SHIRIKA la Viwango nchini (TBS), limesema kwamba, limelazimika kuanzisha mpango mpya wa kudhibiti kabisa uingizwaji wa bidhaa zisizo na ubora hapa nchini, na kazi hiyo limeikabidhi kwa makampuni ya kutoka Ulaya, ili kulinda na kukuza uchumi wa nchi na faida kwa watumiaji wa bidhaa hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Ubora na Viwango kutoka TBS, Kezia Mbwambo aliyasema hayo hii leo Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na shirika hilo, na kufanyika kwenye ukumbi wa Mandela katika Hoteli ya Gold Crest.
Mbwambo aliutaja mpango huo ulioanzishwa kuwa ni Mkakati wa Ukaguzi wa Ubora wa Bidhaa kabla hazijaingizwa nchini, na kusema TBS imedhamiria kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini na zile zinazoingizwa sokoni kutoka nje ya nchi lazima ziwe zimekidhi ubora wa Kimataifa, na si vinginevyo.
“TBS tumelazimika kuweka mkakati huu ili kuhakikisha tunadhibiti kabisa uingizwaji wa bidhaa feki. Tunataka bidhaa zote zinazozalisha na viwanda vyetu na zile zinazotoka nje lazima ziwe na viwango vinavyokubalika Kimataifa.
“Mkakati huu wa ukaguzi wa ubora wa bidhaa kabla hazijaingizwa nchini utaanza kutumika rasmi Februari mwaka ujao 2012. Makampuni ya nje ndiyo yatakayosimamia, maana tunataka Watanzania wasiathirike na bidhaa feki”, alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa Kitengo cha Ubora na Viwango wa TBS.
Hata hivyo, Mbwambo aliyataja makampuni yaliyopewa kazi ya usimamizi wa programu hiyo mpya kuwa ni Bureau Veritas ya Ufaransa, SGS ya Swezland na kampuni ya Intertek International ya kutoka nchini Uingereza, na kwamba makampuni hayo yataweka mitandao yake kote nchini, yakiwemo maeneo ya Bandari ili kunasa bidhaa hizo feki.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Kitengo cha Ubora na Viwango wa TBS, aliwataka wamiliki wote wa viwanda hapa nchini kuhakikisha wanazalisha na kuingiza sokoni bidhaa zenye ubora unaotakiwa, na kwamba shirika lake halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kuzalisha bidhaa feki.
Alisema, zipo athari nyingi zinazowapata watumiaji wa bidhaa feki na zisizo na ubora, na mojawapo ni Tanzania kupata hasara kwa uchumi wake kuporomoka kutokana na bidhaa zake kukosa soko duniani, pamoja na watumiaji wake kulazimika kutumia fedha nyingi kununua bidhaa nyingine tofauti na matarajio.
Awali, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Evarist Welle Ndikilo, alilitaka Shirika hilo la Viwango nchini (TBS), kuhakikisha linashirikiana na wadau pande zote za nchi, ili kukomesha kabisa uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango vinavyotakiwa kisheria.
“TBS mnao wajibu wa kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wanaoingiza au kutengeneza bidhaa feki na kuwauzia watu. Shirikianeni na wadau wote na muwe wakali sana katika utekelezaji wa majukumu yenu haya”, alisema Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza, Ndikilo.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.