Matumizi ya sheria na busara kumaliza mgogoro mgodi wa Rwanda

Utatatuzi wa Mgogoro wa Fidia kati ya wawekezaji na wananchi katika maeneo ya mgodi wa Makaa ya Mawe Rwanda wilayani Mbinga utategemea busara ya Serikali. Hii inatokana na ukweli kuwa bila busara, kutumia sheria na uelewa kunaweza kuzuka mgogoro wa muda mrefu utakaozuia uendelezaji wa mgodi.

Kumekuwa na lawama za mara kwa mara kuhusiana na wananchi waliohamishwa kutoka maeneo yao ya asili ili kupisha uchimbaji wa madini kwa kutolipwa fidia ya ardhi zao. Pia wananchi wanalalamika kutopata sehemu ya mrahaba licha ya maisha yao kuathiriwa na shughuli za uchimbaji.

Miongoni mwa malalamiko ya wananchi ni pamoja na hali inayoonekana ya sekta ya madini kutochangia vya kutosha katika maendeleo ya nchi hasa ya kiuchumi na kijamii.

Imeonekana kuwa ushiriki wa kampuni za madini katika maendeleo ya jamii, wananchi wengi hawaridhishwi na kiwango cha mchango wa kampuni katika maendeleo yanayopatikana katika maeneo ya migodi hiyo

Mwaka 1998, Serikali ilitunga sheria mpya ya madini na kuifanyia marekebisho Sheria ya Fedha za kigeni (The foreign Exchange Act, 1992) ili kukidhi mahitaji ya sekta ya madini na kuzingatia Sera ya Madini ya 1997

Uchunguzi umebaini kuwa mara nyingi migogoro huibuka katika maeneo mengi duniani inayotokana na kutokuwa na makubaliano na wananchi wanaoishi katika maeneo yenye migodi ya Madini.

Migogoro hiyo imekuwa ikitokea pindi wananchi wanapotakiwa kuhama makazi na kutakiwa kulipwa fidia zao za usumbufu na za kujikimu baada ya kufanyiwa tathmini.

Mwandishi wa Makala haya amebaini kwa hapa Tanzania yapo maeneo mbalimbali ambayo yamejikuta yakiingia katika Migogoro baada ya kugundulika uwepo wa Rasilimali za Madini na kupelekea migogoro kati ya mwekezaji na wananchi hata kupelekea watu kujeruhiwa na hata kupoteza maisha.

Hali hiyo inajitokeza wakati kwenye mapitio ya sera ya madini imeonekana kuwa kufuatia umuhimu wa sekta ya madini Serikali ilipitisha Sera ya Madini ya Mwaka 1997 ikiwa na madhumuni ya kuchochea utafutaji na

uendelezaji wa uchimbaji madini, kuboresha uchimbaji mdogo wa madini, kupunguza umaskini, kuimarisha miundombinu ya kijamii na kiuchumi, kuingiza fedha za kigeni na mapato kwa serikali.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa ambayo imebahatika kuwa na Rasilimali za Madini ambapo baada ya kugunduwa kuwepo kwa Rasilimali hizo taratibu za tathmini zilianza kama ilivyo kawaida ili kupisha kazi ya uchimbaji kuanza.

Mwandishi wa Makala haya anaelezea Mgodi wa Makaa ya Mawe uliopo Wilaya ya Mbinga katika Kata ya Rwanda Tarafa ya Nanswea Kijiji cha Mtunduwalo ambako inakadiriwa kuwepo madini ya makaa ya mawe kiasi cha Tani Milioni 400 kufuatia utafiti uliofanywa na wataalamu.

Utafiti huu umebaini baada ya kupatikana mwekezaji katika mgodi huo taratibu za tathimini zilianza kupitia Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na Mwekezaji aliyewekeza mgodini hapo Kampuni ya Tan Coal kwa ufadhili wa Kampuni ya Atomic Resources Limited ya Australia ili kuwezesha kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi katika eneo la mgodi.

Inaelezwa Tathmini hiyo imefanyika na Mtathmini wa Serikali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Faraji Kaluwa na baada ya kutathmini  wafadhili walmewalipa wananchi fidia kiasi cha shilingi  2,118,892,536  ambazo zimedaiwa na wananchi hao kuwa ni ndogo na hazitoshi kwa ujenzi.

Watathimini hao kutoka halmashauri ya wilaya ya mbinga wamefanya tathimini ya kwanza kwa kaya 440 ambapo kampuni ya Tan Coal imelipa Fidia Yenye Thamani Ya Shilingi 2,118,892,536 kwa kaya zilizofanyiwa uthamini.

Mtathimini wa majengo kutoka wilaya ya Mbinga Faraji Kaluwa amesema katika kufanya kazi ya tathimini kuna kuwa na uajibikaji mkubwa kwa kufuata kanuni,taratibu na sheria.

Kaluwa amesema kabla ya kufanya tathimini hiyo walikaa Kikao na wananchi kuwapa elimu na mwongozo wa namna watakavyotoa fidia hizo na kuwajulisha nini wanakwenda kutathmini na wananchi wakakubalina.

Kuluwa ameongeza kuwa wamewaambia wananchi kuwa wao wanatathmini kile kinachoonekana na kwamba tathmini yao inajumuisha ardhi na maendelezo kwa kulipa kile ambacho wamekiwekeza.

Amesema upande wa nyumba wameangalia aina ya ujenzi ulliotumika,  umetumia bati za aina gani, mwezeko wa aina gani kama ni ya tofali tofali za aina gani na pia hali ya nyumba ikoje imechoka au bado nzima na tathmini imefanyika vilevile kadiri ya hali halisi waliyoikuta, hawajalipa zaidi ya kile walichokiona kwa na kwamba tathmini inaongozwa na  vipimo ambavyo huwa wanavichukua.

Mtathmini huyo amesema sambamba na malipo hayo pia wamelipa Malipo ya Fedha za usumbufu(Distabance Allowance),  Fedha ya usafiri (transport Allowance)  na fedha ya kujikimu/ pango (Accomodation allowance ambayo kisheria hutolewa pango ya miezi 36 sawa na miaka mitatu.

Amefafanua kuwa kisheria fidia ya usafiri inakuruhusu kwenda umbali usiozidi km 12 fidia ya kuwezesha kusafirishia mizigo, pia amesema sheria hairuhusu kumfanyia uthamini mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18 isipokuwa kama ameachiwa urithi wa nyumba ambapo sheria inamtaka awe na mdhamini aandikwe jina na uhusiano wake na mtoto ndipo akithibitishwa anafanyiwa tathmini na ndiye anayepokea malipo.

Wananchi wanaoshi maeneo ambayo mgodi upo wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kiwango walicho kadiriwa kime kuwa kidogo sana hakiendani na gharama za ujenzi kwa kipindi hiki kiasi kwamba hata nyumba za bati walizozijenga awali hawatamudu kuzijenga wanako hamishiwa kutokana na fidia ndogo walizokadiriwa.

Wakitoa mifano ya Fidia walizokadiriwa wananchi hao wamesema mtu mmoja mwenye familia anakadiriwa Sh. Milioni 4 mpaka laki sita fedha ambayo kwa kulinganisha na gharama za ujenzi kuwa juu haziwezi kukidhi kukamilisha ujenzi na kwamba hapo wanapoishi walipanda miti ya matunda na mazao mengine yanayowaingizia pesa ya kujikimu.

Wananchi hao wamesema licha ya kupunjwa wengine hawakukadiriwa kabisa pia kuna mambo ambayo wawekezaji walihaidi kuwatekelezea na kukamilisha baada ya miaka mitatu jambo ambalo hadi hivi sasa halijatekelezwa wameiomba Serikali kuangalia kwa makini pande zote mbili.

Wamesema kuna ahadi nyingi ambazo walihaidiwa kulipwa ikiwa ni pamoja na fedha za usumbufu, pango na makaburi ambazo hawajatekelezewa na hawafahamu mapunjo waliyopunjwa wamepunjwa na nani kati ya mwekezaji na Serikali.

Wananchi hao wameshauri Serikali ingebaki katika kusimamia na siyo kupanga bei kati ya mwekezaji na serikali halafu wananchi wamepewa maelekezo kuwa utalipwa kiasi hiki wameona huu ni uonevu na kwamba hawakutendewa haki.

Miongoni mwa Wananchi wanaolalamikia Mapunjo ya Fedha za Uhamisho ni pamoja na Teodesia Betram Mkwera  Mkazi wa kijiji cha Rwanda amesema wao hawakatai kuhama bali wanacholalamikia ni pesa ndogo waliyokadiriwa kwa kulinganisha na hali ya sasa amesema kiasi cha Sh. Milioni 4 hadi laki 6 kwa mtu mwenye Nyumba, Mashamba na Miti ya Matunda haiwezi kukidhi kwenda kujenga anakotakiwa kuhamia.

Ameongeza kuwa Pesa waliyopewa Milioni 4 sio kwamba hawajaitumia wamenunua Vifaa kama bati, boriti, Misumari na Vifaa vingine vya ujenzi na kujikuta wameishiwa pasipokubakiwa fedha ya usafiri wala ya Ujenzi hivyo hawaelewi watajenga kwa pesa ipi.

Naye Juma Alfred Komba Mkazi wa Liyombo ameomba Serikali iwafikirie kwa kina kuwaongezea pesa  badala ya milioni nne waliyopewa kwa kuwa kwa hali ilivyo sasa huwezi kujenga nyumba ya bati kwa pesa hiyo vinginevyo watawasababishia familia kukimbia kwao na kwenda mjini kufanya kazi za ukahaba.

Juma ameongeza kuwa wao hawana nia mbaya na Serikali wala mwekezaji wanaipenda nchi yao na wanafahamu kuwa Maendeleo yoyote yanayopatikana ni ya wananchi wote, amesema wapo waliokadiriwa Milioni mbili  hadi laki sita fedha ambayo akinunua boriti na Bati inakuwa imeisha  na kwamba wana miti ya matunda na miti ya mikorosho ambayo inawaingizia kipato, mti mmoja wa mkorosho anapata gunia mbili na akiuza anapata laki sita halafu leo fidia ya mti huo anapewa elfu kumi itamsaidia nini.

Wameyataja baadhi ya Mambo ambayo mwekezaji alihaidi kutekeleza ni pamoja na upatikanaji wa umeme ambao kupitia mtambo wa umeme ungeweza kutoa ajira kwa wananchi wasiopungua 400 mradi ambao utekelezaji wake ulitakiwa kukamilika 2013 lakini mpaka sasa haujakamilika.

Pia wamesema ahadi zingine ni zile za kusogeza huduma karibu kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ukarabati wa miundombinu ya Barabara na Ujenzi wa Shule, pia wamelalamikia Kampuni hiyo kuchangia kuharibu Miundombinu ya Barabara kama madaraja kutokana na uzito wa magari yanayosafirisha Makaa ya Mawe ya Kampuni hiyo kuzidi uwezo wa Daraja hizo.

Kutokana na Malalamiko hayo na kutoelewana baina ya wananchi na Serikali kumepelekea wananchi kufanya maandamano na kuziba Barabara ili gari za Kampuni ya Tancoal zinazosafirisha Makaa zisipite na Makaa.

Wananchi hao walifunga njia kwa siku 2 na baadaye Polisi kikosi cha kutuliza ghasia kutoka Makao makuu ya Mkoa Songea walikwenda katika eneohilo kutuliza ghasia ambako kulipelekea watu kujeruhiwa na wananchi 20 waliwekwa ndani (Rumande) kwa kile kilichoitwa ni kuleta uchochezi na kuongoza maandamano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa RuvumaDeusdedit Nsimeki amewaomba viongozi wa Serekali walioteuliwa kuwaongoza wanachi wasiwe chanzo cha Machafuko katika maeneo yao.

 Kamanda huyo wa Polisi ameyasema hayo baada ya kuwakamata viongozi watano wa serikali ya kijiji ambao walikuwa wakiongoza kuzuia magari ya Kampuni ya Tan Coal  kusafirisa Makaa ya Mawe hadi walipwe fidia zao za makaazi walizo punjwa

 Kamanda Nsimike amesema kuchukua Sheria mkononi ni kosa la Jinai wananchi wanatakiwa kudai haki zao kwa kupitia Mahakamani au kutumia vikao halali vilivyo idhinishwa pia amesema kutumia watoto wadogo na wanawake kwa kuwalaza barabarani katika mgomo ni kukiuka haki za binadamu .

Utafiti huu umebaini kuwa hadi sasa wananchi hawajahama na Serikali imeendelea kumruhusu mwekezaji kuendelea na uchimbaji wakati wananchi waliotakiwa kufanyiwa uthamini upya hawajafanyiwa tena.

 Mgodi wa Makaa ya Mawe Mbinga uligundulika mwaka  2006 ambapo  wananchi wanaoishi Kijiji cha Mtunduwalo Kata ta Rwanda Tarafa ya Nanswea walijikuta hatarini kuteketea kwa Moto baada ya kugunduwa kuwepo kwa mlipuko wa moto uliokuwa ukiunguza Makaa ya Mawe.

Inadaiwa pengine eneo hilo liliwahi kuchimbwa Makaa ya Mawe na Wajerumani Mwaka 1945 na Uchimbaji huo ulikoma Mwaka 1953, hata hivyo Tabaka la Makaa ya Mawe limepitia katika Makazi ya watu katika vijiji vya Mkapa, Ngaka, Liyombo, Mkulu na Mbuyula.

Jitihada za kuuzima moto huo zilianza mara baada ya Mzee Mapunda Mkazi wa Kijiji cha kugundua kuwaka kwa moto huo ambapo baadhi ya waandishi akiwemo Mwandishi wa habari wa Star Tv, Adam Nindi alifika katika eneo hilo mwaka 2006 na kutangaza uwepo wa hatari ya wakazi wa eneo lile kuteketea kwa Moto uliokuwa ukiwaka chini kwa chini uliodhaniwa huenda chini kuna Madini yalikuwa yakiteketea.

Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania baada ya kusikia kilio cha wana Mbinga juu ya hatari ya kuteketea kwa Moto ili tuma watalamu wake kufanya utafiti ili waweze kuudhibiti usiendelee, katika jitihada hizo Serekari ilitumia shilingi milioni 59 kufanikisha kuuzima moto huo.

Hata hivyo Sheria ya madini ya mwaka 2010 na Sera ya madini ya mwaka 2009, ambazo kwa pamoja zinaruhusu serikali kuwa na ushiriki wa kimkakati katika miradi ya uwekezaji mkubwa wa madini kama itakavyoona inafaa, ikiwa ni njia ya kutatua matatizo ya kutokuwa na uwekezaji wa ndani wenye hisa katika maeneo ya mgodi.

Kwa Maoni yangu nashauri Serikali inapotokea sehemu zenye rasilimali kama hizi wanatakiwa watoe elimu mapema kwa wakazi wa eneo kabla ya mwekezaji kuanza kazi pia wanapofanya tathmini waangalie na uhalisia wa gharama za ujenzi kwa wakati ambao wanatathmini kwa kuwa hata kama nyumba imechoka huwezi kuijenga kwa gharama ulizojenga awali pia haihamishiki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *