Mgomo wa Madaktari na udhaifu wa kutawaliwa “wapendavyo”

Jamii Africa

Kuna kanuni  ya msingi inagombaniwa katika mgomo huu wa madaktari ulioanza tena baada ya kusitishwa kwa muda wa wiki tatu. Kwamba je wananchi wa Tanzania watatawaliwa jinsi ili watawala wanataka au jinsi wanavyotaka wao kutawaliwa? Kwamba, serikali inaweza kufanya lolote na kutenda lolote bila kuulizwa, kuhojiwa na kupingwa na wananchi wake? Je, wananchi wanalazimika kukubali na kupiga magoti ya kuitikia pale “serikali” inaposema jambo  moja lifanyike hata kama jambo hilo linaonekana linapingana na maslahi ya wananchi hao? Ndugu zangu, tunachoshuhudia sasa hivi ni wananchi wa Tanzania wakisimama kudai watawaliwe ipasavyo!

Mgomo huu wa madaktari ni miongoni mwa migomu ya ajabu kabisa kutokea duniani! Toka mwanzo tulionesha kuwa ni mgomo ambao ungeweza kuepukika mapema sana kwa watawala kuonesha heshima, nidhamu na kujali madai ya madaktari badala ya kuyapuuzia na kuwakebehi madaktari kana kwamba Tanzania ni koloni la mafisadi! Madaktari walichohitaji kuona ni uongozi wenye kuonesha heshima, kujali, na kuyapa uzito madai ya madaktari lakini badala yake walichopewa ni dharau na kejeli na sasa wamepewa hadi ubabe!

Madaktari wetu wamegoma kama chaguo la mwisho!

Sote tunafahamu kuwa madaktari wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na vile vile tunafahamu kabisa kuwa hata katika mazingira haya magumu wanajitahidi sana kuhudumia wananchi na kuponya na kuokoa maisha ya watu wetu wengi huku wakati huo huo na wao wenyewe wakijijenga kimaisha wakati mwingine kwa kufanya vibarua vingine vitatu! Nilipoandika huko nyuma niliwahi kudokeza jinsi ya baadhi ya madaktari ambao waliamua kabisa kuachana na kazi ya kutibu na kwenda kwenye biashara zao wakitambua kuwa hata kama ni kujitolea nako kuna mipaka!

Kwa muda mrefu madaktari wamekuwa wakifanya kazi katika hali ngumu kweli – bila ya shaka siyo wao peke yao – lakini kwa namna ya pekee madaktari kazi yao inahusiana na uzima na kifo. Kwa muda huu mrefu wao madaktari na wauguzi wamejaribu kuishi na kufanya kazi katika mazingira haya bila kulalamika sana. Na tunafahamu jinsi gani tumepoteza madaktari wengi kwenda nje ya nchi kutafuta maisha bora zaidi na hawa wachache waliopo bado wanafanya kazi katika mojawapo ya uwiano mkubwa kabisa wa daktari na wagonjwa. Inakisiwa katika Tanzania daktari mmoja anahudumia watu 30,000-50,000 kutegemeana na mahali.

Inapofika madaktari kugoma ujue kuwa hali imekuwa ngumu sana na kwa kweli ni lazima tuoneshe shukrani ya pekee na heshima ya pekee kwao kwa kukubali na kufanya kazi katika mazingira magumu hivi na hata kukubali kurudi kazini Ikumbukwe kuwa mgomo huu ulianza mwanzoni kabisa kwa sababu ya watawala kupuuzia madai ya madaktari.

Kwa muda mrefu – kusema ukweli kuanzia 2006 – serikali imekuwa ikitoa ahadi ya “tunashughulikia” kila suala la maslahi na madai ya madaktari yalipokuwa yanatolewa. Hili si kwa madaktari tu limekuwa kweli hata kwa walimu na wafanyakazi wa kada nyingine. Baada ya kuvurugika kwa mgomo wa 2006 ambao mimi niliupinga kwa sababu moja kubwa – serikali mpya ndio ilikuwa imeingia madarakani – watawala wetu walifikiria kuwa sasa wamepata uhuru wa kutawala wapendavyo.

Na kweli kwa karibu miaka sita wametawala wapendavyo; bila mashinikizo bila kusukumwa. Kwa muda wote huo tumewaacha watawala na kuamua kufanya watakalo. Upinzani pekee ambao wameupata umetoka kwenye vyama vya siasa zaidi na siyo kwa wafanyakazi. Hili ndilo kosa kubwa zaidi la utawala wetu wa leo. Kwamba, wanafikiria upinzani pekee nchini ni wa kisiasa na ndio maana hata hivi sasa baadhi yao hawaamini kabisa kuwa mgomo huu umetokana na sababu zake zenyewe na unasukumwa na wahusika wenyewe na siyo wanasiasa.

Watawale wapendavyo au watutawale ipasavyo

Tatizo la mfumo wowote wa utawala wa kifisadi (a corrupt political regime) ni kuwa unafikia mahali unaamini kuwa unaweza kutawala upendavyo. Ndivyo ilivyokuwa kwa utawala lwa Hosni Mubarak, ndivyo ilivyokuwa kwa Bashir Al-Assad, ndivyo ilivyokuwa kwa Milosevic, ndivyo ilivyokuwa kwa kina Augustino Pinochet na watawala wengine wa mrengo wa kifisadi.

Msingi wa kutawala “wapendavyo” ni imani kuwa wao ndio walioumbwa na waliopendelewa na mbingu kutawala milele na kuwa hakuna mtu mwenye haki wala sababu ya kuwapinga, kuwahoji, au kuwakatalia. Katika utawala wa namna hiyo watawala  wanataka watumie fedha za umma wapendavyo bila kuulizwa, walindane bila kugombezwa na wakandamize wanyonge bila kukatazwa!

Kimsini utawala wa kifisadi kama ulivyo utawala wa kiimla hujenga ndani yake mbegu za maamgamizi yake. Tunachoshuhudia sasa hivi nchini ni kuanza kuchipuka kwa mbegu hiyo kwani kwa miaka kadhaa sasa ufisadi umepandwa, umemwagiliwa maji, umekua na kuzaa matunda. Sasa wamekuja watu wanataka kuukata na hapa patakuwa pachungu. Patakuwa pachungu kwa sababu wapo wanaonufaika na utawala wa kifisadi. Wapo wanaokula na kusaza matunda ya ufisadi. Maslahi ya hawa ni kuona kuwa utawala uliopo unaacha “upumue”.

Wakati wowote linatokea kundi linalotoa changamoto kwa utawala uliopo na kuufanya utawala huo uonekane katika udhaifu wake watetezi watajitokeza. Watajitokeza kujaribu kutumia kila mbinu kuonesha kuwa utawala uliopo umefanya yote mazuri na unahitaji “muda kidogo” ili “kushughulikia” matatizo yanayolalamikiwa. Naam! Watetezi hawa wataita watu majina, wataanzisha ugomvi na watafanya hivyo wengine wakiamini kuwa wakitetea vizuri zaidi labda na wao watakuja kusogezwa karibu zaidi katika meza ya ufisadi – kama watakaa kwenye viti au pembeni wao haiwajalishi sana!

Madaktari wetu wameonesha kile ambacho kilikuwa kinakuja nacho ni kukataa kutawaliwa wapendavyo watawala. Unajua watawala hawapendi kubughudhiwa kabisa wanapotawala wapendavyo. Hawataki kuulizwa wala kukosolewa na wanapokoselewa wanaweka masharti ya jinsi gani wakosolewe na kuulizwa! Hawataki kuoneshwa mapungufu na udhaifu wao na wakioneshwa huja juu na kudai – tena kwa haraka sana – “kwani mazuri yetu hamuyaoni!?”

Madaktari wamekataa kuona nchi inatawaliwa wapendavyo watawala. Tukumbuke mojawapo ya vitu vilivyotuudhi wengi ni kuwa wakati serikali inasema haina fedha za kuwalipa madaktari maslahi bora wabunge waliamua kujiongezea posho nono ati kwa sababu “maisha ni magumu kule Dodoma”. Hili lilikuwa tusi na limebakia kuwa tusi kwani inaonekana baadhi yao hadi hivi sasa hawaoni kabisa tatizo la wao kudai zaidi huku serikali yao ikiwanyima wengine kile wanachodai zaidi! Hawa watawala wanaona kama wameonewa na wengine kuona kuwa yeyote anayewapinga hawatakii mema!

Mgomo huu unahusu kanuni kubwa zaidi

Ndugu zangu, mgomo huu unahusiana na kanuni kubwa zaidi. Na hakuna kosa kubwa ambalo serikali itafanya kama kuamua kuleta madaktari wa kigeni ili kuwaonesha madaktari wetu kuwa hawana thamani. Naamini hili litakuwa ni tusi la mwisho na msumari wa mwisho kusababisha mgomo mkubwa wafanyakazi nchini! Mgomo huu haukupaswa kabisa kufika hapa; Kikwete ameamua kupuuzia na akiliachilia hili mikononi mwa Waziri Mkuu mtu ambaye hajaunda baraza la mawaziri wala hana uwezo wa kuliwajibisha.

Yote haya yamefika kwa sababu Kikwete haamini kuwa alipaswa –mara moja – kuwafukuza kazi watendaji wote wakuu wanne wa wizara hiyo; kwanza kwa sababu ya kuhusika kwao kwa kusababisha mgomo na pili kutokana na kashfa mbalimbali ambazo zimetokea kwenye wizara hiyo. Madaktari wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kuhusu matatizo hayo; kuna barua nyingi tu kwenda kwa Katibu Mkuu kiongozi, na Ikulu ambazo zimeanisha migongano kati ya viongozi hao wakuu. Lakini Kikwete kwa kuogopa kuonekana serikali yake ina matatizo ameendelea kuwakumbatia viongozi hawa wabovu na walioshindwa.

Matokeo yake ni mgomo huu ambao kwa kweli kabisa unastahili kuungwa mkono na Watanzania. Watawala inawapasa kutambua kuwa hawawezi kuendelea kutawala wapendavyo. Haiwezekani polisi waendelee kuua wananchi bila kujali (with impunity) halafu wananchi wakija kucharuka siku moja serikali ione inaonewa! Kuna mistari haipaswi kuvukwa na kwenye hili la madaktari na mawaziri kuna mstari umevukwa mstari ambao hauwezi kurudishwa isipokuwa kwa kujiuzulu au kufukuzwa kazi kwa uongozi wa juu wa wizara hiyo pamoja na kufanyia mabadiliko makubwa ya kimuundo.

Katika sakata hili madaktari wamechukua uamuzi mgumu zaidi kuliko maamuzi ya sekta nyingine yoyote ya kutaka viongozi wazembe wawajibishwe ili kwamba kiongozi atakayeshika uongozi katika wizara hiyo ajue kabisa kuwa siyo wizara ya kuchezea, siyo wizara ya kuzemba na siyo wizara ya kuongozwa kwa ubabe, kejeli, dharau na uzandiki. Wanaweza kuchezea sehemu nyingine lakini linapokuja suala la afya za wananchi wetu hakuna wa kuonewa huruma.

Ni matumaini yangu kuwa serikali itaamua mara moja kuwaachisha kazi watu hawa wanne ili kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania na kurudisha heshima katika fani za tiba nchini na hatimaye kuanza kwa mabadiliko (reform) ya sekta hiyo ili hatimaye kuboresha afya nchini.

Endapo mgomo huu utaendelea hata kwa siku moja zaidi mwenye kosa siyo Waziri Mkuu Pinda – kwani hajaunda baraza la mawaziri na hana uwezo wa kumfukuza waziri yeyote – bali itakuwa ni Rais mwenyewe ambaye ndiye amewawekea kinga viongozi hawa. Endapo mgomo huu utaendelea kwa siku nyingi ya ziada na kusababisha madhara zaidi wananchi wanayo haki kabisa ya kuanza kuandamana kutaka Rais mwenyewe awajibike – hata kujiuzulu – kwa sababu kama hadi hivi sasa hajaona uzito wa tukio haiwezekani kumfanya aone huko mbeleni.

Watanzania wanastahili kutawaliwa ipasavyo na siyo kutawaliwa wapendavyo watawala. Hili ndilo kiini hasa cha mgomo wa madaktari. Ni kujitambua sisi kama watawaliwa tunataka tutawaliwe vipi. Je watu wawili wanaweza kubebwa na kuonewa huruma kuliko watu elfu? Je, kuhofia kutengeneza mazoea ya wananchi kushinikiza serikali kunatosha kufanya watawala wahofie kuamua sasa? Madaktari wamesema tunastahili kutawaliwa ipasavyo kwa gharama yoyote ile. Hili ni somo gumu sana kulifuzu.

16 Comments
  • Ni ajabu kuona kiongozi mkuu wa nchi anaendelea kuzurula bila kuonyesha uongozi unaostahili kuepusha mauaji ya raia wasio na hatia. Naiota siku ile ambapo waziri mkuu Mizengo Pina ataambatana na Jakaya Kikwete kujibu mashitaka ya watanzania wanaokufa kutokana na kibuli chao katika kushughulikia mgomo huu.

  • Udhaifu wa serikali zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya mwalimu kung’atuka yameleta matatizo makubwa katika nchi hii na ni sahihi kabisa kwa wananchi kudai uwajibikaji na maboresho ya huduma muhimu za jamii maana hizi ndio msingi mkuu wa mkataba wa kijamii baina ya wananchi na watawala.

    Katika sakata hili la madaktari, sikubaliani na uamuzi wa wafanyakazi hawa wasekta ya afya kuweka roho za watanzania rehani kwa sababu ya madai ambayo walishajadiliana na serikali na serikali hii hii kuahidi kuyapatia ufumbuzi. Masuala mengi yanahitaji bajeti na kwa mwenendo wa mfumo wa uendeshai wa serikali, ukweli ni kwamba hakuna ziada katika bajeti ya mwaka huu inatakayowezesha utekelezaji wa matakwa ya madaktari mara moja. Hapa inahitajika programu ya muda mrefu, angalau miaka kumi kwa sababu hauwezi kubadilisha madudu ya miaka hamsini ndani ya muda mfupi.

    Mgomo huu una maslahi gani kwa wananchi? Je sisi ndio tumekuwa “collateral damage”? Mbona sisi hatushtaki pindi uzembe wa wahudumu wa afya unapotupotezea ndugu zetu au kutupa vilema? Je weledi wa wahudumu hawa unakuwepo wapi hapo au bado ni suala la serikali katika kila tukio la uzembe wa wahudumu hawa?

    Njia pekee ya kumaliza msuguano huu baina ya wahudumu wa afya na serikali ni kwa njia ya mwafaka. Katika mwafaka kila upande ni lazima ukubali kupunguza madai yake na katika hili suala, wahudumu hawa wa afya wasitake kutuua sisi wananchi kwa madai ambayo yanaingilia upangaji kazi wa rais ambayo ni medani ya siasa.

    Serikali nayo ni bora ikahikikisha madai ya msingi yenye maudhui ya taaluma ya uuguzi yanashughulikiwa kwa haraka tena ndani ya muda (within a mutually agreed time frame)

    • Serikali lazima iwajibike,hakuna kulemba hapo,kwani mnataka madactari wanyamaze halafu kiwe nini.

      Kwani madai ya uzembe wa mawaziri hauathiri madaktari tu hata ww mwananchi ktk angle ya huduma na vifaa haya wakiacha halafu hakuna vitendea kazi utakuwa ume-solve nini?

      Wananchi acheni kukurupuka kuona madaktari wana yao. Mi naunga mkono kwa sababu wananchi hatupati tiba mbadala kwasababu hakuna vitendea kazi navyo vinahtaji muda gani? Mbona mbunge akifa faster uchaguzi hata katikati ya bajeti what does it imply?

      Ndugu zangu amkeni

    • pamoja na mgomo una athiri maisha ya wananchi lakini wakatimwingine unakua mzuri ilikuokoa maisha ya wengi.

      hi wizara imekua na mambo yaajabuajabu sana na hakuna anae jali.
      fikiria zile dawa feki za maleri zilizoingizwa nchini ni wananchi wangapi wameathirika nazo

      na vile vifaa feki vyakupimia damu vilivyo ingizwa nchini na kusambazwa mikoani na hakuna mtu alie wajibika

      kwakutoa tathimini ni wananchi wengi sana wameathirika na mambo yaajabu kwenye hii wizara tofauti na hata watako athirika na huumgomo

      wakina mama wangapi wanashindwa kujifungua kisa hospitali hazina vifaa lakini waziri anatetea posho ya mbunge akisinzia bungeni

      hatanchi inapopigani vita kuna wanao umia lakini lengo kikulinda nchi na walio wengi so naunga mkono huumgomo ili watu wejue na watimize wajibu wao

      • Kwa kuongezea tu; ni wangapi wanaathirika kwa kuagiza mashine feki za kupima maambukizi ya virusi? Ukosefu wa madawa hosipitali za serikali? kupunguza bajeti za afya na kuongeza zile za kwenda kutibiwa nje ? haya nayo kwani ni mgomo wa madaktari jamani? Mgomo wa madaktari ulikuwa unadai haya yarekebishwe. Wasaidieni madaktari tupambane na haya!!

  • Serikali ingefikiria sana juu ya jambo hili kwani mvutano na madaktari mwathirika ni mgonjwa ambaye maskini hana jinsi zaidi ya kulazimika kufa. Nadhani watumishi wawili wa kisiasa wasileta dhahama kwa watanzania walio wengi, Hebu Waziri Mponda na naibu wako jiuzuluni tafadhali ili kuepusha vifo vya watanzania

    • Tatizo kubwa ni kwa sababu hata sisi tunaoathirika ” yaani hao maskini” tunadanganyika na tunasimama upande wa hao viongozi ndio maana hata siku moja hawatakaa wawajibike hata kama tunakufa; Tungesimama kidete upande wa madaktari tungewalazimisha waondoke na hii migomo isingetokea. Wakati sisi tukifa wao wanekwenda zao Indiaaa hata kama hawaumwi; wengine wanakwenda Ulayaaa kujifungua pesa zote hizo si zingeboresha hospitali zetuu????

  • Hili ni tatizo la kuingiza mdudu siasa kwenye mambo ya kiutendaji. Kauli za watu ambao ni professinal kuonekana wanachochewa na wanaharakati bado linakuwa dharau na kejeli kwao. wao ni wasomi na wanaelewa madai yao ya msingi ni yapi. Bora serikali ingeweka hizo inferiority pembeni na kushughulikia suala la wizara hiyo kama jambo la dharura.

  • TATIZO SIKU ZOTE HUWA NI TATIZO TUU SO TUSIKUBALI TATIZO LIWE KUBWA KUPITA TATIZO LENYEWE LA MSINGI HEBU TUANGALIE WAPI NA SEHEMU GANI YA MSINGI YA KUSHUHULIKIA TATIZO HILI LA MSINGI.

    TUKIANZA KUCHANGANYA TATIZO LA MSINGI NA MAMBO MENGINE AMBAYO SI YA MSINGI TUTAZIDI KULIKUZA TATIZO LA MSINGI KUWA TATIZO KUBWA NA HIYO KUTUPA UGUMU KULITATUA TATIZO LA MSINGI. SWALA LA MADAKTARI NI YA MSINGI PIA SERIKALI NAYO INGETAKIWA ITOWE MAELEZO AMBAYO NI YA MSINGI ILI KUTATUA TATIZO LA MSINGI. SIO BLALA BLAA KILA UPANDE KUONYESHANA UBABE WAKATI WANANCHI WANAUMIA. USHAHIDI WA KIHISTORIA UNAONYESHA KUWA UBABE HAUKUWA KUSHINDA POPOTE DUNIANI.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA

  • Naamini tz hatuna uongzi ila picha za uongozi kwani kama ni kweli tungekuwa na uongozi haya yote yasingetokea.
    Heshima kwa viong zi Mkapa Na Nyerere

    AM PATRIOTIC

  • Haya ni matokeo ya serikali inayowekwa madarakani na kikundi cha wanamtandao. Daima serikali ya namna hiyo huwajibika kwa wanamtandao na sio kwa wananchi.

  • Madaktari si wehu itokee tu from no where wagome, kipo kiini na kiini hicho waziri na naibu wake wanakijua, kinachosumbua hapa ni ile spirit ya watanzania kutokubari kuwajibika!

    Jamani hebu kwanza JK kama ana mapenzi na watanzania alinganishe uhai wa watanzania watakaopoteza maisha yao kutokana na sinema hii aliyoact yeye na waziri na naibu wa afya italinganishwa na huo urafiki?

    Inaumiza sana JK kushindwa kujari wananchi wa hali ya chini vile yeye na ukoo wake wote mafua wanaenda kuchekiwa ulaya kwa pesa yetu…..!Chonde chonde JK vaa sura ya Magufuri acha kucheka na rafiki zako la sivyo utatolewa kama Gadaffi……

  • hivi hii nchi tunaelekea wapi? ni swali ninalojiuliza na mwisho wa siku nakosa jibu sahihi ‘cos kwa nchi yenye viongozi makini na wanaowajali wananchi waliowaweka madarakani hawawezi kusubiri hadi dazeni ya wapiga kura wao wafe ndiyo washtuke, hivi bila hawa wananchi wanaokufa kwa kukosa tiba kwa ajili ya mgomo wa madaktari mtamuongoza nani? Hongereni madaktari kwa kutetea haki zenu pia na za walalahoi bila uoga, umoja ni nguvu “Komaeni” Mh. rais vaa sura ya kazi acha kucheka na viongozi wazembe na wasiokuwa na moyo wa kizalendo na huruma kwa Watanzania.

    Madaktari si wendawazimu kiasi cha kuamua kuzua mgomo bila sababu za msingi vile vile sipendi na wala siamini kuwa wao ni mbumbumbu wanaoweza kushawishiwa kuanzisha mgomo kwa maslahi ya chama, mtu au kundi fulani. Waswahili husema “Mficha ugonjwa kicho humuumbua”. Mh JK mtimue waziri na naibu wake upange safu upya ili kunusuru wananchi na hasa wa hali ya chini (maskini).

    MUNGU IBARIKI TANZANIA!

    • Ni wakati muafaka pia wanajamii tuwaelimishe wananchi including wagojwa wetu kuwa huu mgomo haukuwa kwa maslahi ya madaktari tu, bali kwa maslahi yao; kama mtakumbuka madaktari wanadai wagonjwa wasilale chini; bajeti ya kupeleka waheshimiwa India Ipunguzwe fedha hizo ziboreshe hospitali zetu. Wakubwa hawa wanlipiwa mabilioni huko kwenye hospitali za Private “Aga Khani na Regency; Zikilipwa Muhimbili Itaboreka na kunufaisha Wengi!!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *