WASTANI wa wajawazito 200 wanajifungua kila mwezi, katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda (BDDH) pamoja na kuzikosa huduma wanazostahili kupata bure.
Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, makundi maalum wakiwemo wazee wasiojiweza, walemavu, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito, yanatakiwa kupata huduma bure.
hospitali teule ya wilaya ya Bunda inavyoonekana kwa mbele
Utawala wa hospitali hiyo mshirika wa serikali umesema, ukosefu wa fedha za kununua dawa, vifaa tiba na uchache wa watoa huduma wenye ujuzi unapunguza ufanisi wa utoaji huduma.
Akizungumza na wanahabari hivi karibuni, Kaimu Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Revocatus Kato alisema huduma bure kwa wajawazito na makundi mengine maalumu zilianza kutolewa mwaka 2005/2006.
Kato aliilaumu serikali kwa kuchelewesha fedha za Matumizi Mengineyo (OC) na zile za Mfuko wa Pamoja (Busket Fund) ambazo ni muhimu kwa ununuzi wa dawa na vifaatiba.
“Kuna upungufu wa vifaatiba mapokezi, chumba cha upasuaji na X ray, na maabara, vifaa hivyo hununuliwa na msambazaji mkuu Bohari ya Dawa Tanzania,” alisema.
Alisema pamoja na umuhimu wake mkubwa, mifuko ya damu, mipira ya mikononi (gloves), mirija ya maji (drips), na uzi za kushonea waliopasuliwa ni kawaida kukosekana katika hospitali hiyo.
Alisema hali hiyo hutoboa zaidi mifuko ya wajawazito ambao hulazimika kutumia Sh 2,500 kununua mifuko ya damu, Sh 2,000 mirija ya maji na Sh 5,000 hadi 8,000 kwa ajili ya uzi wa kushonea.
Asopharet Majanjara ambaye ni muuguzi wa wodi ya wazazi hospitalini hapo, alisema walanazimika kutumia mpira mmoja kufanya kazi tatu tofauti wakati wa kumzalisha mjamzito kwasababu ya kukosekana kwa mipira hiyo.
Akizungumza na wanahabari Desemba mwaka jana, Mganga Kiongozi wa hospitali hiyo, Dk William Karekamoo alitoa taarifa ya hospitali hiyo kusimamisha kwa muda usiojulikana utoaji huduma bure kwa makundi maalumu.
Alisema makundi hayo ambayo Serikali imeahidi katika Sera ya Afya kuwa yatapata huduma ya afya bure, yataanza kujinunulia vifaatiba, dawa na kulipia gharama nyinginezo za matibabu kama wanavyofanya wengine.
Dk Karemakoo alisema wamechukua uamuzi huo baada ya serikali kuchelewa kutoa ruzuku za uendeshaji kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kuifanya ishindwe kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji.
Alisema kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2011/2012 hospitali hiyo ilipokea Sh Milioni 2 tu kati ya Sh Milioni 28 kama ruzuku ya uendeshaji na mpaka wakati huo (Desemba mwaka jana) ilikuwa haijapokea Sh milioni 34 kutoka Mfuko wa Pamoja.
Alisema mbali na kuathiri huduma ya bure kwa makundi hayo, ukosefu wa fedha pia umeathiri huduma nyinginezo hospitalini hapo zikiwamo za usafi wa mazingira, maji na chumba cha kuhifadhia maiti.
Dk Karemakoo alisema jokofu la chumba hicho liliharibika na kushindwa kutengenezwa kwa muda mrefu pamoja na huduma yake kutegemewa na wakazi wengi wa wilaya hiyo na mikoa ya Mara na Simuyu.
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Rainer Kapinga alikiri hospitali hiyo kuchelewa kupata fedha kutoka serikalini kwa wakati, hata hivyo akaukosoa utawala wake kwamba hauna vipaumbele kutokana na makusanyo wanayofanya na ndio maana huduma zake zinalegalega.