Watumishi jiji la Mwanza hatiani kwa kubomoa choo na kibanda cha bibi lishe

Jamii Africa

SHAURI  la kudharau  amri  ya Baraza la Ardhi  na Nyumba  lililokuwa  limefunguliwa na ‘bibi  kizee’ mmoja jijini  hapa, Moshi Juma Mzungu(67) dhidi  ya watumishi  wa Halmashauri ya Jiji  la Mwanza  limetolewa uamuzi, ambapo  wafanyakazi saba  wametiwa hatiani  na hivyo  kuamriwa  wakamatwe ili washtakiwe  katika mahakama zenye uwezo    wa kusikiliza kesi za jinai.

Shauri  hilo  ambalo  lilikuwa kivutio  kikubwa  miongoni mwa  wakazi  wa Jiji  tangu kufunguliwa kwake  Desemba mwaka jana, liliamriwa  jana  na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Christian  Mwashamwa.

Aliliambia  Baraza kuwa baada ya  kupitia  ushahidi  uliowasilishwa na mlalamikaji, Baraza hilo  limeridhika kwamba  watuhumiwa  kwa  pamoja  walidharau amri  iliyokuwa imetolewa  na  Baraza hilo na kuamua kwenda kubomoa choo, bafu pamoja  na banda la mama ntilie; mali ya mlalamikaji.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Josephat Manyerere (Chadema)

“ Baraza hili  limeridhika  na  ushahidi  uliowasilishwa na mlalamikaji ; na hivyo  wale  wote  waliohusika  na uvunjaji, wakiwemo  watumishi  wa halmashauri ya Jiji la Mwanza  wanatakiwa  wakamatwe ili washtakiwe  katika mahakama zilizopewa mamlaka ya  kuendesha kesi za jinai”  Mwenyekiti   aliliambia Baraza.

Alisema  pia  kuwa gari lenye namba za usajili SM 3359 Mitsubish Center, mali ya Halmashauri   lililokuwa likitumiwa na  maafisa hao  siku ya tukio nalo linatakiwa likamatwe  kama kielelezo.

Aliwataja  wafanyakazi  wa Halmashauri ya Jiji  wanaotakiwa kukamatwa kuwa ni Abdon Baraka, Kitia Kagoroba, Mwita Wambura, Kasim, Kingi, Lazaro  Matulanya  pamoja na dereva  wa gari hilo  aliyetajwa kwa  jina la Victor Mashamba.

Wengine  waliokuwa wamefuatana na watumishi wa halmashauri ya Jiji wametajwa kuwa  Shida Manyama, Sospeter Mjinja, Hamza Kalibuhe, Athumani Faraji na  Hamis  Faraji.

Mwenyekiti huyo  alisema  amri hiyo  ilitolewa   mwaka  jana  na kwamba  ilikuwa  inazuia  kufanyika kwa  shughuli zozote katika eneo na nyumba  namba 244, Kitalu ‘L’ iliyoko  katika mtaa  wa  Pasiansi Mashariki  Jijini Mwanza.

“ Matokeo yake ni kwamba   watu hao, wakiwemo watumishi wa Jiji  ambao  wanatakiwa  kusimamia sheria  za mipangomiji  Desemba 23 mwaka jana, majira ya asubuhi  waliamua  kwenda  kuvunja nyumba  ya mlalamikaji ambaye ni  Bibi Moshi Juma Mzungu, huku wakifahamu fika kwamba  kesi ya msingi  bado  haijatolewa  maamuzi”  alisema.

Alisema kitendo hicho  ambacho ni cha uonevu  kilisababisha usumbufu  kwa mlalamikaji  ambaye ni bibi kizee  na pia mjane.

Mwenyekiti huyo  alisema kwa kufanya hivyo pia, watendaji wa Halmashauri ya Jiji  waliingilia  mwenendo wa kesi   ya jinai ; kesi  ambayo  alisema bado  inaendelea  kulisikizwa katika  mahakama   ya mkoa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe

Alisema  Baraza limetoa adhabu hiyo ili liwe fundisho  kwa watendaji  wa  Halmashauri ya Jiji la Mwanza  pamoja na watendaji wengine  katika  ofisi za serikali jijini  hapa  ambao  mara kwa mara wamekuwa na tabia ya  kukiuka  sheria  za nchini  na kusababisha  kuwepo  kwa  mashauri mengi ya yanayotokana na migogoro  ardhi jijini.

Katika  shauri hilo, mlalamikaji alikuwa akitetewa na  kampuni  ya uwakili  ya Muna  Advocates ya Jijini hapa  ambapo   Halmashauri ya Jiji  lilitetewa na wanasheria  wake.

Habari hii imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza

1 Comment
  • wazee ni kundi lililosahaulika mwiongoni mwa wanajamii ya Tanzania. Wananyimwa huduma nyeti za afya,chakula na kumiliki ardhi kama hili la mwanza. zaidi ya yote ni mtizamo hasi ya wanajamii walionao kwa wazee, hebu angalia kichwa cha habari cha taarifa hii,WATUMISHI JIJI LA MWANZA HATIANI KWA KUBOMOA CHOO CHA KIZEE- NENO KIZEE LINA UKAKASI WA MTAZAMO HASI KWA WAZEE, hebu waandishi na wanajamii tubadilikeni kuhusu hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *