Utoaji mimba wakithiri Ifakara, wafanywa kwa kati ya Sh 30,000 na 85,000

Frank Leonard

WAKATI kutoa mimba kwa mujibu wa sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 (kifungu cha 150 hadi 152) ni kosa la jinai, wilayani Kilombero mkoani Morogoro, huduma hiyo hutolewa kwa kati ya Sh. 30,000 na Sh. 84,000.

Utoaji mimba huo hufanyika nje ya taratibu za hospitali, vituo vya afya na zahanati wakati mwingine ukihusisha wataalamu wa kitabibu wasio na ujuzi na kazi hiyo.

Desemba 5, 2012, Mary Joseph (19) alifika katika hospitali teule ya Mtakatifu Francisco ya mjini Ifakara, wilayani Kilombero mkoani Morogoro na kulipa Sh 3,000 ili kupata kadi (nakala yake tunayo) kwa ajili ya kumwona daktari.

Bila kumtaja jina, Mary anasema daktari huyo alimueleza kwamba yeye ni bingwa wa magonjwa ya akinamama.

Mary alitaka kutoa mimba ya mwezi mmoja na nusu: alipewa dawa aliyotakiwa kuingiza ndani ya uke wake karibu na mlango wa uzazi ili imletee uchungu.

Aliambiwa huduma hiyo inatolewa kwa siri bila uongozi wa hospitali hiyo kujua na hivyo hakupaswa kumwambia mtu yoyote.

Gharama ya huduma hiyo kwa mujibu wa Mary ilikuwa Sh 84,000: Sh 50,000 ikiwa ni gharama ya hospitali inayotozwa kwa mgonjwa anayetakiwa kufanyiwa matibabu yasiohusiana na utoaji mimba katika chumba cha upasuaji.

 “Shilingi 4,000 kwa ajili ya dawa za maumivu na Sh 30,000 kwa ajili ya daktari atakayenipa huduma” Mary anachanganua gharama hiyo na kuongeza kwamba alisita kutoa mimba hiyo baada ya kuelezwa kwamba kizazi chake kinaweza kuharibika.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Anjelo Nyamtema anakanusha huduma ya aina hiyo kutolewa hospitalini hapo, lakini anasema huenda wapo baadhi ya madaktari wanafanya kazi hiyo kwa siri, ndani au nje ya hospitali hiyo kwasababu vifaa vya kutolea huduma hiyo vipo na vinauzwa madukani.

Hata hivyo anasema, katika hospitali yao wanatoa tiba za dharula zitokanazo na utoaji mimba usiokamilika au usio salama na mimba zilizotoka zenyewe.

Anasema kati ya mwaka 2011 na 2012 walipokea wanawake 862 waliopata madhara yaliyotokana na matatizo hayo.

Kati yao, 16 walipoteza maisha wakati wa matibabu kwasababu walifika wakiwa wamepoteza damu nyingi pamoja na baadhi yao kuoza mfumo wa uzazi.

Wanawake hao wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 walifanyiwa upasuaji na kusafishwa kizazi; gharama yake ni kati ya Sh 20,000 na Sh 50,000 kulingana na ukubwa wa tatizo.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0784991020 au 0655991020 na www.frankleonard.blogspot.com

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *