Choo cha muuguzi na vichaka vya nyasi

Kulwa Magwa

Unaweza usiamini kuwa unaingia kwenye choo kinachotumiwa na mtu anayejua nini maana ya neno ‘afya bora’. Hata hivyo, katika hali halisi, choo kinachotumiwa na muuguzi, Ester Malangwa, hakifai kutumiwa na binadamu kutokana na kuzingirwa na nyasi. Choo hicho kiko katika nyumba ya serikali anayopaswa kuishi mtumishi wa umma.

Pengine kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Ester hapendi kuishi kwenye nyumba ya zahanati ya kijiji hicho cha Mwadui-Lohumbo, badala yake amekuwa akiishi umbali wa kilometa 11 kutoka sehemu hiyo, ambako amepanga chumba.

choo-nyasi

CHOO CHA NYUMBA YA MUUGUZI WA ZAHANATI YA MWADUI-LOHUMBO, WILAYA YA KISHAPU, MKOANI SHINYANGA

Ni wazi kwamba nyasi zilizokizunguka choo hicho zinaonekana kwamba zimeota siku nyingi, lakini juhudi za kuziondoa hazijafanyika.  

Nani wa kumhakikishia Ester usafi wake wa mazingira? Namsaka, lakini hapatikani. Wenyeji wanasema yupo Mwadui-Mgodini ambako ana makazi mengine.

Hata hivyo mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph Jisena, anasema; ”Hilo ni suala dogo, ni jukumu la kijiji na tutalifanya”.

Anapoulizwa lini wataondoa nyasi hizo ili muuguzi huyo akae katika makazi hayo ya umma, Jisena anasema; “Wakati wowote, nadhani hata wiki ijayo, ila naahidi tutaondoa nyasi hizo”.

Muuguzi mstaafu wa zahanati hiyo, Ester Bushesha ambaye anaishi mita 100 kutoka makazi ya muuguzi huyo, anasema licha ya nyasi kuwa nyingi katika mazingira ya nyumba hiyo, pia nyumba yake imechakaa – ndiyo maana hapendi kuishi hapo.

Anasema, tangu hali ya uchakavu wa makazi na choo hicho ‘kuvamiwa’ na nyasi, muuguzi huyo haishi katika nyumba hiyo, suala ambalo limekuwa likikwaza wagonjwa wanaofuata huduma, hasa zile za sidano za kila baada ya muda.

“Sasa kama mtu anaishi huko mbali unategemea nini kwa mgonjwa ambaye anakuja kwa sindano? “anasema mama huyo.

Mkazi wa kijiji hicho, Erasto Jacob, anasema hali ya mazingira ya nyumba ya muuguzi huyo pamoja na choo ni kikwazo cha upatikanaji wa huduma za afya, ikizingatiwa kwamba hata daktari naye hapendi kuishi kwenye nyumba ya zahanati.

Anasema, usumbufu ni mkubwa zaidi kwa wagonjwa nyakati za usiku, maana kuwakuta muuguzi na daktari ni suala la kubahatisha.

nyumba-muuguzi

NYUMBA YA MUUGUZI WA KIJIJI CHA MWADUI-LOHUMBO

“(Usiku) ni vigumu kuwakuta kwa kuwa wana makazi mengine Maganzo na Mwadui mgodini na huko ni mbali. Ukiugua ghafla labda utafute usafiri, tena wa pikipiki ukupeleke Maganzo kupata tiba, “ anasema Jacob. Umbali kutoka Mwadui-Lohumbo hadi Maganzo ni zaidi ya kilometa 20.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kijiji anasema wanakusudia kuweka mazingira ambayo yatawafanya watumishi hao wa umma watulie katika makazi yao ikiwemo kununua na kufunga mashine za umeme wa jua kwenye nyumba zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *