Ukosefu wa zana bora wakwamisha maendeleo Nyasa

UMASKINI ni kitendo kinachopigwa vita na Mataifa mengi Duniani ikiwa ni pamoja na nchi zinazoendelea.
 
Umoja wa Mataifa katika mikakati ya kupunguza umaskini na kukuza uchumi tangu mwaka 1953 umetenga siku maalum ya kujadili mbinu za kupunguza umaskini na kuinua uchumi, ambapo kila tarehe ishirini na saba ya mwezi wa kumi na moja wadau mbalimbali huandaa kongamano la kujadili mikakati hiyo.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea duniani ambayo ina mipango na mikakati mbalimbali katika kupigana na adui umaskini kwa kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na umaskini na kukuza uchumi.
 
Mwandishi wa Makala haya amebaini kuwa maskini mara zote ana nafasi finyu ya kupata fursa, na kwamba hata kama anakuwa na fursa ya kumwezesha kuondokana na umaskini anakosa nyenzo au elimu ya kuweza kunufaika na fursa zinazomzunguka.
 
Umaskini ninaouzungumzia katika makala haya ni umaskini unaotokana na wananchi kukosa fursa ya kunufaika na rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao kutokana na ukosefu wa nyezo za kumwezesha kujikwamua na umaskini huo.
 
Fursa ninayoizunguzia hapa ni Rasilimali muhimu ya Ziwa Nyasa linalopatikana wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma kwa upande wa Tanzania ambapo wananchi wake wanakabiliwa na umaskini kutokana na ukosefu wa zana bora za kuvulia.
 
Wilaya ya Nyasa yenye ukubwa wa kilometa za mraba 3811 Uchumi wake mkubwa unategemea mapato yatokanayo na Ziwa nyasa (uvuvi)   na kilimo.
 
Ziwa Nyasa ambalo linakadiriwa kuwa na tani zisizopungua 165,000 za samaki ndani yake kukiwa na aina 500 za samaki wakiwemo, hangu, mbasa, mbelele, sflish, vitui, dagaa, kambale na mbufu.
 
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa wilaya ya Nyasa kwa mwaka inavuna Tani elfu kumi tu za samaki zikiwa na thamani ya shilingi bilioni nane.
 
Wataalamu mbalimbali wakiwemo Maafisa Uvuvi wa wilaya hiyo wanadai kuwa kutokana na kukosa zana bora za kuvulia wavuvi wa wilaya ya Nyasa hulazimika kwenda umbali usiopungua kilometa mbili na kushindwa kwenda kwenye kina kirefu ambako samaki wa uhakika wanapatikana.
 
Wamesema inawalazimu kuishia umbali huo kutokana na kutumia mitumbwi ambayo haina uwezo wa kwenda kina kirefu na wakati mwingine samaki wanapatikana kwa wingi ambapo hutumia mitumbwi hiyo kubebea na wanapozidiwa uzito kwa kuhofia usalama wao majini wanaamua kupunguza dagaa au samaki waliovuliwa kwa kuwamwaga ziwani ili kupunguza uzito.
 
Kwa habari za kuthibitishwa nimeongea na baadhi ya wavuvi ambao wamesema wanashindwa kufikia lengo la kuondokana na umaskini kutokana na ukosefu wa zana bora za kuvulia ambapo wanaishia kwenye kina kifupi kwa kuhofia kuzama na kupoteza maisha.
 
Wamesema wanashindwa kunufaika na uvuvi kwa kukosa zana bora kama boti zenye ingine na kujikuta wanaonufaika zaidi na ziwa hilo ni wavuvi wa nchi ya Malawi ambako kina cha maji siyo kirefu kama kilivyo upande wa Tanzania.
 
Hata hivyo imeelezwa kuwa kutokana na matumizi ya ngalawa na mitumbwi katika uvuvi baadhi ya wavuvi wamepoteza maisha baada ya kuzidiwa na mawimbi dhoruba linapopiga.
 
Kwa habari za kuthibitishwa na Mganga mkuu wa wilaya ya Nyasa Dr. Papalika amesema kwa mwaka watu wasiopungua sita wanapoteza maisha kutokana na matumizi ya zana duni.
 
Uchunguzi huu umebaini kuwa wilaya ya Nyasa mpaka sasa ina Mitumbwi 1550 na Boti za Ingine 20 wakati mahitaji halisi ni Boti 200.
 
Inadaiwa baadhi ya vikundi vya uvuvi waliobahatika kupata Boti moja moja wanakumbana na changamoto ya vipuri vya kuweza kufanyia matengenezo zinapoharibika kwa kuwa hakuna karakana ya kuuza vifaa vya boti hizo.
 
Wavuvi wa Wilaya ya Nyasa wameiomba Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwenda kuwekeza wilaya ya Nyasa kwa kuwakopesha boti za kisasa na kuweka karakana yenye vifaa vya kuweza kufanyia matengenezo boti hizo zinapoharibika.
 
Pia nimeongea na wanakikundi cha uzalishaji dagaa mbamba bay wakiwakilishwa na katibu wake Lucia Mapunda amesema wanakabiliwa na ukosefu wa sehemu maalum za kukaushia dagaa wakishavuliwa badala yake wanakausha kwa kutumia vichanja au wanazianika kwenye mchanga laini jambo ambalo linapunguza ubora wake.
 
Wamesema wangewezeshwa kujengewa karakana kubwa ya kuwezesha kuhifadhi dagaa wanazozikusanya na mahali pa kukaushia, wanaamini dagaa zingekuwa na soko na wao wangepunguza umaskini.
 
Miongoni mwa wavuvi nilioongea nao ni pamoja na Charles Makenzie mkazi wa Lituhi amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa soko la uhakika, hawana mahali pa kuuzia, dagaa wanapokuwa wengi wanalazimika kusafiri nazo wenyewe kwenye makapu na kwenda kutafuta wachuuzi Songea mjini ambako wanauza kwa bei ya chini.
 
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Shaibu Mnunduma amekiri kuwepo kwa changamoto hizo katika sekta ya  uvuvi ambapo amesema serikali ina mikakati ambayo inapanga katika kuwawezesha wavuvi ambako kutawafanya waongeze pato la ndani ya halmashauri na taifa kwa ujumla.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa bado ni changa,  toka ilipoundwa ina miezio saba lakini miongoni mwa maboresho wameazimia baada ya miaka miwili kuhakikisha wameinua pato kutokana na uvuvi wa samaki na uchumi wa wananchi wakiwemo na wavuvi.
 
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miezi saba toka kuanzishwa kwa halmashauri hiyo na baada ya kusimamia katika ushuru utokanao na samaki wamekusanya shilingi milioni miamoja kutoka kwenye milioni kumi walizokuwa wanakusanya.
 
Amesema mkurugenzi huyo; ni imani yao kuwa wakiwatafutia wavuvi boti zenye uwezo na ubora watakuwa na mapato mengi zaidi. Katika jitihada hizo amesema mpaka sasa wamehamasisha wazawa wa wilaya hiyo ambao wana uwezo wanaoishi maeneo mbalimbali kuja kusadia boti kwa wavuvi wa Nyasa ambapo wamekubali kuchangia shilingi milioni 300 zitakazogawanywa katika maeneo matatu ikiwemo na ununuzi wa boti za kuvulia.
 
Mnunduma ameongeza kuwa wanaendelea na jitihada ambapo pia wameandika mradi UNDP kupitia Profesa Mbele mhadhiri wa Chuo Kikuu na mzawa wa Wilaya ya Nyasa (Kilosa), wamepata mradi wa miaka minne ambao utekelezaji wake unaanza mwezi wa sita mwaka 2014 na kwamba katika mradi huo wamepanga kununua boti za ingini zipatazo 500 ili kuwasaidia wavuvi wa wilaya hiyo waweze kuvua kwa tija.
 
Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo amesema wito wake mkubwa kwa wananchi na wadau mbalimbali mkoani Ruvuma na nje ya mkoa wanaokwenda kufanya biashara zitokanazo na Ziwa nyasa wasikimbie kuchangia ushuru ili kuinua maendeleo ya wananchi wa mwambao wa ziwa Nyasa.  
 
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni miongoni mwa Wizara za Sekta ya Uchumi ambayo iliundwa mwaka 2010 kupitia tangazo la Serikali Na 494 (A) na miongoni mwa majukumu iliyopewa ni pamoja na Kusimamia maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi ziweze kuchangia pato la taifa, kukua kwa uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kilishe na kimapato;
Wizara inatekeleza majukumu haya kwa kuzingatia masuala ya kiuchumi mkuu (macro-economy) kitaifa yakiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025), Malengo ya Milenia (MDGs), Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II), Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) ya Mwaka 2010 na masuala ya kiuchumi ya ngazi ya kisekta (micro-economy) ambayo yanajumuisha Sera ya Taifa ya Mifugo (2006), Sera ya Uvuvi na Mikakati yake (1997), Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo (2011), Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi (2012).
 
Hata hivyo mwandishi amebaini kuwa Dira ya Wizara inatamka kuwa ifikapo mwaka 2025 kuwe na rasilimali za uvuvi zinazoendelezwa na kutunzwa katika mazingira endelevu, kibiashara na ushindani wa soko na kukua kiuchumi kwa viwango vikubwa na kuboresha maisha ya wananchi.
 
Binafsi nashauri kwa maoni yangu: Mipango ya Wizara na Serikali ya Halmashauri ni mizuri katika kukuza uchumi isipokuwa wajitahidi kuhakikisha utekelezaji unakwenda sambamba na vitendo na si kwa maneno maana uzoefu unaonyesha Nchi yetu imekuwa na mipango mingi mizuri ambayo haitekelezwi kama inavyokusudia na pengine unakuta mwisho katika utekelezaji wananufaika wageni na kuwaacha wazawa wakiendelea kufa maskini.
 
Nashauri viongozi na wasimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa wakifanikiwa mipango yao waangalie sana wananchi wa maeneo yao katika kuwawezesha kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kutosha ya namna ya kuweza kujikwamua na matumizi ya boti hizo zikishafika wasibague.

Utafiti wangu umegundua kuwa Wananchi wa Wilaya ya Nyasa wana kiu ya kuwa na mabadiliko na kupata maendeleo tatizo kubwa ni uelewa na watu hawaendi kutoa elimu ya aina yoyote kwa kuwa ni pembezoni na ikizingatiwa ni wilaya changa  ambayo ipo umbali wa km 176 toka makao makuu ya mkoa na miundombinu ya barabara si mizuri hasa kwa wakati wa masika wanasema wanapata elimu mara chache sana kupitia asasi za kiraia vinginevyo wanabaki kuwa nyuma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *