Sekta ya Uvuvi Kigoma ipo mashakani

Emmanuel Matinde
Sekta ya Uvuvi ni kati ya sekta muhimu ndogo ya uchumi Tanzania. Sekta inatoa ajira nyingi, kipato, uchumaji riziki, fedha na  mapato ya kigeni kwa nchi.
 
Tasnia ya uvuvi inaajiri zaidi ya watu 4,000,000 wanaojishughulisha na uvuvi na shughuli zinazohusiana ambapo zaidi ya watu 400,000 wameajiriwa kwenye sekta hiyo.
 
Kulingana na Utafiti wa Hali ya Uchumi wa Taifa ya Mwaka 2009, Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.3 ya pato la taifa (GDP). Wastani wa ulaji samaki kwa kila mtu ni kilogram 8.0 na asilimia 30 ya ulaji wa protini ya wanyama inatokana na samaki.
 
Mkoani Kigoma Sekta ya Uvuvi ni moja ya nguzo tatu za Uchumi wa Mkoa wa Kigoma, ambapo mpaka kufikia Disemba Mwaka jana,sekta hiyo pekee ilikuwa ikichangia asilimia 8% kwenye pato la mkoa.
 
Nguzo nyingine ni Kilimo ambacho huchangia asilimia 82% na sekta ya biashara ambayo inachangia asilimia 10%. Kulingana na takwimu za mwaka 2010, sekta ya uvuvi kwa nchi nzima ilichangia asilimia 1.4%.
 
Licha ya mchango wake katika pato la mkoa na taifa, sekta hii ya uvuvi kwa muda mrefu imekabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa zaidi ni matukio ya wavuvi kuvamiwa na kuporwa zana zao za uvuvi na maharamia wanaodaiwa kuwa ni kutoka nchi jirani ya Congo DRC.
 
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1993 hadi mwezi April mwaka huu 2014, zana za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6, ambazo zilikuwa zikitumiwa na wavuvi katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma zimeishia mikononi mwa maharamia hao katika matukio mbali mbali ya uvamizi.
 
Zana hizo ni pamoja na Injini 1,234, Mitumbwi 278, Nyavu za kuvulia samaki 368, Taa 4,828 na Mafuta ya Petroli Lita 31,000.
 
Matukio mawili ya hivi karibuni la ujambazi katika Ziwa Tanganyika, yalitokea April 29 na Mei 5 mwaka huu ambapo maharamia wakiwa na silaha yalivamia wavuvi na kupora zana mbali mbali za uvuvi.
 
Tukio la kwanza la tarehe 29 lilitokea maeneo ya Nondwa na mlima Kibirizi, wilaya na mkoa wa Kigoma ambapo majambazi wakiwa na silaha walivamia wavuvi na kupora Injini saba za Boti na vifaa vingine vya uvuvi vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 22,105,000.
 
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Frasser Kashai, ilieleza kuwa katika tukio hilo majambazi hao walimteka nahodha mmoja wa boti za uvuvi Bw.Justine Benard, mkazi wa Katonga na kumuamuru awapeleke huko Kalemie katika jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo wakiwa na vifaa hivyo.
 
Hata hivyo nahodha huyo alionyesha kitendo cha kishujaa pale alipofanikiwa kuwatoroka maharamia hao akitumia moja ya boti zilizotekwa na kurudi nchini na kuokoa Injini 4 aina ya Yamaha HP 40, kati ya saba zilizoporwa, na Jenereta moja aina ya Tiger.
 
Katika tukio la Mei 5 ambalo lilitokea katika kijiji cha Mwamgongo Kata ya Kalinzi wilayani Kigoma, wavuvi walivamiwa na watu wenye silaha na kuporwa mtumbwi mmoja na Injini 2 HP 40.
 
Kamanda Kashai alisema kwenye tukio hili la pili polisi walifanya msako na kufanikiwa kukamata majambazi 3 kutoka Kabimba huko Congo DRC. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Ramadhani Kasongo (20), Ado Nonda (35),na Banza Monga (28), ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi wa awali utakapokamilika.
 
Matukio hayo ni mfano tu wa matukio mengi ya wavuvi kuvamiwa, kutekwa na kuporwa mali zao ambayo yamekuwa yakitendeka ndani ya Ziwa Tanganyika na kuwa tatizo kubwa linalozorotesha jitihada za wavuvi za kujiletea maendeleo.
 
Mbali na matukio hayo, matukio mengine yaliyotokea siku za nyuma ndani ya Ziwa Tanganyika upande wa Kigoma yamegharimu maisha ya watu, ambapo katika kipindi cha kuanzia mwaka 1999 hadi kufikia mwaka jana watu saba wamefariki kufuatia matukio hayo ya uvamizi.
 
Jambo lingine ni kwamba uvamizi wa mara kwa mara dhidi ya wavuvi sambamba na kuporwa zana zao za kuvulia samaki unasababisha nafasi za ajira zinazotokana na shughuli za uvuvi kupotea.
 
Uchunguzi unaonesha kuwa Mtumbwi mmoja au Kipe kimoja kama inavyojulikana, unapoporwa na majambazi takribani watu 10 hupoteza ajira. Kwa maneno mengine jumla ya watu 12,340 walipoteza ajira katika sekta ya uvuvi mkoani Kigoma,katika kipindi cha kati ya mwaka 1993 na mwezi April mwaka 2014.
 
Changamoto ipo kwa serikali ambayo mara kwa mara wavuvi wamekuwa wakielekeza kilio chao cha muda mrefu cha kuporwa zana zao za uvuvi na kusababisha hali yao kimaisha kuendelea kudorora licha ya kuwa na rasilimali ya Ziwa Tanganyika.
 
Serikali ya Mkoa wa Kigoma mara kwa mara imekuwa ikieleza kuvalia njuga tatizo hilo kwa kushirikiana na wenzao wa Congo DRC, lakini bado wavuvi katika Ziwa Tanganyika wangali
Je kuna mikakati gani endelevu ya kukabiliana na tatizo la ujambazi katika Ziwa Tanganyika?
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, alisema ipo mikakati ya kudumu wa kukabiliana na tatizo la ujambazi ndani ya Ziwa Tanganyika upande wa Kigoma, bila kubainisha mikakati huo akidai sio wakati wake kuibanisha mikakati hiyo.
 
“Upo mkakati wa kudumu, hatuhitaji kumwaga mtama palipo…; Kiswahili kinaeleweka hicho, lakini mikakati ya kudumu ipo, sio mahali pake hapa kwa kweli,”alisema.
 
Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma aliushukuru ubalozi mdogo wa Congo kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa pindi matukio hayo yanapojitokeza, ambapo aliahidi kwamba nchi hizi mbili zitaendelea kushirikiana kukabili suala hilo pamoja na kuhakikisha Injini zilizo mikononi mwa majambazi zinarudi.
 
Aidha aliwataka wavuvi kutoajiri watu wasiowafahamu kwenye shughuli zao za uvuvi, hatua ambayo wavuvi wameanza kuichukua.
 
Hii ni kutoka na kuwepo kwa hisia kwamba majambazi katika Ziwa Tanganyika ambao wanadaiwa kuwa wanatoka nchi jirani ya Congo DRC, labda wana washirika wao eneo la Kigoma wanaowasaidia kufanikisha uhalifu wao nao ni wale wanaodhaniwa kuwa pia ni raia wa Congo DRC.
 
Mwenyekiti wa Wavuvi Mkoa wa Kigoma Ramadhani Kanyongo, alisema wameanza kuchukua hatua kwa kuagiza kila mwalo wa wavuvi kuweka sensa ya wenye mali na wafanyakazi wao ili waweze kutambuana.
 
“Siku za nyuma tulikuwa tunapeana kazi kienyeji kienyeji, lakini hivi sasa tumewaagiza viongozi wote wa mwalo wahakikishe kila mwenye chombo anakuwa na takwimu ya wavuvi wake wale wa kudumu,”alisema.
 
“Lakini tusiajiri mtu hatumjui kule anakotoka kuja leo anafika unampa kazi. Hicho hata sisi tumeshakikataa. Ni lazima pale tunapopewa mwongozo na viongozi wa serikali na sisi tutii.”
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishina Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Frasser Kashai, alisema ofisi yake inazo taarifa za kuwepo kwa mtandao wa baadhi ya raia wa Tanzania hususan wanaoishi katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambao wana mahusiano ya karibu na watu wanaovamia na kuteka wavuvi na kupora mali zao.
 
“Raia wema walishatupatia majina ya watu hao, tutawasaka mmoja mmoja mpaka tuwakamate na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,”alibainisha Kamanda Kashai.
 
“Lakini nachosema tu ni kwamba vile vile doria yetu sasa hivi ya majini ipo saa 24. Muda wote tupo kazini japokuwa eneo letu la operation ni kubwa, lakini tutajitahidi kwa kushirikiana na wavuvi kuhakikisha kwamba tunalipunguza tatizo hili la wizi wa ziwani.”
 
Balozi mdogo wa Congo DRC katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo uliopo mkoani Kigoma Bw.Rick Molema, alikiri kwamba kuna vikundi Fulani vilivyoko nchini kwake eneo la Kalemie, ambavyo vinaifahamu vizuri Kigoma ndivyo vinavyofanya ujambazi katika Ziwa Tanganyika.
 
Alisema miaka miwili iliyopita vikundi hivyo vilikuwa vimedhibitiwa lakini sasa vimeanza tena.
“Sisi kama ubalozi tunafanya kazi pamoja na polisi, tunatoa taarifa kamili juu ya kile tunachokifanya, tunajua mipango yetu jinsi tulivyopanga na kwa muda mfupi mtaona matokeo yake,”alisema.
 
Alisema kuwa serikali ya mkoa wa Kigoma inajitahidi kujenga mazingira mazuri ya kuendeleza mkoa kiuchumi ujenzi wa bandari kavu na miradi mingine ya uwekezaji, na kwamba wao kama serikali ya Congo DRC, hawawezi kuacha majambazi waendelee kuhujumu miradi ya maendeleo ya jirani zao.

Pichani ni mkuu wa mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, mwenye suti nyeusi pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wakiangalia zana za uvuvi zilizorudishwa baada ya kuporwa na majambazi kutoka Congo DRC.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *