimeielekeza Serikali katika dhamira njema ni kuhakikisha ukweli na uwazi na shughuli za Serikali unaendelea kuwa bayana wakati wote”, amesema Polepole.
Licha ya Polepole kuikubali ripoti ya CAG aliwatupia lawama wanasiasa akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwamba anaupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo juu ya kile kinachodaiwa ni kutojulikana kwa zilipo trilioni 1.5 ambazo ripoti ya CAG ilihoji.
“Sisi kama chama hatuna tatizo na mtu anayetoa taarifa mbalimbali hadharani; ni uhuru kutoa maoni hadharani lakini sisi tuna tatizo la mtu mwongo anayetoa taarifa za uongo za kuupotosha umma”, amesema Polepole.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
Akizungumzia suala la trilioni 1.5, amesema kinachotokea ni kutokueleweka kwa kwa taarifa ya CAG kwasababu vitabu na hesabu za Serikali ziko vizuri na hakuna upotevu wa pesa yoyote na kinachofanyika ni wanasiasa kujenga taharuki kwa wananchi.
“Sasa nianze na trilioni 1.5 maana yake nini, tuoneshane hapa kuwa huyu mtu ni mwongo, mwongo mkubwa. Hesabu zote zimeeleza vizuri kabisa, vitabu vya Serikali vimeeleza vizuri kabisa. Mjue kwamba mtu huyu ni mwongo anatoa taharuki”, amesema Polepole na kuongeza kuwa,
“Ndio maana Mkaguzi na Mdhibiti wa fedha za Serikali amesema hili jambo ni hesabu na kwenye ukaguzi wa hesabu baada ya kuwa ukaguzi umepita yako mambo mnarekebisha ili mambo yakae sawasawa. Imepotea wapi? Hakuna senti tano iliyopotea”.
Amesema kulingana na mfumo mpya wa ukaguzi wa kimataifa unaitaka Serikali inapokuwa inahesabu fedha zake za mapato kuhusisha na fedha ambayo tayari imetolewa kwenye huduma mbalimbali kwa wananchi.
Ameeleza kuwa mfumo wa zamani ilikuwa ni lazima Serikali ihesabu fedha zake ambazo imekusanya tayari na sio zile ambazo ziko kwenye huduma na hazijaingizwa kwenye mapato.
“Matumizi ya Serikali katika mtindo mpya ambao unafuata vigezo vya kimataifa vya ukaguzi wa hesabu za umma unaitaka Serikali inapokuwa inahesabu fedha zake ziliyoingia kuhesabu pia na fedha baada ya kuwa Serikali imetoa huduma. Zamani ilikuwa lazima pesa tuishike mkononi”, amesema Polepole.
Ameendelea kutoa maelezo na kudai kuwa “Tumekusanya trilioni 25.3 pesa ambayo huduma imetoka inatarajiwa tumekwisha kuiingiza ipo. Lakini hii trilioni 25.3 ambayo ni makusanyo ya jumla. Ukitaka kujua makusanyo halisi unachukua pesa halisi unatoa makusanyo tarajiwa”.
Amesema makusanyo tarajiwa ambayo yanapatikana kwenye huduma ambazo Serikali imetoa kwa mwaka 2016/2017 na zilikuwa bado hazijakusanywa ni bilioni 687.3 na trilioni 25.3 ni fedha au mapato ghafi ambayo yanajumuisha fedha halisi na mapato tarajiwa (receiver bonds).
Amebainisha kuwa katika trilioni 25.3 ziko fedha zingine za Serikali ya Zanzibar ambazo zinafikia bilioni 203.92 na kwamba hazijumuishwi kwenye mapato na bajeti ya Tanzania Bara lakini zinatambulika kwenye mfumo wa mapato.
“Ukichukua trilioni 25.3 ukatoa bilioni 687.3, ukatoa bilioni 203.92 utapata 24.4 (trilioni 24.4), hii ndio pesa halisi iliyotumika 2017/2018. Sasa yule Bwana wa chama cha Mbunge mmoja anasema ilitumika kutoka ile trilioni 25.3 ni 23.79 (trilioni) kwahiyo kwenye trilioni 25.3 imetumika 23.79”, amesema Polepole.
Amesema katika trilioni 23.79 wakati CAG anakagua mapato, fedha ya Serikali ilikuwa kwenye hati fungani (unmatured bonds) yenye thamani ya bilioni 697.85 ambapo ikijumlishwa na fedha halisi za trilioni 23.79 unapata trilioni 24.4 ambazo zilikuwa ni makusanyo halisi ya mwaka 2017/2018.
“Nimekueleza mapato na matumizi, ukichukua trilioni 25.3 ukatoa trilioni 23.79 (fedha zilizotumika) utapata 1.5 trilioni ambayo huyu Bwana Zitto anasema imepotea, hesabu hajui”, amesema Polepole.
Zitto kushtakiwa
Kutokana na kile kinachodaiwa ni upotoshaji wa ripoti ya CAG kwa wananchi juu ya upotevu wa trilioni 1.5 kulikofanywa na Zitto, CCM kimetaka mwanasiasa huyo achukuliwe hatua za kisheria.
“Siasa za namna hii ni siasa za hovyo, kauli ya Chama Cha Mapinduzi ni kwamba wale wenye dhamana ya kusimamia sheria wafanye hivyo; mizaha na kuchekacheka na watu wa tabia kama hii ndiyo iliyotufikisha pabaya. Kutoa taarifa za uongo ni kosa katika nchi yetu”, ameshauri Polepole na kuongeza kuwa,
“Tabia hii haivumiliki, wanaosema mambo ya uongo, wanaoleta taharuki kwa watu wetu sheria ichukue mkondo wake”.
Kulingana na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, inaeleza kuwa mtu yeyote anayetoa taarifa za uongo zenye lengo la kupotosha au kupingana na zile zilizotolewa na mamlaka husika atakabiliwa na adhabu ya kufungwa kifungo kisichopungua miaka 2 au kulipa fidia.
Kwa upande wake, Zitto ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa, “Kuna mtu anasema nikamatwe kwa kupotosha Kuhusu TZS trilioni 1.5 zinazohojiwa na CAG. Mimi Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mwenyeji wa Kigoma, Muislam, NAAPA kwamba Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano imeshindwa kuonyesha kwa CAG matumizi ya shilingi trilioni 1.5.
Nipo tayari kukamatwa kwa kusema hivyo ( haitafuta ukweli wa ubadhilifu huo ). Nipo tayari kuuwawa kwa kusema hivyo ( mawazo yangu hayatakufa)”.