Vijiji vinavyozunguka ziwa victoria katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, vimeelezwa kuwa na tatizo kubwa la magonjwa ya zinaa (STI) kutokana na sababu mbalimbali.
Mganga mkuu wa zahanati ya Guta Lucy Charles anasema kuwepo kwa kambi ya wavuvi katika vijiji vya Guta, Nyabehu na Kinyambwiga ni sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa maambukizi makubwa ya magonjwa ya zinaa.
Anasema idadi kubwa ya wajawazito wanaokuja kupimwa katika zahanati yake, wanakutwa na magonjwa hayo, hivyo huzungumza nao, namna ya kuwatibu pamoja na kuwaleta wenza wao ili kuhakikisha magonjwa hayo yanayoweka katika vijiji hivyo.
Naye Mganga mkuu wa Wilaya ya Bunda Rainer Kapinga amekiri kwamba magonjwa ya zinaa kwa wilaya yake ni moja kati ya magonjwa kumi yanayoongoza katika wilaya yake.
“Tunajitahidi kupeleka kondom, elimu pamoja na tiba katika vijiji vinavyozunguka ziwa, maana sehemu yenye magonjwa mengi ya zinaa, inaonyesha dalili kuwa watu hao wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ukimwi, nafafanua….
Mganga mkuu wa zahanati ya Guta ameeleza madhara yanayoweza kumpata mtoto aliyeko tumboni kwa mama mwenye magonjwa ya zinaa, kuwa mtoto anaweza kuzaliwa mfu, kinga ya mtoto inakuwa dhaifu,lakini pia mtoto huyo anaweza kuzaliwa na upofu.
Anaeleza madhara anayoweza kuyapata mama mwenye magonjwa ya zinaa, anasema mama anaweza kupata ugumba na mimba inaweza kutunga nje ya mfuko wa uzazi.
Ameyataja magonjwa hayo kuwa ni kisonono na kaswende.