Wakazi Ziwa Nyasa kulipa gharama za uchafuzi wa mazingira

UCHAFUZI wa mazingira ni jambo linalostahili kupigwa vita katika kujiletea maendeleo. Kupigwa vita huko kunatokana na athari zinazokuja kujitokeza baada ya uchafuzi kufanyika. Nyingi ya athari zinaweza kuhatarisha usalama wa wananchi kiafya na kiuchumi.

Utafiti  wa Mwandishi wa Makala haya katika fukwe za ziwa Nyasa umeonesha kuwapo kw ahatari kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanyika kwa sasa.

Ufukwe wa Ziwa Nyasa wenye mchanga mdogo wa aina yake ambao ni kivutio kikubwa kwa wageni na hali nzuri ya hewa unakabiliwa na changamoto ya kutotunzwa ipasavyo wakati kuna sheria inayosimamia mazingira.

Sheria hii iliyopo  inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana  kuweka masharti na miongozo ya kuzuia na kudhibiti utoaji au umwagaji wa vichafuzi kwenye mazingira.

Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 inakataza kufanyika kwa shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya fukwe, shughuli ambazo zinaweza kuathiri vibaya uhifadhi na ulinzi wa fukwe za bahari na ukanda wa Ziwa, kingo za mito, mabwawa ya maji, au hifadhi ya maji ndani ya mita sitini (60) za eneo hilo.

Sheria inafafanua kuwa ni jukumu la mwananchi kupinga kubinafsishwa kwa fukwe zetu kwani fukwe ni zawadi yetu sote toka kwa mwenyezi mungu; Sheria hii pia inasisitiza kuwa, ni kosa kutoa au kutawanya kichafuzi ambacho kinachafuwa hewa kinyume cha kiwango kilichowekwa.

Kwa mujibu wa sheria hii kifungu namba 4 (1) na (2) kimeeleza kila mtu anayeishi Tanzania atakuwa na haki ya kuwa na mazingira safi, na salama kiafya inayohusisha haki kwa kila raia kutumia elementi za umma au sehemu mbalimbali za mazingira kwa madhumuni ya kiafya, kijamii, ki ibada, kiutamaduni, burudani, elimu na kiuchumi.

Sheria hii ya mazingira (2004) kifungu namba 5 (1) na (2) kimetamka wazi kuwa mtu yeyote anao wajibu wa kudai haki/kushtaki dhidi ya mtu ambaye kitendo chake kinaweza kusababisha au kimesababisha madhara ya ki afya au mazingira. Lengo la sheria hii katika kifungu namba 7 kinasema ni kuraghabisha na kuboresha uendelezaji, ulinzi, uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

Pia katika sheria hii kifungu namba 6 kimetamka kwamba mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira.

Lakini huenda sheria hii haijulikani kwa wakazi wa fukwe hizi na kama wanajua basi wanadharau kwa kuwa unakuwa ni utamaduni kujisafisha kw akupeleka uchafu ziwani.

Mmoja wa wananchi hao Victor Oddo (Zambia) mkazi wa Liuli ameshauri katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira iwekwe orodha ya wawindaji, wachoma mkaa, wachana mbao na wavuvi kwenye ofisi za watendaji wa vijiji na Kata ili uharibifu huo unapotokea wao wawe wa kwanza kuwajibishwa.

Hata hivyo Merina Charle naye pia mkazi wa Liuli, amesema wananchi wanatakiwa kubadilika kwani japo kwenye ofisi za Forodha kumejenga choo lakini bado wananchi wanajisaidia vichakani badala ya kwenye choo hicho.

Amesema wapo wananchi wengi ambao wanaishi hawana vyoo badala yake wanatumia vichaka vilivyo jirani na kwenye mito au wanapokwenda ziwani kuogelea hujisaidia humo jambo ambalo ni tatizo kwa afya za binadamu na viumbe wa majini.

Naye Josefu Ndomondo Mkazi wa Liuli anayefanya biashara ya kusafirisha watalii toka ufukweni kwenda kisiwa cha Pomonda na katika milima ya Livingstone amesema uchafuzi wa mazingira unasababishwa na wananchi kutofahamu umuhimu wa kutunza fukwe na kufumbiana macho ambapo wengine wanadiriki kufanya biashara ya kuuza fukwe na mchanga uliopo ufukweni mwa ziwa Nyasa bila ya kuchukuliwa hatua.

Amesema yeye binafsi wakati anasafisha eneo analoishi wananchi wenzake walimcheka sana na kumuita mwenda wazimu kwa nini anasafisha eneo ambalo halina makazi kwa hiyo ameomba mashirika na serikali ijitahidi kutoa elimu juu ya utunzaji wa fukwe na mazingira kwa ujumla.

Ameongeza kuwa uchafuzi huo unaendelea sambamba na kukosekana kwa barabara nzuri za kufika ziwani katika fukwe huku barabara zake zimechakaa na kuwa mapori na vichaka lakini  wananchi hawaoni umuhimu wa kuzisafisha.

Pamoja na uchafuzi imebainika kuwa wapo wananchi kutokana na kutothamini wala kufahamu thamani ya fukwe wanadiriki kuuza baadhi ya maeneo ya fukwe hizo kwa wageni jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya Taifa na wenyeji wa wilaya hiyo.

Mwandishi wa Makala haya amebaini kuwa asilimia 60 ya wakazi wa vijijini katika wilaya ya Nyasa hawana vyoo wala vizizi vya kuhifadhi mifugo ambapo unakuta mifugo inafugwa kiholela.

Katika uchunguzi wangu nimebaini kuwa fukwe zinazozunguka ziwa nyasa nyingi hazina vyoo na baadhi ambzo zimechimbwa vyoo vya kienyeji hazitumiki ipasavyo ambapo watu huendelea kujisaidia vichakani na ziwani.

Hali hiyo nimeibaini baada ya kutembelea fukwe mbalimbali za Ziwa Nyasa ikiwemo na fukwe ya Pomonda iliyopo Kata ya Liuli ambako kuna kisiwa kizuri cha kuvutia lakini hakuna vyoo vya uhakika kwa wageni wanaokuja kupiga kambi katika shughuli za uvuvi na ulanguzi wa mazao yatokanayo na Ziwa hilo.

Ushahidi wa kukosa vyoo unadhihirika pale unapotembea kuelekea Iwani na kuona vinyesi vikizagaa ovyo vichakani ambapo ni dhahiri kuwa wakati wa masika vinyesi hivyo husombwa hadi ziwani.

Nimeongea na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Odo Mwisho amekanusha kuwepo kwa uchafuzi wa kukithiri katika fukwe hizo amesema hali ilivyo ziwa Nyasa ni tofauti na maeneo ya bahari na maziwa mengine wao wanajitahidi.

Alipoulizwa kuhusu mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira hususani katika fukwe amesema kuna sheria ndogo ndogo ambazo zimewekwa katika jitihada za kuhakikisha fukwe zote zinakuwa safi wakati wote ikiwa ni pamoja na uundaji wa vikundi vya ulinzi wa mazingira kila kitongoji vinavyosimamia uharibifu wa aina yoyote.

Ameongeza kuwa miongoni mwa mikakati ni pamoja na kwamba wametenga siku maalumu ya usafi wa mazingira kiwilaya ambayo hufanya usafi wa mazingira kwa pamoja kila jumamosi ya mwisho wa mwezi siku ambayo wameiita siku ya Kahindi (Kahindi day) jina la Mkuu wa wilaya hiyo kama ni njia ya kuiweka wilaya katika hali ya usafi.

Mwisho amesema mikakati ya halmashauri katika kuhakikisha wanatoa elimu ya mazingira kwa wananchi wanatekeleza kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali kutoka ngazi ya mkoa ambao wanawapa kibali cha kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na athari za uchafuzi wa mazingira kupitia midahalo na makongamano kwa ushirikiano na wataalamu wa halmashauri.

Uchunguzi huu  umebaini wananchi wengi hawaifahamu sheria ya mazingira na wachache wanaoifahamu wanaifumbia macho kwa kuogopa kuelimisha wengine au kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka uhifadhi wa mazingira kutokana na imani za kishirikina na mila na desturi zinazowazunguka.

Inadaiwa wapo wananchi wanaolima kwenye vyanzo vya maji na kukata miti ovyo kiasi cha kusababisha jangwa pia wengine wanatupa uchafu ziwani lakini inapotokea mwingine anaonya au kumuadhibu mkosa katika jamii zile kunaibuka chuki na migogoro kwa nini kamsema mwangangu kutokana na tamaduni za wanyasa kuwa na sifa ya kujiona kila mmoja ana mamlaka na hawezi kufundishwa na mwenzie.

Nilipoongea na wavuvi juu ya athari wanazozipata kutokana na uvuvi wamesema wanakosa soko kwa kuwa wapo wachuuzi (walanguzi) wanaokwenda moja kwa moja ziwani kununua dagaa wanapokuta mazingira machafu wanapata sababu ya kununua samaki/ dagaa kwa bei wanazozitaka wao kwa visingizio vya uchafu.

Naye Mganga wa Wilaya ya Nyasa Dokta Papalika amekiri kuwepo kwa athari zitokanazo na uchafuzi katika fukwe hizo. 

Kwa maoni yangu nashauri, ni vizuri ikatolewa elimu zaidi kwa wananchi katika kuelimisha umuhimu wa uhifadhi na athari za uchafuzi wa fukwe ili uwekezaji uwe endelevu katika kuvutia wageni kutembelea fukwe hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *