Iringa yenye masoko yenye thamani yasiyotumika

Francis Godwin

KUWAPO kwa  masoko yasiyotumika katika Halmashauri ya Iringa  na  Manispaa ya  Iringa, pamoja na kujengwa kwa thamani kubwa ni ishara ya wazi kwamba yalijengwa kinyume na kipaumbele  halisi cha wananchi wa wilaya  hizo.
Miradi  mingi ambayo  huanzishwa kwa  matakwa ya   wananchi wenyewe huwa mkombozi  kwa  wananchi  wanaozunguka  miradi  hiyo na hata baadhi ya  miradi  kufanikisha  kuwakomboa  wananchi hao na hali duni ya maisha.

Ukitazama  sera  za  miradi  yenye ushiriki wa wananchi kama TASAF na hata  DADS   wananchi  wanapaswa kuchangia nguvu  zao  katika uanzishwaji  wa  miradi hiyo nah ii ndio siri kubwa ya mafanikio ya miradi hiyo katika utekelezaji na matumizi yake.

Katika utafiti uliofanywa na mwandishi  wa  makala  haya   katika miradi  ya ujenzi  wa masoko kwenye Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa na Iringa  vijijini  imebainika kuwepo kwa baadhi ya masoko ambayo yalijengwa kati ya  mwaka  2007 hadi 2009 hayatumiki.

Masoko haya kimsingi yamebaki kuwa makazi ya  ndege na wanyama wa  porini kutokana na kutotumika na   wananchi wanaozunguka masoko  hayo.

Sarah Sanga  ni  mkazi  wa Tagamenda  katika  Halmashauri ya wilaya  ya  Iringa vijijini  anasema kuwa Halmashauri  hiyo  ilipata  kuwajengea  soko  lililokamilika mwaka 2009 .

Soko hili kwa mujibu wa mwananchi huyo lilifanya shughuli zake kwa wiki mbili kabla ya  kuondoka na  kurudi katika eneo lao la mwanzo.

Anasema  kuwa  tatizo lililopelekea   kutoendelea  na biashara katika  soko hilo ni kuwa  mbali na makazi  ya  watu na hivyo  kukosa wateja  japo  wananchi   walishirikishwa katika  ujenzi  japo  baadhi  walikuwa wakipinga soko  hilo kujengwa  eneo hilo ambalo ndilo ardhi  ilipatikana .

“Hili  soko  sisi tulipendekeza  lijengwe eneo letu la biashara  ambalo ni  mita kama  800 kutoka eneo  hilo ila wao  walilazimisha  kujengwa hapa ….lakini tunajengewa  soko  bila  kupewa mitaji  tutauza nini hapa  sokoni wakati  sisi  biashara  zetu ni za  magengeni  na si za kuweka sokoni kama  wao  walivyotujengea  soko.”

Hata  hivyo  alisema  ni vema  eneo hilo la soko ili  kuweza  kuwavuta  wateja  zaidi na  wafanyabiashara wakageuza majengo hayo ya  soko kuwa klabu cha  pombe za  kienyeji  ambayo ndio  ina  soko kubwa katika kijiji  hicho.

Naye  Lusajo Kalinga  mkazi  wa  kijiji cha Muwimbi anasema  kuwa  wanashindwa kujua sababu ya  serikali kujenga  soko  eneo la Ulete wakati  wakijua  mahitaji yao  eneo hilo hayakuwa ni  soko bali   maji  safi na  salama ya  bomba  kwa  kipindi  hicho .

Hivyo alisema  sababu  ya  kushindwa  kuendelea  kwa  soko hilo ni kutokana na wananchi kutokuwa na tabia ya kuuza biashara  zao kwenye jengo la soko huku  kila mmoja akiuza  kivyake mitaani na baadhi  huuza  bidhaa zao katika klabu  cha  pombe.

Zuwena Mussa  mmoja kati ya  wananchi  wanaojishughulisha na biashara  ndogo nje  ya soko la Magari mabovu  kata ya Miyomboni Kitanzini katika Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa anasema kuwa  soko hilo linaendelea  kuchakaa bila  wafanyabiashara  kutumia  kutokana na wafanyabiashara kulipishwa ushuru wa Tsh 500 pale  wanapoingia kufanya  biashara  katika soko hilo huku  biashara  zao utokaji  wake ukiwa mdogo  zaidi.

Mstahiki  meya  wa Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa Aman Mwamwindi akizungumzia matumizi ya masoko, alitolea mfano soko   la  Magari Mabovu ambalo limejengwa na  Halmashauri  kwa msaada  wa SIP kupitia  mradi  wa Mazingira.Alisema  upo mkakati wa kulifufua soko la samaki kwa kuwaondoa  wauza samaki wote mitaani na kuwapeleka eneo hilo.

Mwenyekiti wa  serikali ya  kijiji cha Tagamenda  Joel Mofuga anasema  kuwa   soko   la Tagamenda  kuchakaa kwake kunatokana na wakazi hao  kugoma  kufanyia biashara  katika  soko  hilo na badala  yake  kuendelea  kulipa ushuru wa Tsh 500 kwa mtu  binafsi ambae anamiliki  nyumba  aliyoijenga kama  sehemu ya matumizi ya klabu  cha  pombe za kienyeji ambalo ni eneo  lililochangamka  zaidi.

Mofuga  anasema kuwa hivi   sasa mkakati  wa kijiji  hicho katika  soko hilo ni  kupigania  kuingiza umeme katika  majengo hayo  ili  kubadili matumizi ya  soko na kuweka shughuli kama za uungaji wa vyuma ,mashine za kukamua  alizeti  na shughuli nyingine rafiki na  wananchi  badala ya kuendelea  kuliacha  soko hilo  likiendelea kuchakaa.

Hata  hivyo anasema  mradi ambao  ungeweza  kuwakomboa   wananchi wa  eneo hilo ambao  wengi  wao  ni wakulima  ulikuwa ni mradi  wa bwawa la maji ambalo  lingeweza  kutumika kwa  kilimo cha umwagiliaji na kuwaongezea kipato  zaidi  wananchi wa  eneo hilo.

Abel Mgimwa ambaye ni afisa mipango  wa Halmashauri  ya wilaya ya  Iringa na kaimu mkurugenzi  wa Halmashauri hiyo anasema Halmashauri  yake  ina masoko matano  ambayo  yamejengwa kwa  ufadhili  wa DADS na masoko matano mengine yamejengwa  kwa ufadhili wa mradi wa DADPS .

Anataja  masoko ambayo yamejengwa na DADS kuwa ni Muwimbi, Ifunda kibaoni , Ilolompya,Itunundu na Tungamalenga na  kuwa kati ya masoko  hayo   ni masoko mawili ambayo  hayatumiki kabisa  likiwemo soko la Muwimbi na  Ilolompya  wakati mengine yanatumika  vema.

Kwenye  mradi  wa DADPS masoko  yaliyojengwa ni  Tagamenda , Ng’enza,Ndiwili  , Luganga na Kitayawa na  kuwa masoko ambayo hayatumiki baada ya  kujengwa ni Tagamenda na Ndiwili wakati yaliyobaki yanatumika  japo si kwa asilimia  kubwa .

Mgimwa ambae  ndie  alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi  wa masoko  hayo anasema  kuwa ujenzi  huo umeanza kati ya mwaka 2007  na kukamilika mwaka 2009 na  kuwa ukiacha soko la Ifunda  Kibaoni lililojengwa kwa Tsh milioni 38. 9 masoko  mengine yote  yamejengwa kwa zaidi ya  Tsh milioni 64 fedha  kutoka kwa wahisani.

Pia  anasema  kuwa si  kweli kama  wananchi  hawakushirikishwa katika ujenzi huo kwani  kabla ya  kuanza ujenzi vikao  vilifanyika na  wao kuonyesha maeneo  ya  ujenzi ila  baada ya  kujengwa  ndipo  walipoanza kususa  kufanya biashara katika masoko hayo .

Anasema  kuwa lengo la  kujenga masoko  hayo ni  kuwakomboa  wananchi ambao  wengi  wao  ni wakulima na masoko  hayo  yangewasaidia  kuuza mazao  yao  bila kuibiwa na  wafanyabiashara  ambao wamekuwa  wakinunua mazao majumbani kwa bei  wanayoitaka  wao .

Ofisa huyo pamoja na kueleza umuhimu wa masoko hayo amesema hataki kuamini kama  fedha  za ujenzi  wa masoko  hayo zimepotea kwani  tayari Halmashauri  imeanza  kuunda kamati za watumiaji wa masoko hayo  ili  kufufua masoko  yaliyokufa.

Aidha  alisema anashangaa kuachwa kutumika kwa masoko hayo kwani ni vyanzo vya mapato kwa Halmashauri za vijiji kwani asilimia 20 huenda Halmashauri na vijiji hupata asilimia 80  ya makusanyo  hayo.

Mratibu mkuu  wa miradi  hiyo Ofisa  kilimo wa mkoa  wa Iringa Adam Swai ambae ni katibu tawala msaidizi katika uchumi na uzalishaji anasema  kuwa  jumla  ya masoko 23 ndio  ambayo yamejengwa katika mkoa  wa Iringa kabla ya  kutengana na Njombe.

Hata  hivyo anasema  lengo la masoko hayo ni  kuwakomboa wakulima katika  soko na  kuwa na eneo  moja la kuuzia mazao  yao kwa  vipimo stahiki ,wazalishaji  mazao  na kuuza kwa bei yenye faida .

Anasema  japo  baadhi ya masoko  uendeshaji  wake si mzuri na yapo  ambayo yameanza kuchakaa bila  kutumia kama lile ya Ruaha Mbuyuni ,Lukani ,Magulilwa na Kitwiru  mjini  Iringa ambayo yote yamejengwa kwa pesa za ASDP – DADPS  ipo haja ya kuwa na mikakati ya  kuyafanya masoko  hayo kuanza kunufaisha  wakulima.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *