REGINALD Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Limited (pichani), amesema mafisadi wanatumia fedha kuzima harakati za mapambano dhidi ya ufisadi, na kuonya kwamba kutochukuliwa hatua kwa mafisadi ni hatari kwa amani.
Mengi amesema kwa sasa makundi yaliyokuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi yamenyamazishwa kwa fedha, vitisho na mbinu mbalimbali chafu, na kusema kuna kila sababu ya kufufua upya mapambano dhidi ya ufisadi.
Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi tangu kashfa kubwa za ufisadi zilipoanza kuibuliwa, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa chakula cha mchana na watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam, ambapo alisema baadhi ya wapambanaji hao wamepoteza mwelekeo katika vita ya ufisadi.
“Wapambanaji wa ufisadi pamoja na vyombo vya habari vilivyokuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi vimenyamazishwa kwa njia mbalimbali,” anasema na kuongeza;
“Rushwa ya fedha kutoka kwa mafisadi imewanyamazisha, nguvu za mafisadi kwa kutumia fedha zinatumika kuwatisha ama kuanzisha mikakati inayolenga kuzorotesha vita hiyo.”
Kauli ya mwenyekiti huyo wa IPP Limited, ambaye anafahamika kwamba msururu wa vyombo vya habari ulishiriki katika kufichua ufisadi tangu mwaka 2006, imekuja katika wakati ambao vita dhidi ya ufisadi imeonekana kuzorota na kukosa nguvu katika siku za karibuni.
Hali hiyo imetafsiriwa na wachunguzi wengi wa siasa na utawala kwamba mafisadi wanaweza kuendeleza ufisadi wao bila hofu kwa kuamini kwamba hakuna mpambanaji atayethubutu kuwagusa tena.
Vita hiyo ya ufisadi ilishika kasi katika Bunge la Tisa, baada ya Spika wa Bunge hilo Samuel Sitta (sasa Waziri wa Afrika Mashariki) kutoa uwanja mpana wa mijadala ya aina hiyo ambayo ilishuhudia wabunge wa upinzani wakiibua kashfa kubwa za ufisadi na kuungwa mkono na wale wa Chama cha Mapinduzi.
Kashfa kama ya ununuzi wa Rada, wizi wa fedha za EPA, mkataba wa Richmond, ununuzi magari ya jeshi, Ndege ya Rais na nyinginezo nyingi, ambazo zilianza kuibuliwa na mtandao wa kijamii wa JamboForums.com (sasa jamiiforums.com) zilifikishwa Bungeni na kambi ya upinzani kupitia wabunge wa CHADEMA na zikazua mjadala mrefu uliowafumbua macho wananchi.
Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Wilbrod Slaa, akiwa Mbunge wa Karatu, alikuwa mstari wa mbele kufichua kashfa hizo hadharani na kuungwa mkono na wabunge wa CCM kama Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Anne Kilango (Same Mashariki) na na James Lembeli (Kahama).
Wengine ni wabunge wa zamani Lucas Selelii (Nzega), Aloyce Kimaro (Vunjo) na William Shelukindo (Bumbuli ).
Hata hivyo ni Dk. Slaa pekee na baadhi ya viongozi wenzake wa Chadema,dio walioendeleza kasi ya vita dhidi ya ufisadi huku baadhi ya wabunge waliokuwa mstari wa mbele wakipoteza nafasi zao za ubunge mwaka 2010.
Mengi alisema ripoti nyingi za uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari, zimefichua ufisadi wa aina mbalimbali ambao mpaka sasa haujakanushwa ikiwamo ule wa Kagoda na Meremeta.
“Hii inamaanisha kuwa ripoti hizi ni za kweli, lakini ripoti hizi ni za muda mrefu na hadi sasa waliohusishwa na ufisadi hawajachukuliwa hatua,” alisema Mengi.
Mengi alisema wananchi wamekatishwa tamaa ya ushindi dhidi ya ufisadi kutokana na watuhumiwa kutochukuliwa hatua za kisheria.
“Wananchi sasa wanaona kama ufisadi umekubalika kuwa ni sehemu ya maisha, vitendo vya kifisadi lazima vichukuliwe hatua za kisheria haraka mara vinapobainika ili kuepusha uvunjifu wa amani katika jamii,” alisema
Aliongeza kuwa inashangaza kuona mtu aliyechota fedha za EPA anakiri uporaji huo na anatamba amerudisha fedha, lakini hachukuliwi hatua yoyote eti kwa sababu hakuna ushahidi
“Kama kurudisha si ushahidi, ni ushahidi gani unaotakiwa?,” alihoji.
Mengi, ambaye aliwahi kutoa orosha ya mafisadi aliowaita ‘mafisadi papa’, alisema mfumo mzima wa jamii umechafuliwa na ufisadi unaowahusisha baadhi ya viongozi wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa umma na biashara ya dawa za kulevya inayodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa dini.
Mwenyekiti huyo wa IPP Limited mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kupiga vita fisadi akitajwa kuwa nyuma ya makamanda wa ufisadi.
Kwa kutoa mchango mkubwa kupitia vyombo vyake vya habari na vyombo vingine, mwaka 2008 alitunukiwa tuzo ya kimataifa na serikali ya Marekani inayojulikana kama Martin Luther King, Jr. Drum Major for Justice Award.
Kutokana na mchango wake huo, amekuwa akiandamwa mara kwa mara na watuhumiwa wa ufisadi kwa mambo mbalimbali ya wazi na mengine yasiyoonekana. Tayari baadhi ya watuhumiwa wamejitokeza hadharani kutishia kumshughulikia na baadhi wakitumia mbinu mbalimbali kumdhibiti yeye pamoja na wote wanaotajwa kuwa karibu naye.
Habari zaidi soma: http://www.mwananchi.co.tz/habari/4-habari-za-kitaifa/19625-mengi-awarushia-kombora-wapambanaji-ufisadi-nchini