Plan International kutumia Euro 800,000 kuwakomboa watoto migodini

Jamii Africa

SHIRIKA la Plan International, limepanga kutumia Euro 800,000 (sawa na Sh. Bilioni 1.6) katika kutekeleza mradi wa kupambana ajira za watoto kwenye maeneo ya migodi Wilayani Geita Mkoani Mwanza.

Mwezeshaji wa semina ya utekelezaji wa mradi wa kupambana na ajira kwa watoto wilayani Geita Mkoani Mwanza

Imeelezwa kwamba, umasikini, elimu duni na mtazamo hasi kwa baadhi ya jamii wilayani Geita, ni miongoni mwa vitu vinavyochangia zaidi kuwepo kwa ongezeko kubwa la ajira kwa watoto waliopo chini ya miaka 18 katika maeneo ya migodini wilayani hapa, jambo linalotakiwa kukomeshwa haraka.
Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, David Muthungu ameyasema hayo jana wilayani Geita, wakati alipokuwa akizindua utekelezaji wa mradi wa kupiga vita na kupambana na ajira za watoto katika maeneo ya migonini wilayani hapa, uliofanyika katika ukumbi wa Nkola Hoteli.
Alisema, mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano, utajikita zaidi kuwasaidia watoto hao kuondokana na athari mbali mbali zinazowakumba katika ajira hizo zisizo rasmi, na kwamba Plan International itahakikisha mradi huo unazaa matunda makubwa.

Meneja wa Mawasiliano wa Plan International Tanzania, Tenga B. Tenga (wa pili kulia), akiwa na Meneja wa Plan Wilaya ya Geita Mwanza (wa mbele kulia), Daniel Kalimbiya wakimsikiliza kwa makini Ofisa mradi wa Plan, Perrine Savoie (kushoto), wakati wakijadiliana jambo juu ya mradi huo jana.

“Plan International tumelazimika kuanzisha mradi huu ili kuwasaidia watoto wadogo katika ajira mbaya maeneo ya migodini.

“Mradi huu ni mkubwa na mzuri sana, na utagharimu Euro 800,000 ambazo ni sawa na kiasi cha sh. Bilioni 1.6 fedha za Kitanzania!. Tutawashirikisha wadau mbali mbali katika utekelezaji wa mradi huu ili tuweze kufikia malengo”, alisema Muthungu.

Hata hivyo, Muthungu alibainisha kwamba, mradi huo utatekelezwa katika maeneo ya Kata nane za Katoro, Bukoli, Mwigiro, Mtakuja, Kaseme, Lwamgasa, Nyarugusu pamoja na kata ya Nyakagwe.

Alisema, mradi huo umelenga kuwasaidia na kuwakomboa watoto 4,500 waliopo katika ajira hizo zisizo rasmi, na kwamba watoto wa kiume 30,200 na wasichana 30,800 wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi 13 watasaidiwa kurudishwa kwenye mfumo mzuri wa elimu.
“Pia mradi huu utasaidia kuwarudisha kwenye mfumo wa elimu watoto wa kiume 30,200 na wasichana 30,800. Tumebaini tatizo la ajira kama hizi mbaya linatokana na umasikini na kukosekana kwa elimu bora”, alisisitiza Mkurugenzi huyo wa Plan International hapa nchini, Muthungu.
Awali, viongozi mbali mbali wa mashirika yasiyo ya Kiserikali waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo kutoka wilayani Geita, walisema kwamba, karibu robo ya watoto wilayani Geita wanafanyakazi machimboni, hivyo wamekuwa wakiathirika vibaya na kushindwa kujitibu.
Walitoa mfano katika machimbo ya Nyarugusu, Nyakagwe na Kaseme ambapo walisema, watoto wengi wamejiingiza kwenye ajira hizo mbaya, huku baadhi yao wakilazimishwa kufanya hivyo na wazazi wao ili kuzisaidia familia zao fedha za chakula na kujikimu.
“Robo ya watoto hapa Geita wapo kwenye ajira machimboni. Hii ni hatari sana maana wamekuwa waathirika wakubwa na kemikali za madini na Mekuri. Tunashukuru Plan kwa kuanzisha mradi huu mzuri”, alisema Katibu wa shirika la Mwarema, Golden Hainga.
Duru za habari zinasema kwamba, wapo baadhi ya watoto wanaofanya kazi katika maeneo ya machimbo wilayani Geita, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili, ikiwa ni pamoja na kubakwa, kudhurumiwa haki zao, kupigwa bila sababu na kufanyishwa kazi ngumu jambo linalodaiwa kuathiri zaidi maisha yao.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *