WAJAWAZITO 303 KATI 100,000 HUPOTEZA MAISHA WILAYANI IRINGA

Frank Leonard

WASTANI wa wajawazito 303 kati ya 100,000 wamekuwa wakipoteza maisha wakati wakijifungua wilayani Iringa.

Vifo hivyo vinaendelea kutokea wakati serikali na washirika wake wakiongeza kasi ya kufikia malengo ya Millenia ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.

Kuhusu vifo vya watoto, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudensiana Kisaka alisema vifo vimekuwa vikiwakumba zaidi wale wenye umri  wa siku sifuri hadi siku 28.

“Kati ya watoto 1,000 wanaofariki ni asilimia 15 hadi 19.3; hii ina maana kwamba katika kila watoto 1,000; watoto 15 hadi 20 wanafariki, hizo ni takwimu kubwa sana ni ni muhimu tukaongeza jitihada za kukabiliana na hali hiyo,” alisema.

Akizungumzia changamoto hizo katika maadhimisho ya baraza la uuguzi na ukunga nchini yaliyofanyika kiwilaya katika Hospitali teule ya Tosamaganga, Iringa, Kisaka alisema takwimu hizo zinazorotesha mipango ya kitaifa ya kufikia lengo namba nne na tano la millennia la kupunguza vifo vya watoto na wajawazito.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudensiana Kisaka, akitoa misaada na zawadi kwa wagonjwa na akinamama wajawazito waliojifungua siku ya uuguzi na ukunga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudensiana Kisaka, akitoa misaada na zawadi kwa wagonjwa na akinamama wajawazito waliojifungua siku ya uuguzi na ukunga.

Alisema kuzorota kwa utoaji wa huduma ya afya ya uzazi kunachangiwa na miundombinu iliyopo ikiwemo majengo na vifaa vya kutolea huduma kutokidhi mahitaji.

Pamoja na miundombinu alizitaja sababu zingine kuwa ni upungufu wa dawa na vifaatiba, watumishi wenye ujuzi, matumizi ya wataalamu na vifaa, na uchache wa wataalamu.

Akitoa takwimu za wauguzi, Mkurugenzi huyo alisema halmashauri yake ina asilimia 66 tu ya wauguzi wenye ujuzi ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 50.

“Kwahiyo katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma, upungufu wa wauguzi wenye ujuzi ukiwemo wa kuzalisha wajawazito ni asilimia 34,” alisema.

Ili waweze kutoa huduma bora kwa wajawazito na watoto, alisema halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya sekta ya afya itawekeza katika kuwaendeleza kielimu wauguzi na wakunga wake.

“Tunataka wapate elimu katika ngazi ya Stashahada na Shahada, wakiwa na viwango hivyo vya elimu hakuna shaka kwamba huduma watakaozkuwa wakitoa zitakuwa bora zaidi,” alisema.

Naye muuguzi mfawidhi wa hospitali hiyo, Sister Julieta Mzena alisema hospitali hiyo ina uhaba wa watumishi unaochangia msongamano mkubwa wa wagonjwa.

Alisema wakati hospitali hiyo ikiwa na manesi waliosajiliwa 19 na wauguzi wakunga 46, ina upungufu wa wauguzi 65.

Alisema upungufu huo umesababisha wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi, wapate huduma saa saba mchana.

Pamoja na upungufu huo, Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Edmunda Mosha alisema msongamano wa wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma unachangiwa na baadhi ya wauguzi kushindwa kufuata kanuni za utoaji wa huduma kwa namna inavyotakiwa na wizara.

Wakati wa maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uuguzi, wauguzi na wakunga walitoa misaada mbalimbali vikiwemo vitenge, khanga na sabuni kwa wagonjwa wa hospitali hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *