WANAUME nchini wametakiwa kushiriki kwa vitendo na wake au wenza wao katika kukabiliana na hali ya maabukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kupenda kwenda hospitali au vituo vya afya kupata elimu ya uzazi na jinsi ya kujikinga na maabukizi hayo.
Wito huo umetolewa na ofisa mradi mwandamizi mawasiliano mradi wa CHAMPION Muganyizi Mutta, alipokuwa akitoa mada kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya zinazolenga kushirikisha wanaume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya (VVU).
Mutta alisema kuwa mradi huo ni mradi wa kwanza Tanzania unaolenga kushirikisha wanaume katika mapambano chanya dhidi ya maambukizi ya VVU, hivyo wameona ni vema ukatoa maarifa kwa waandishi wa habari ili waweze kuelewesha jamii kwa kuandika au kutangaza kwa ufasaha habari baada ya kujua faida za wanaume kutimiza wajibu wao katika mapambano hayo.
Alisema kuwa kinachokwamisha baadhi ya wanaume kushiriki katika huduma za afya na kwenda hospitalini na wake au wenza wao ni pamoja na mila na desturi zinazoeleza kuwa jukumu la kutunza mimba na kulea mtoto ni la mwanamke.
"Mbali na hilo pia kuna mitazamo ya kimazoea Stereotype ambapo mwanaume kwenda na mkewe kliniki jamii inamshangaa, hivyo umefika wakati jamii ibadilike na kuona suala la mimba kabla na baada ya kujifungua ni jukumu la wote yaani mwanamke na mwanaume'' alisema Mutta.
Alisema kuwa mradi huo unasimamiwa na shirika la EngenderHealth na shirika mwenza linalojulikana kwa jina la FHI360 na kufadhiliwa na USAID ambapo wanaifikia jamii hasa wanaume kwa njia mbalibali ikiwemo mwanaume mmojammoja, mikusanyiko (jamii) na maeneo ya kazi.
Baadhi ya washiriki walisema kuwa ili jamii iweze kuepukana na ongezeko la VVU elimu iwafikie kikamilifu ili kabla ya kupanga kuzaa watoto wanandoa na hata wenza waweze kufika katika vituo vya afya na hospitali kupima afya zao ili hata kama watakuwa wameambukizwa au mmoja wao waweze kupata mbinu ya kutomwambukiza mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.