WATOTO wa kike wanazaa watoto. Watoto wanaolewa. Watoto wanaacha masomo. Maambukizi ya virusi vya Ukimwi yanaongezeka huko ni wilayani ileje mkoani Mbeya.
Ingawa wazaliwa wengi wa wilaya ya Ileje wana kimo kifupi, lakini utawatambua wasichana ambao bado umri wao wangetakiwa kuendelea na masomo wakiwa wamebeba watoto katika migongo yao huku baadhi wakinyonyesha.
Hali hiyo haishangazi tena wilayani humo, bali sasa imekuwa ni kama sheria na hao si wote walioolewa bali ni baadhi yao huku wakiwa na furaha.
Unajiuliza kuwa yawezekana wanaume waliopeana nao mimba na baadhi kuwaoa walitumia udhaifu wa sheria ya ndoa inayoruhusu binti kuolewa akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi wake unagundua kuwa hata hiyo sheria hawaijui.
Chanzo cha mimba hizi za utotoni ni nini? Jibu ni kwamba licha ya njia za kawaida za kutongoza watoto hao wa kike pia baadhi yao wanapata mimba hizo katika masoko ya mazao yaliyopo eneo la isongole, Chitete na Kijiji cha Ikumbilo yaliyopo wilayani humo.
Mbali na mabinti wakiwemo wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari, pia baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakienda katika magulio hayo na kushawishiana na baadhi ya wafanyabiashara ambao wanafika maeneo hayo kisha hufanya ngono bila kinga.
Gulio la Chitete na Ikumbilo hayana nyumba za kulala wageni hivyo ngono nyingi hufanyika vichochoroni na kando ya mto Songwe uliopo kati ya Tanzania na Malawi hasa katika eneo la Ikumbilo.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii Novemba 2012 kwa muda wa wiki tatu, umebaini kuwa katika maeneo hayo kata ya Isongole na Itumba zina idadi kubwa ya mabinti waliopata mimba na baadhi yao kuolewa chini ya umri wa miaka 15.
Eneo la Ikumbilo linaongoza kwa wananchi waliojitokeza kupima na kubainika kuwa na maambukizi ya VVU huku idadi kubwa ikiwa ni wanawake.
Utafiti huo uliohusisha mahojiano ya baadhi ya wananchi wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo, wananchi hao hasa kijiji cha Ikumbilo, walikiri kutumia kinga ikiwemo mipira ya kiume kufanya ngono na wapenzi wao wapya mara mbili na ilipofika mara ya tatu na nne na kuendelea hawakutumia kinga yeyote kabla ya kupima afya zao.
Mwananchi Henry Kayuni anasema kuwa baada ya yeye kujitambua kuwa anaishi na virusi vya ugonjwa huo amekuwa akijitangaza na kupatiwa huduma na hospitali za nchini Malawi.
‘’Mimi na baadhi ya wenzangu tunachukua dawa na kupata huduma zingine Malawi Chitipa ikiwa ni pamoja na mayai kreti mbili kila mwezi hivyo tunaona ni vema tukaendelea kuhudumiwa Malawi kwasababu nchi yetu bado haijawa na mfumo kama wa Malawi.’’anasema Kayuni.
Baadhi ya mabinti wakiwemo wanafunzi licha ya baadhi kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, wamekuwa wakibeba mimba na kuzaa huku baadhi wakikiri kuwa hawawajui wazazi halisi wa watoto wao kutokana na kujihusisha na ngono zaidi ya mwanaume mmoja ambao si wakazi wa maeneo wanayoishi.
Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Hossana Ows Centre la wilayani humo linaloshughulika na masuala ya afya Nsanya Mwalyego, anasema kuwa mpaka sasa shirika lake linahudumia zaidi ya wananchi 350 ambao wanaishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Anasema idadi hiyo ni ya wananchi waliopo katika kata nne tu kati ya kata kumi na nane zilizopo katika wilaya hiyo ya ileje.
‘’Tunahudumia watu 350 waliojitokeza katika kata nne ambazo ni Itumba, Isongole, Chitete na Mlale tu ambao tunawafundisha jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya, kutojinyanyapaa na tunawapatia dawa baridi kwa wagonjwa wa majumbani wakiwemo wenye vidonda’’ anasema Mwalyego.
Alipoulizwa sababu za baadhi kutojitokeza kujitangaza na changamoto zonazowakabili, anasema wengi wao hawataki kutambulika na jamii wanayoishi nayo, hivyo wanakimbilia nchini Malawi ambako ndiko wengi wanapatiwa huduma na wanadai huduma za kule ni nzuri ikiwemo kuwapatia mayai wagonjwa.
‘’Changamoto kubwa tuliyonayo kuhusu watu kutojikeza katika upimaji wa afya zao ni kwamba wakienda wataalam ambao ni wenyeji huwa hawajitokezi lakini wakienda wataalam wageni wengi hujitokeza kupima afya zao na sisi hatuna uwezeshaji wa kutosha kutoka kwa wahisani na serikali’’anasema Mkurugenzi huyo.
Naye Jane Chaula ambaye ni mwelimishaji rika kutoka katika shirika hilo anasema kuwa hali ya mabinti chini ya umri wa miaka 18 kupata ujauzito imeshika kasi katika wilaya hiyo na wanafanya jitihada kubwa za kuendelea kuelimisha jamii kujikinga na maambukizi ya VVU na wale waliopata kutopata maambukizi mapya.
‘’Kuhusu hali hii ya mimba mimi mwenyewe nina mfano hai kutokana na binti yangu kupata ujauzito akiwa kidato cha pili katika sekondari ya Itumba day lakini namshukuru Mungu tulipompima hakuwa na maambukizi’’ anasema Jane.
Hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) alitoa takwimu za wanafunzi waliopata mimba katika kipindi cha mwaka 2010/2011 kuwa ni 998 kati yao 358 wa shule ya msingi na sekondari ni 640.
Pamoja na hayo, mkuu huyo wa mkoa alilalamikia tabia ya wazazi ambao watoto wao wanapewa mimba kukaa na upande wa mwanaume na kusuluhisha kienyeji na kuwaagiza maofisa elimu wote kuhakikisha wazazi wenye watoto waliopewa mimba nao wanabanwa, ili kukomesha tabia hiyo.
Hata hivyo jitihada za kupambana na suala la kuzuia mimba kwa wanafunzi na kuwabana wazazi kutoendelea kusuluhisha kesi hizo kienyeji linaonekana kuwa litaendelea kugonga mwamba kutokana na sheria inayoruhusu mabinti kuolewa wakiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi huku sheria hiyo ikikinzana na sheria Mama ambayo ni Katiba ainayomtambua mtu mzima kuwa ni yule mwenye umri wa miaka 18.
Hata hivyo hakuna sheria yeyote ya nchi inayokataza mtu mzima kuwa na mahusiano ya kingono na mwanafunzi wa shule ya Msingi, Sekondari hata vyuo lakini kuna sheria ya ubakaji kifungu 130 (2) (e) na 131 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ambayo adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 30 jela.
Wilaya ya Ileje ina jumla ya kata 18 ambazo ni Itumba, Bupigu, Chitete, Ifinga, Ikinga, Isongole, Itale, Kafule, Lubanda, Luswisi, Malangali, Mbebe, Ndola,Ngulilo, ngulugulu, Sange, Kalembo na Mlale.