St. Aggrey kupunguza adha ya wataalam wa afya nchini

Gordon Kalulunga

WANAFUNZI 120 wa chuo cha afya cha St Aggery College of Health Sciences kilichopo Jijini Mbeya wanatarajia kuhitimu mafunzo yao katika kada zaidi ya mbili mwaka huu 2013.

Kada hizo ni pamoja na madawa(Clinical Medicine), meno (Dental), Maabara(Laboratory)na uuguzi (Nursing).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Meneja wa taasisi ya St.Aggrey Jackson Kamugisha alisema kuwa wanafunzi hao wakihitimu watakuwa msaada mkubwa kwa serikali na watapunguza wimbi lililopo la upungufu wa watumishi wa afya nchini.

Kamugisha alisema kuwa wanafunzi hao wamejifunza fani hizo kwa usahihi na kwa vitendo ambapo katika masomo yao ya vitendo walipelekwa hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya mkoa wa Mbeya, hospitali teule ya wilaya ya Mbeya (Ifisi), Igawilo na kiwanja mpaka.

‘’Uhakika wa kuajiliwa wahitimu wetu ni mkubwa ukizingatia kuwa chuo chetu kimesajiliwa na NACTE kwa namba REG/NO/HAS/116P katika fani hizo nilizozitaja’’ alisema Kamugisha.

Alipoulizwa changamoto wanazozipata kama chuo alisema kuwa ni kutojibiwa haraka maombi ya kuwapeleka wanafunzi hao kwenye mafunzo ya vitendo katika hospitali mbalimbali.

Alisema kuwapeleka wanafunzi hao kwenye mafunzo ya vitendo ni lazima wanawatawanya lakini mara kadhaa wanakumbana na ucheleweshaji wa kujibiwa maombi hayo kwenye hospitali wanazopaswa kuwapeleka.

‘’Hali hiyo inasababisha hisia tofauti kwa wanafunzi na kudhani kuwa chuo hakina nia ya kuwapeleka mara kwa mara kwenye mafunzo hayo ya vitendo na muda mwingine kusababisha migomo isiyo kuwa ya lazima’’ alisema Kamugisha.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni wanafunzi wengi huwa hawapendi kupangiwa vijijini hivyo kuleta ugumu wa kuwatawanya kwa ajili ya mafunzo ya vitendo lakini wamejitahidi kuwaelewesha na baadhi wameelewa ingawa vijijini kunaonekana kuwa na changamoto kubwa za kiutendaji.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za baadhi ya wanafunzi waliosajiliwa katika chuo hicho kuwa na alama moja ya D ya ufaulu katika somo la Baiolojia katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha nne badala ya utaratibu wa sasa ambao unataka kila mwanafunzi awe na angalau D tatu.

‘’Awali ilikuwa hivyo na wale wote waliosoma kabla ya utaratibu kubadilika watapata ajira lakini kwa sasa serikali imeweka utaratibu mzuri sana na kuanzia mwaka huu hakuna chuo kilichodaili wanafunzi ambao hawana alama D katika masomo ya Kemia, Biolojia na Fizikia’’ alisema Kamugisha.

Kwa upande wake Makamu mkurugenzi wa taasisi hiyo Neema Mwambusi alisema kuwa mwaka jana iliwahi kujitokeza mitazamo ya kwamba chuo hicho hakikusajiliwa kutokana na wanafunzi kuchelewa kuanza mafunzo kwa vitendo ndipo uongozi wa taasisi ukalazimika kuwagharamia wawakilishi wa wanafunzi kwenda kuhakiki Wizarani na Nacte.

‘’ Changamoto ambayo ilikuwa ikiikabili taasisi yetu kabla ya chuo cha afya, kwa upande wa chuo cha ualimu ilikuwa ni suala la vyeti vya kugushi ambalo hivi sasa halipo kutokana na wanachuo wengi wanaojiunga ni wale waliohitmu hivi karibuni ambao vyeti vyao vina picha nan i rahisi kubaini kupitia baraza la mitihani’’

Taasisi hiyo ya elimu inatoa taaluma ya masuala ya afya, elimu ya awali, Msingi, Sekondari na ualimu kwa ngazi ya cheti daraja la tatu na stashahada.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *