WAJAWAZITO wa kijiji cha Mgowelo kilichopo kata ya Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa, wanalazimika kutembea kwa miguu zaidi ya kilomita 16 hadi kijiji cha Mtandika kufuata huduma za matibabu.
Kero hiyo ni matokeo ya kijiji hicho kuchelewa kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) unaotaka kila kijiji kiwe na Zahanati.
Miaka miwili iliyopita kijiji hicho kilipokea mchango wa Sh 100,000 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo Profesa Peter Msolla kama njia ya kuhamasisha wananchi kuanza ujenzi wa zahanati.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Antoni Kiwonde, tangu wakati huo, jitihada za kijiji kuwa na zahanati yake hazijazaa matunda.
“Hakuna kinachoendelea baada ya nguvu kazi ya kijiji kufanikiwa kufyatua tofali 18,000 na kukusanya mawe roli 12 hadi katika eneo la ujenzi,” alisema.
Kiwonde alisema wajawazito na watoto ndio wanaoathiriwa zaidi na ukosefu wa zahanati katika kijiji hicho.
Rose Ngunwa alisema pamoja na kusafiri umbali mrefu kufuata huduma; sehemu yake kubwa hazitolewi bure kama sera ya afya inavyoelekeza.
“Wakati mwingine tunalazimika kununua dawa na vifaa tiba kama mipira ya kujifungulia na ya kuvaa mikononi pindi inapokosekana katika kituo cha afya cha Mtandika,” alisema na kuongeza kwamba kituo hicho kinamilikiwa na Kanisa la Katoliki.
Ni kweli. Huduma ya bure kwa wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, inatamkwa katika Sera ya Afya ya mwaka 2007. Sera hii iliandaliwa rasmi kwa kuzingatia mabadiliko ya sera za kiuchumi na kijamii yaliyojitokeza kitaifa na kimataifa.
Sera inalenga kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, inayowapa wanawake maamuzi juu ya masuala ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuamua idadi ya watoto katika familia.
Ni sera hii pia inayolenga kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanayoelekeza kupunguza, kwa asilimia 75, vifo vya wajawazito na watoto ifikapo mwaka 2015.
Grolia Mwakyusa na Neema Mlawa wameiomba serikali kuwajengea zahanati ili kukabiliana na changamoto mbalimbili zinazowakabili wakati wakifuata huduma.
“Ilikuwa majira ya saa moja usiku wa Novemba mwaka juzi nilipojifungua njiani wakati ndugu zangu wakinisindikiza Mtandika, hatukuwa na usafiri; tuliweza kutembea umbali wa kilomita mbili tu kabla ya kubanwa na uchungu na hatimaye kujifungua,” anasema Mlawa.
Mwakyusa anasema kwa wenye uwezo hulazimika kutumia zaidi ya Sh 10,000 kukodi pikipiki maarufu kama bodaboda, kwa kuwa hakuna huduma nyingine ya usafiri wa abiria.
Elentina Mtahuka alisema tatizo la mawasiliano ya simu katika kijiji hicho wakati mwingine hukwamisha upatikanaji wa huduma ya usafiri wa bodaboda.
“Mawasiliano ya simu za mkononi sio ya uhakika, wakati mwingine unaweza kuwa na fedha kwa ajili ya kukodi pikipiki lakini ukashindwa kuipata kwasababu ya kukosa mawasiliano,” alisema.
“Tunaomba serikali isikie kilio chetu, itusaidie fedha ili tuanze ujenzi, vinginevyo wajawazito na watoto wataendelea kuupata taabu kutafuta matibabu na hata kusababisha vifo vyao,” alisema.