Wanafunzi wa shule ya msingi Mpanda iliyopo kata ya Ipyana wilayani Kyela wanalazimika kusoma kwa kupokezana kutoka na madarasa ya shule ya kuchakaa na kutokufanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hilder `Kajubili ameiambia Fikra Pevu kuwa shule yake inakabiliwa na upungufu wa madarasa kutokana na ukweli kwamba madarasa yaliyokuwepo yalijengwa muda mrefu na tayari yameanguka.
Jitihada za kujenga madarasa mapya ili kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi zimekuwa zikisuasua jambo linaloleta changamoto katika ufanisi wa walimu kufundisha darasani.
“Tuna uhaba wa madarasa sana, kwahiyo tuna double sessions (mikondo miwili) umeona madarasa tuliyanayo mengi ni magofu. Kwa hiyo tuna vyumba vya madarasa 6 tu, hao ni wengi sana (wanafunzi)wengine wanaingia mchana, wengine wanaingia asubuhi,” amesema Mwalimu Hilder.
Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1957 ina wanafunzi 832 ambapo wavulana ni 417 na wasichana 415 ambao hutumia vyumba 6 tu. Hiyo ina maana kuwa kwa wastani kila darasa lina wanafunzi 72 ambapo ni juu ya uwiano unaohitajika wa darasa 1 kwa wanafunzi 40 (1:40).
Awali kabla ya madarasa kubomoka wanafunzi wote walikuwa wanaingia asubuhi, lakini uchakavu na kuanguka kwa kuta za madarasa kulikosababishwa zaidi na mvua za msimu kumeifanya shule hiyo kuzungukwa na magofu.
Upungufu huo wa madarasa pia umechochewa na mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto shuleni baada ya kuanza kwa utekelezaji wa elimu bila malipo lakini imekuwa ni changamoto kwa walimu kuwahudumia wanafunzi wote katika shule hiyo.
Moja ya darasa liliaharibika katika shule ya msingi Mpanda
Licha ya shule hiyo kukabiliwa na upungufu wa madarasa, pia ina upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo ambapo walimu na wanafunzi wanatumia matundu 4 tu.
“Tulijenga vyoo vya muda kwanza, vyoo vya kawaida lakini ni vichache matundu yako manne; mawili wasichana na mawili wavulana. Ni vile vya kuflashi, unamwaga maji,” amesema Mwalimu Hilder.
Licha ya shule msingi Mpanda kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo kwa miaka miwili mfululizo, bado walimu wameendelea kufundisha kwa moyo na kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba wilayani Kyela.
Mathalani katika matokeo ya mwaka 2016, wakati choo cha wanafunzi kimetitia, shule hiyo ilishika nafasi ya 8 kiwilaya na mwaka uliofuata wa 2017 ilipanda na kushika nafasi ya 3 kati ya shule 42.
Naye mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Joyce Mwabwagilo (13) amesema wanashirikiana na walimu wao kuhakikisha mazingira yanayowazunguka ikiwemo usafi wa vyoo yanawasaidia kupata maarifa sahihi. “Masomo tuko vizuri, ufaulu uko vizuri lakini changamoto ni upungufu wa madarasa.”
Kwa upande wake, Mwalimu Douglas Mwalukasa ameiomba serikali na wadau kuguswa na hali iliyopo shuleni hapo na kuchukua hatua ya kuwaboreshea mazingira ya kufundishia ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri kitaaluma.
“Tuna upungufu wa madarasa, vyumba kama viwili hivi. Tunaendelea kufanya juhudi kuwasiliana na wadau kuweza kutusaidia kukamilisha vyoo vipya tunavyojenga.
Darasa lingine ambalo halina madirisha na limepata nyufa
Akizungumza na Fikra Pevu, Mratibu wa Elimu kata ya Kyela, Hezron Mwaikinda amesema wanaendelea na mipango ya kutatua changamoto za elimu katika shule za msingi ikiwemo kujenga madarasa na vyoo katika shule ambazo zina upungufu mkubwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea.
“Tunayo mipango kazi, kuna mambo ambayo unakuwa umepewa kipaombele kwa msimu wa mwaka huu ni kujenga madarasa na vyoo. Jukumu tulilonalo ni kuwaomba wadau mbalimbali watusaidie katika ujenzi,” amesema Hezron
Kwa upande wake, Katibu wa Muungano wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Kyela, Loth Mwangamba amesema wataendelea kushirikiana na Halmashauri ya Kyela kuhakikisha wanatafuta fedha kutoka kwa wafadhili ili kuboresha elimu wilayani humo.