Vifo vya wajawazito Tanzania sawa na ajali tano za ndege za abiria kila siku

Gordon Kalulunga

VIFO vya wanawake wajawazito vinavyotokea kwa mwaka nchini, ni sawa na ajali tano za ndege za abiria zinazoweza kutokea kila siku.

Hali hiyo imeelezwa na Mkurugenzi mkazi wa mradi wa Evidence for Action( E4A) Craig Ferla unaoshughulikia masuala ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto nchini.

Hayo aliyaeleza katika ukumbi wa mikutano wa mfuko wa vyombo vya habari Tanzania, Tanzania Media Fund (TMF) uliopo Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiwaongezea maarifa, waandishi wa habari wanaobobea kwenye masuala ya habari za afya ya uzazi nchini.

Craig alisema kuwa kwa sasa takwimu za vifo vya wajawazito na watoto Tanzania zinatisha ambapo kwa mwaka wanawake 8,500 wanakufa na watoto 50,000 wanakufa kila mwaka.

“Vifo hivyo ni sawa na wastani wa vifo vya wanawake wajawazito 23 na watoto 137 chini ya miaka mitano vinavyotokea kila siku’’ alisema Mkurugenzi huyo wa E4A.

Crain-Ferla

PICHA: Mkurugenzi wa mradi wa Evidence for Action Craig Ferla akizungumza na waandishi wa habari Tanzania wanaobobea kuandika habari za afya ya uzazi

Alisema kuwa vifo hivyo sawa na vifo vinavyoweza kutokana na ajali za ndege tano za abiria kwa kila siku hali ambayo alisema kuwa haipaswi kufumbiwa macho na jamii pamoja na serikali ya Tanzania.

Naye Dr. Moke Magoma alisema kuwa kwa sasa kuna idadi kubwa ya wajawazito wanaojifungulia hospitali tofauti na hapo awali ambapo wengi wao walikuwa wakijifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi.

Alisema dhana ya kuwa hospitali nyingi nchini zinawafanyia upasuaji wajawazito na kukwamisha baadhi yao kwenda katika vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya kujifungua, inapaswa kuondoka kwasababu kujifungua kwa njia ya upasuaji ni njia bora zaidi na haina madhara kama wengi wanavyodhani.

‘’Sababu kubwa za kumfanyia mjamzito upasuaji ni pamoja na kuokoa maisha yake na mtoto, kumwepusha na Fistula na utindio wa ubongo kwa mtoto anayezaliwa’’ alisema Dr. Magoma.

Alitanabaisha kuwa hakuna miujiza ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto nchini badala yake jamii ihamasike kwenda kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali huku akitolea mfano wa nchi ya Sirlanka ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo hivyo huku Rais wa nchi hiyo akihusika kwa asilimia kubwa kutokomeza vifo hivyo.

2 Comments
  • UFAFANUZI MUHIMU KWA TAARIFA ZILIZOMO KWENYE MAKALA HAYA
    Inatia moyo kusoma makala hii ambayo inatoa mchango wake katika kuhamasisha jamii ya watanzania kufahamu ukubwa wa changamoto zinazowakabili mama zetu na vichanga wakati wa ujauzito na kujifungua. Katika tukio hilo adhimu la kuleta uhai duniani inasikitisha mno kwamba akina mama na watoto wachanga wengi hufariki hapa nchini.
    Ni muhimu pia kutolea ufafanuzi kuhusu baadhi ya taarifa zilizomo kwenye makala hii.
    Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa wanawake 8,500 na watoto wachanga 50,000 hapa Tanzania hufariki kila mwaka katika kipindi cha ujauzito na kujifungua. Ni takwimu za kushtusha sana. Ni muhimu kufafanua zaidi kuwa mtoto mchanga ni mwenye umri wa tangu siku 0 hadi 28, ikiwa ni pamoja na wanaozaliwa wameisha kufa. Kuna idadi nyingine kubwa zaidi ya watoto walio chini ya miaka mitano ambao hufariki kila mwaka (kama ilivyojumuishwa kwa makosa kwenye makala hii, badala ya vichanga peke yake). Ila izingatiwe kuwa vifo vya watoto katika siku 28 za kwanza za kuishi ni karibu theluthi moja ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano hapa Tanzania.
    Ukichukua takwimu za wastani wa wanawake 8,500 na vichanga 50,000 wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua kila mwaka nchini Tanzania, hii ni sawa na akina mama 23 na vichanga 137 wanaofariki kila siku. Hili ni janga, hasa ukizingatia kuwa wengi wa akina mama na vichanga hawa wangeweza kuokolewa kama wangepata huduma bora. Hata hivyo ni vigumu kuona na kuzingatia uhalisia wa kiwango na wingi wa vifo hivi katika maisha ya kila siku, hasa pale takwimu kubwa kama hizo zinapotumiwa. Hivyo basi ndiyo sababu ukawekwa mfano huu kueleza ukubwa wa janga hili la kuwapoteza mama zetu na vichanga kila siku.
    Ukisafiri ndani ya Tanzania kwa usafiri wa anga, kawaida ndege zinazotumika ni zile zenye kubeba abiria wapatao 30 hivi. Na ndipo tulipoona muafaka kutumia mfano wa vifo vya akina mama 23 na vichanga 137 kila siku, kuwa ni kama ndege tano za abiria zingeanguka kila siku, ambapo kati ya hizo ndege tano, ndege moja ingebeba akinamama na nyingine nne zingebeba vitoto vichanga. Kuielezea hali kwa namna hii ni kwa nia ya kufikisha ujumbe wa ukubwa wa janga hili linalozikumba familia na taifa kwa ujumla kila siku. Hebu fikiria kama kungekuwepo kweli na ajali tano za ndege kila siku—kungekuwa na taharuki kubwa sana na wanajamii wa ngazi zote kulikemea jambo hili kudai likomeshwe mara moja, huku juhudi za kila aina zingefanywa lisitokee tena.
    Ili kuboresha hali ya uzazi salama kwa kiwango kikubwa, ni muhimu sana wanawake wengi zaidi watafute nakupata huduma bora. Iwapo kila mama atajifungulia kwenye kituo cha tiba ambacho kinatoa huduma bora, akina mama wengi na vichanga tunaowapoteza kwa sasa wataokolewa. Kwa sasa wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya bado ni wachache: kwa mujibu wa utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) 2010 ni mwanamke mmoja tu katika kila wawili ndiye anayejifungulia katika kituo cha afya. Yaani kigezo cha hatua hii muhimu ambayo ingeweza kuchukuliwa na kupunguza vifo vya mama na vichanga kwa kiasi kikubwa kimekuwa hivyo hivyo katika kipindi cha miaka 25 bila mabadiliko. Hii ni tangu ulipofanyika utafiti wa TDHS wa kwanza 1990 ambapo ni nusu tu ya wanawake walikuwa wakijifungulia kwenye vituo vya afya.
    Na japo kwa usahihi kabisa, makala hii imeeleza kuhusu ongezeko la idadi ya vizazi hai katika vituo vya afya, ieleweke kuwa pia ongezeko kubwa la idadi ya watu hapa Tanzania linamaanisha kuwa mfumo wa afya nao haujaweza kufanya mabadiliko ya kuendana na kiwango cha ongezeko la wanawake wanaojifungulia vituo vya afya kati ya mwaka 1986 na 2010.
    Ujumbe mkuu hapa ni kuwa idadi kubwa ya akina mama na watoto wachanga wa Tanzania ambao maisha yao yanapotea wakati wa ujauzito na kujifungua kila mwaka yangeweza, na kwa hakika yanatakiwa kuokolewa. Kila mtu, kwa nafasi yake katika jamii ni lazima atambue fursa zilizopo, zinazoweza kugeuza mwelekeo wa janga hili linalotokea kila siku. Jitume, chukua hatua kuhakikisha mama zetu na vichanga wetu wanavuka salama kipindi hiki muhimu cha kuleta uhai

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *