Wachimbaji wadogo wakiwa katika umoja, wanaweza kumaliza changamoto mbalimbali zinazowakabili kama ukosefu wa mitaji, teknolojia na soko la kuuza wanachokizalisha.
Mjumbe wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Haki Madini na mchimbaji wa madini ya tanzanite, Lawrence Gunewe anasema changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo ni mitaji na teknologia.
Gunewe ameongeza kama wataungana itasaidia hata kukopa mitaji katika benki mbalimbali hapa nchini kwa kuwa watakuwa wanatambulika sio kama ilivyo sasa.
Wazo la kuungana lilishazungumziwa miongoni mwa wachimbaji lakini wengine walisema wamewekeza sana na wengine hawajafikia kiwango hicho, basi mpaka leo bado muungano haujafanyika.
Akitolea mfano wa teknolojia na uwezo wa kila kitu, Gunewe amesema kampuni ya Tanzanite One ina kila kitu, mashine za uchimbaji, ina wataalamu kwenye kila kitengo, magari makubwa ya kubebea udongo, wana eneo la kuchekechea udongo (plant) ambapo katika migodi yetu hatuna.
Ameongeza utakuta mchimbaji mdogo kama ana vifaa ama mashine basi ni vichache ,udongo tunabeba kwa viloba, kwa ujumla wake bado tunahitaji mitaji.
Mmiliki wa mgodi kitalu B na D, Stela Shayo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wanawake wachimba tanzanite Mererani, alisema wameamua kujiunga ili waweze kupata mitaji kwa kukopeshwa katika benki na hata serikalini.
Ameongeza kuungana kwao kutawawezesha kuunganisha nguvu ya kipato na kiutendaji kwa kuwa wanampango wa kununua mashine ya kuthaminisha madini ya tanzanite, na kutengeneza vitu mbalimbali kama hereni, shanga, mikufu na kuviuza ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa TANSORT (kitengo kinachoshughulisha na kuthamini na kuuza madini ya vito) wizara ya Nishati na Madini Archard Kalugendo amesema ni vyema wanawake wakajiunga katika vikundi na serikali itawawezesha kupata mitaji, vifaa ambavyo kwa mtu mmoja mmoja haiwezekani kwa sababu ya gharama na ugumu wa kuwapata.
Kalugendo alisema waziri wa nishati na madini Prof. Sospeter Muwongo amesisitiza wachimbaji wadogo wajiunge katika vikundi kwani ndani ya bajeti ya wizara yake ya 2012, ameweka mfuko maalumu wenye kiasi cha shilingi bilioni 8 ili kuwawezesha.