Tunduma tete, Zambia yakamata Watanzania

Jamii Africa

tunduma-chatHALI ya usalama katika mpaka wa Tunduma uliopo wilayani Mbozi mkoani Mbeya kati ya Tanzania na Zambia si salama baada ya wananchi hususani vijana kutaka kuanza msako wa kuwakamata raia wa Zambia baada ya Watanzania saba kukamatwa na kufikishwa mahakamani nchini Zambia kwa kushukiwa kufanyabiashara ya kuuza fedha pasipo vibali.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Watanzania hao kukamatwa Februari 4 mwaka huu na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Nakonde nchini Zambia Februari 7 mwaka huu na kusomewa shitaka la kufanya biashara ya kuuza fedha pasipo kuwa na vibali kisha kunyimwa dhamana.

Wakizungumza na Fikra Pevu katika mpaka wa Tunduma wananchi hao walisema kuwa endapo Serikali ya Tanzania itashindwa kuingilia kati sakata hilo ili watanzania hao wapewe dhamana watachukua maamuzi magumu kwani historia inaonesha kuwa watanzania wanapokamatwa nchini Zambia wanateswa na kuuawa.

‘’Tunaiomba Serikali yetu na mamlaka zinazohusika kuingilia kati suala hili maana wenzetu wamethibitisha kuwa kule mahabausu wanateswa na historia inaonesha kuwa mara nyingi wazambia wanawaua watanzania wanapowakamata hivyo hatutaki hayo yatokee kama yalivyotokea huko nyuma tunaomba wenzetu warudishwe katika rumande ya Nakonde na wapewe dhamana kuliko walikowapeleka Gereza la Isoka’’ alisema Ramadhani Iddi.

John Kandonga mkazi wa wilaya ya Rungwe ambaye ni mzazi wa mmoja wa washukiwa hao waliokamatwa alisema kuwa kutokana na shitaka hilo ambalo halihusiani na wizi ni dhahili kuwa ujirani mwema wan chi hizi mbili upo kinadharia zaidi kwasababu suala hilo linazungumzika.

kikwete and banda greeting
Tanzanian President Jakaya Kikwete (L) is congratulated by his Zambian counterpart Rupiah Banda after he was sworn-in at the Uhuru Stadium in Dar es Salaam, November 6, 2010

‘’Nina masikitiko sana maana sijaweza kukutana hata na wanangu hawa ambapo siyo wezi na sasa dhamana wamekataliwa na ninasikia wanateswa sana sijua kama wapo hai na kitendo hiki kinatoa picha ya kwamba ujirani tulionao na wenzetu hauajawa sawa labda kama kuna mashinikizo ya wakubwa wenzetu kutoka hapa Tanzania’’ alisema Mzazi huyo.

Wakielezea zaidi undani wa tukio hilo, wananchi hao akiwemo Sadick Josiah, Jailo Maena na kijana Ofin Minga ambaye aliteuliwa na Mkuu wa kituo cha Polisi cha mjini Tunduma kuwawakilisha wenzake katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Tanzania na Zambia kilichofanyika katika kituo cha polisi cha Zambia, alisema kuwa muhafaka haukuweza kufikiwa kutokana na Mkuu wa kituo cha Tunduma (OCS) kuwakandamiza zaidi watanzania waliokamatwa.

‘’Mimi niliteuliwa kuwawakilisha mamia ya watanzania wenzangu ambao tulifika katika mahakama kusikiliza mashitaka na baada ya kuona wenzetu wamenyimwa dhamana tulijikusanya na kutaka kuja Tanzania ili kukutana na Afisa usalama wa Taifa lakini OCS alisema tufanye kwanza mazungumzo kulekule Zambia ajabu akashindwa kuleta suluhu badala ya kuwakandamiza watanzania wenzetu’’ alisema Minga.

Alisema baada ya kutopata suluhu katika kikao hicho ndipo watanzania walipotaka kuandamana ili kushinikiza wenzao kupewa dhamana lakini Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani Joseph Mwachembe aliwasihi wasifanye hivyo ili jambo hilo liwekwe kwenye utaratibu wa mazungumzo ndipo watanzania hao wakatulia.

Mwandishi wa habari hii alimtafuta Mwachembe ambaye alikiri kuwepo kwa jazba za watanzania na kusema kuwa mpaka sasa anashangazwa kuona uongozi wa jeshi la polisi Tunduma kutoweza kutoa msaada wowote wakati kuna mahusiano mazuri kati ya jeshi hilo pande zote mbili na hivi karibuni walifanya doria ya pamoja nchini Tanzania kinyume cha sheria.

‘’Mpaka sasa wananchi  wanataka kuandamana na baadhi kuwakamata wazambia walioko huku lakini ninaendelea kuwasihi wasifanye hivyo naamni Serikali kupitia nyie vyombo vya habari litatatua hali hii kabla halijafika mahala pabaya lakini Serikali liliangalie jeshi la Polisi mjini hapa’’ alisema Mwachembe.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Tunduma Frank Mwakajoka alisema kuwa hali hiyo imeleta masikitiko makubwa kwa wananchi wa Tunduma kwasababu biashara hiyo ipo muda mrefu katika mipaka ya nchi hizo na hofu yake kubwa ni kwamba endapo watanzania hao watakapo dhurika hali inaweza kuwa mbaya katika mpaka huo.

‘’Mimi nilipopata tarifa hizo nikawasiliana na viongozi wenzangu wa Serikali akiwemo OCS (Mkuu wa kituo cha Polisi) cha Tunduma ambaye alinipa maelezo ya awali ambayo hayaleti suluhu, wananchi wanachokitaka ni kwamba wenzao wapewe dhamana kisha kesi iendelee maana historia inajieleza kuwa Watanzania wanapokuwa wamekamatwa upande wa wenzetu huteswa na kuuawa’’ alisema Mwakajoka.

Fikra Pevu iliwatafuta baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama wa wilaya ya Mbozi ambao walithibitisha kuwa watanzania hao waliokamatwa wanateswa na maabusu wenzao.

‘’Ni kweli suala la kuteswa tumelithibitisha kwasababa baada ya kupata taarifa hizo za kuteswa kwao baadhi ya wajumbe wenzetu tuliwatuma kwenda kuzungumza nao na waliwaeleza kuwa wanateswa sana na maabusu wenzao na siyo kuwa wanateswa na askari wa Zambia ’’ walisema wajumbe hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe.

Waliokamatwa ni Yohana Mwalisu (40), Sadick Loti, Daniel John , Oscar Leonard, Albert Amanyisye, Ephrahim Mjwanga na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Samora ambao wote wamepelekwa katika gereza la Isoka umbali wa kilomita zaidi ya 120 kutoka mjini Tunduma.

Habari hii imeandikwa na Gordon Kalulunga, Tunduma

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *