Imeelezwa kwamba baadhi ya akina mama wa wilaya ya Butiama, wanajifungulia nyumbani kutokana na umbali wa upatikanaji wa huduma za afya.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Butiama Joseph Musagara, anasema vipo vijiji ambavyo viko umbali wa km 100 kuifikia hospital ya wilaya au kituo cha afya, hali inayowafanya akinamama wengi kujifungulia nyumbani.
PICHA: Mganga mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Butiama, Joseph Musagara akiwa ofisini kwake
Pamoja na kutaja umbali kama sababu inayowafanya akina mama kujifungulia nyumbani, anasema miundombinu ya barabara pia ni tatizo kwa wajawazito, anasema kutokana na hali hiyo wajawazito wanaoishi mbali na hospitali na vituo vya afya wanajikuta wakichelewa kuzifikia huduma na hatimaye kujifungulia nyumbani.
Gati Mituki mkazi wa kijiji cha Siloli Simba wilayani Butiama, anasema kutokana na umbali wa kuifikia hospitali ya Butiama na hata kituo cha afya cha Kiagata, ambapo ni mwendo wa saa tatu kwa gari, amejikuta akijifungulia nyumbani watoto sita, chini ya uangalizi wa mama yake mzazi.
Gati Mituki akiwa na watoto wake wachanga
Anasema alilazimika kufika hospitali ya wilaya ya Butiama kutokana na ujauzito wake wa saba kuwa na matatizo, anasema tayari amefanyiwa upasuaji kutokana na watoto ambao ni mapacha kukaa vibaya tumboni.
Gati anasema anamshukuru Mungu aliwahi kufika Hospitali, kwani pamoja na kufanyiwa upasuaji anajisikia vizuri anapowaona watoto wake mapacha wa kike na wa kiume wakiwa na afya njema na yeye akiendelea kupata matibabu.