UFISADI: Mkuu wa mkoa amwomba Pinda kuivunja Halmashauri!

Jamii Africa

JINAMIZI la tuhuma za ufisadi zinazoikabili Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, limeanza kuchukuwa sura mpya, baada ya Mkuu wa Mkoa huo kutangaza vita dhidi ya mafisadi hao, na kusema atamshauri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aivunje halmashauri hiyo ili ianze upya.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Welle Ndikilo amesema ubadhilifu mkubwa wa fedha za miradi unaoonekana kukithiri ndani ya halmashauri hiyo ya Misungwi ni sawa na ugonjwa wa kansa, hivyo ni vema halmashauri hiyo ikavunjwa na wahusika wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Mbali na hayo, Ndikilo ameviagiza vyombo vyote vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Usalama wa Taifa, pamoja na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kuanza mara moja kuwashughulikia vigogo wa halmashauri hiyo, wanaotuhumiwa na ufisadi huo wa kutisha.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, Ndikilo ameyasema hayo jana wilayani Misungwi, wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo, katika ziara yake ya siku moja katika kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo.

Injinia Evarist Welle NdikiloInjinia Evarist Welle Ndikilo

Ndikilo alilazimika kuyasema hayo kufuatia kuwepo kwa ripoti za wakaguzi mbali mbali, akiwemo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye ripoti yake imebaini madudu mengi ya kuliwa kwa mamilioni ya fedha za miradi katika halmashauri hiyo.

“Tume tatu za ukaguzi ikiwemo ya Tamisemi na CAG ripoti zao zinasema ubadhilifu hapa Misungwi unatisha. Fedha nyingi za maendeleo mnakula tu, hamuwaonei huruma wananchi wetu?.

“Ripoti hizi zinasema sh. Milioni 336.7 za manunuzi zimeliwa maanamatumizi yake  hayakufuata utaratibu. Chanzo ni idara ya fedha, afya na wahusika wapo 12 na wametajwa kwa majina.

“Ripoti hizi zinasema sh. Milioni 242 zimeliwa na watumishi wetu hawa. Ripoti inataja chanzo ni idara ya fedha, afya. Kwa hali hii nitamshauri Waziri Mkuu tuanze upya hapa Misungwi”, alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, Ndikilo.

Kauli hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, imekuja siku chache baada ya vyombo kadhaa vya habari ikiwemo FikraPevu kuripoti tuhuma hizo za ubadhilifu wa fedha za maendeleo wilayani humo.

Ndikilo ambaye alikuwa akiwataja hadi majina ya watumishi wanaotuhumiwa kwa ufisadi huo kupitia ripoti za wakaguzi alizokuwa nazo kikaoni hapo, watumishi hao mafisadi watalaani na wananchi, na kwamba kwa sasa Misungwi nayoongozwa na Mkurugenzi wake, Exavieri Tilweselekwa ipo kwenye ICU na inasumbuliwa na ugonjwa hatari wa kansa.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa mkoa aliambatana na waandishi wa habari, Ofisa Usalama wa Taifa wa Mkoa wa Mwanza, Meja Mutashi, Katibu Tawala wa Mkoa, Doroth Mwanyika, Mkuu wa wilaya hiyo ya Misungwi, Mariam Seif Lugailla, Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo, Mkurugenzi wa halmashaurio hiyo Exaviery Tilweselekwa na wakuu wa idara mbali mbali wa halmashauri ya Misungwi.

Katika hotuba yake hiyo ya machungu, Ndikilo ambaye alitumia muda wa dakika 57 kurusha makombora kwa viongozi wa halmashauri hiyo alisema, zaidi ripoti za wakaguzi zinaonesha zaidi ya sh. Milioni 60.3  zimeliwa kupitia malipo yenye mashaka (malipo hewa), na kwamba watumishi 23 wamehusika.

Kana kwamba hiyo haitoshi, alisema zaidi ya sh. Milioni 56 za manunuzi hazijulikani zilipo kwani matumizi yake hayajaoneshwa kwenye taarifa, huku sh. Milioni 36 za DASIP nazo zimeliwa kwa njia ya udanganyifu na baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo ya Misungwi.

Katika hilo, alionesha wasiwasi na umakini wa baraza la madiwani wa Misungwi lililopo chini ya mwenyekiti wake, Benard Polcarp, na kusema: “Hivi Misungwi hakuna baraza la madiwani?.  Au baraza hili ni sehemu ya tatizo?”.

Alisisitiza kwamba, kufuatia hali hiyo mbaya, yeye na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, wataishauri Serikali Kuu kupitia kwa Waziri Mkuu na mwenye dhamana ya halmashauri kuwachukulia hatua kali vigogo hao, ikiwa ni pamoja na kuivunja ili halmashauri hiyo ianze upya na watumishi wenye damu mpya.

“Mimi na RAS tutaishauri Serikali ianze mara moja kuchukuwa hatua kali dhidi ya halmashauri hii ya Misungwi. Tunahitaji Misungwi tuanze na damu nyingine mpya, maana bila hivyo hatutaenda.

“Halmashauri nyingi tu huwa zinavunjwa zikionekana kuboronga. Hata hule Dar es Salaam iliwahi kuvunjwa kwa sababu kama hizi hizi. Hatutaki mambo haya na ninataka tutoke kwenye ICU na ugonjwa huu mbaya wa kansa”, alifoka Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, Ndikilo.

Akihitimisha hotuba yake hiyo kwa watumishi wa halmashauri ya Misungwi, RC Ndikilo aliagiza watumishi wote wanautuhumiwa kwa ufisadi huo kupeleka maelezo juu ya tuhuma hizo nzito za ubadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao hicho, walimtaka Mkuu huyo wa mkoa awafukuze kazi mara moja watumishi hao, na kwamba walimtaka aondoke na watuhumiwa hao na wala asiwahamishie halmashauri nyingine bali awafukuze kazi mara moja.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *