Biashara ya ‘’viungo vya binadamu’’ imeibainika kuwepo wilayani Bunda mkoani Mara. Damu unit moja inauzwa kati ya Sh.15,000 mpaka 20,000 kisha kuwaongezea wagonjwa wenye upungufu wa damu hususani watoto na wajawazito.
Biashara hiyo imebainika hivi karibuni na kushika kasi katika kata ya Nyamuswa tarafa ya Ikizu wilayani Bunda mkoani Mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wateja wa damu hiyo ambao ni wagonjwa wanaoitibiwa katika kituo cha afya cha Ikizu, wanasema kuwa biashara hiyo ina mikono ya madaktari na wauguzi wa kituo hicho.
Wanasema mgonjwa anayeenda katika kituo hicho na kugundulika kuwa ana upungufu wa damu hasa watoto na wajawazito huambiwa kuwa watoe damu au wanawaitia vijana ambao wanakuwa nje ya uzio wa hositali hiyo na kufanya makubaliano na ndugu wa wagonjwa.
‘’Wakiwaita vijana hao ili kutoa damu, wanataka kupewa Sh. 20,000 na mkiwabembeleza wanashusha mpaka Sh. 15,000’’ anasema mgonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Anjela Hamis.
Mganga mkuu kiongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu Dr.Abahehe Kanora anasema malalamiko hayo si ya kweli bali uongozi wa kituo ulikubaliana na kamati ya afya ya eneo hilo kuwa kutokana na uhaba wa vitendanishi ikiwemo vifaa na dawa za kupimia damu kila anayeongezewa damu anachangia Sh. 2000.
‘’Malalamiko hayo si kweli bali kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wagonjwa na ndugu zao wanaohitaji damu wakiambiwa kuwa hatuna damu ndipo wanalazimika kuwatafuta watu nje ya kituo na kuja nao ili kuwatolea damu hao labda ndiyo wanaowauzia lakini sisi hapa anayechangia damu na anayeongezewa kila mmoja hutozwa Sh. 2,000’’ alisema Dr. Kanora.
Anafafanua kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuchangia gharama ya vifaa na dawa za kupimia group za damu zao na kwa siku moja kituo hicho cha afya kinatumia unit 10 za damu na nyingi hutumika kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Anapoulizwa kuwa kama anajua kuwa hata kuchangisha fedha kwa wagonjwa hao na wanaochangia damu ni kosa kutokana na sera ya afya ya mwaka 2007 katika kipengele cha damu salama,anasema kuwa analijua hilo lakini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na damu yenyewe kutoka katika benki ya damu salama ya kanda iliyopo Bugando mkoani Mwanza ndiyo maana wanalazimika kufanya hivyo.
‘’Unajua tunalazimika kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya watu maana upatikanaji wa damu ni mgumu sana na hata tukisema kuwa watu wachangie damu wachache wanaojitokeza na mkipeleka mkoani ili kupeleka Mwanza tutapoteza masisha ya watu wengi sana’’ anasema Dr. Kanora.
Anasema kutokana na ukosefu wa damu salama katika kituo hicho cha afya watoto wengi hupoteza maisha baada ya kuumwa kwa muda mrefu ugonjwa wa Malaria huku wakicheleweshwa kufikishwa hospitalini na wengi wao wanatoka Serengeti.
Kabla ya kukutana na Dr. Kanora nilikutana na Dr. Safari Matundwe ambaye alikuwepo hospitalini hapo lakini hakuweza kutoa msaada wowote kwa mjamzito Furaha Nyateli mkazi wa Saramakati aliyekuwa akihitaji msaada wa kujifungua ndani ya wodi ya wajawazito.
Akizungumza kwa uchungu na kusema hali hiyo ndivyo ilivyo katika kituo hicho, binti aliyeongozana na mjamzito huyo Doi Hamis, alisema kuwa chupa ya uzazi ya mwenzake ilikuwa imepasuka tangu saa nne asubuhi lakini hakupewa msaada wowote licha ya kulazwa mpaka majira ya saa tisa na dakika ishirini na nne baada ya waandishi kufika na kujionea hali ya mjamzito huyo na kuamua kuhoji kulikoni.
Akielezea hali hiyo, Dr. Safari alisema kuwa hali hiyo inatokana na uchache wa watumishi hasa wakunga ambpo siku hiyo alikuwepo muuguzi mmoja tu ambaye alikuwa akihudumia wagonjwa wa aina zote katika wodi Nne zilizopo katika kituo hicho cha afya.
Muuguzi mkuu wa hospitali ya wilaya ya Bunda Adelaida Masige anasema kuwa katika wilaya hiyo kumekuwa na tatizo kubwa la damu salama ingawa mwanzo walikuwa wakijitolea zaidi wafungwa na wanafunzi.
‘’Damu salama ni tatizo kubwa kinachofanyika wagonjwa wanaotaka kuongezewa damu wanakuja na ndugu zao tukiwachukua damu tunapima VVU na magonjwa ya zinaa lakini hakuna utafiti uliofanyika kujua kama walioongezewa damu wameambukizwa au la’’ anasema Adelaida.
Kaimu muuguzi mkuu wa hospitali teule ya wilaya ya Bunda maarufu kwa jina la DDH Revocatus Kato, anasema kuwa kwa upande wa hospitali hiyo damu ni tatizo kubwa na wagonjwa wanaofika hapo wanalazimika kuchangia gharama za mifuko ya kuwekea damu.
‘’Tunawataka wagonjwa au ndugu zao kutoa Sh. 2500 kwa ajili ya kununulia mifuko ya kukusanyia damu, mirija ya drip ya kumwingizia mgonjwa Sh. 2000 na kama atakuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji anatoa pesa ya nyuzi Sh. 5000 na kumshona ni Sh.8,000/=’’ anasema kaimu muuguzi huyo Kato.
Lakini mjamzito Agness Baraka mkazi wa kijiji cha Kambubu kata ya Nyamang’uta anasema kuwa aliwahi kukimbizwa katika hospitali hiyo teule (DDH) akiwa mjamzito ambapo alilipa Sh.16,000 kwa ajili ya nyuzi za kumshonea tu baada ya kufanyiwa upasuaji mbali na gharama za damu.
Diwani ya kata ya Nyamang’uta Kalemba Jonathan Ilubi, anasema kuwa ni kweli kuna ongezeko kubwa la vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutokana na kupungukiwa damu na kucheleweshwa kupelekwa hospitali lakini wananchi wengi wanadai kuwa wanaogopa kuwapeleka hospitali watoto wao ili kukwepa (kauli mbaya) kutukanwa na wahudumu wa vituo vya afya.
Kwa upande wake mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani humo Daines Limo anasema kuwa sababu nyingine inayochangia kupungua kwa damu kwa wajawazito ni kutokana na kukosa lishe ya kutosha.
‘’Lishe kwa sasa katika wilaya hii hasa kwa wajawazito ni tatizo ambapo hata samaki hawapatikani kwa wingi kama zamani minofu yake inapelekwa viwandani na wanawake wakila samaki minofu inaongeza madini chuma na damu mwilini’’ anasema Daines.
Anasema kwa sasa wajawazito kumi wanaofika kujifungua katika vituo vya afya au hospitalini, kati yao wawili hugundulika kuwa na upungufu wa damu na kutakiwa kuongezewa damu.
Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Rainer Kapinga anakiri kuwa kuna tatizo la upatikanaji wa damu salama wilayani humo na anazo taarifa za baadhi ya watumishi kuhusika kuuza damu kwa wagonjwa na tayari watumishi watatu wamewajibishwa kutokana na kushirki kuuza damu.
‘’Utaratibu wa halmashauri tunanunua vifaa vyotte vya kutolea damu na kuwekea lakini binadamu wana mambo yao hasa watu wa maabara na tayari watu watatu wamewajibishwa kutokana na suala hilo’’ anasema Dr. Kapinga.
Anaeleza ukubwa wa tatizo hilo la upungufu wa damu wilayani humo kuwa asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa damu kutokana na ukanda huo kuwa ni ukanda wa Maralia.
‘’Asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa na damu kutokana na ukanda huu kuwa wa Maralia na mtu anapokuwa mjamzito kinga zake hupungua’’ anasema Dr. Kapinga.
Katika wilaya mpya ya Butiama mkoani Mara, nako tatizo la damu ni kubwa ambapo kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya Butiama Dr. Joseph Musagafa anasema kuwa vifo vingi hasa watoto chini ya miaka mitano wanakufa kutokana na ukosefu wa damu.
Anasema kuwa hospitali hiyo wamejipanga kutoka na kwenda kuzungumza na jamii kuhusu umuhimu wa kuwawahisha wajawazito na watoto hospitalini wanapoona wanaumwa.
‘’Vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano vinatokea kwa kukosa damu na kuwachelewesha kufika nao hospitali’’ anasema Dr.Musagafa.
Anaeleza sababu zingine zinazosababisha mpaka hali hiyo ya ukosefu wa damu hasa wa watoto chini ya miaka mitano kuwa ni pamoja na baadhi ya wazazi wakiona watoto wao wanaumwa wanawanunulia dawa kwenye maduka ya dawa muhimu za binadamu wengine kuamini kuwa watoto wao wamelongwa hivyo kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji.
‘’Wengine wanapenda kuwaleta watoto wao mapema lakini wanakosa usafiri wa kuwafikisha mapema na baadhi hawana uchumi mzuri wa kuwawezesha kufika hospitali na kumudu gharama’’ anasema Dr. Musagafa.
Kwa upande wa wanawake anasema kuwa wengi wao wanajifungulia majumbani kutokana na sababu mbalimbali kama alizozitaja hapo juu ikiwemo sababu ya usafiri na miundombinu huku akitolea mfano maeneo ya Bugoji, Majile na Bulangi ambayo yapo umbali wa kilometa 100 ili kufikia hospitali hiyo.
Kuhusu uuzwaji wa damu anasema kuwa hawana damu kabisa hivyo wanalazimika kuchukua kwa ndugu wa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo na bada ya kuchukua damu hiyo wanapima VVU na Kaswende kisha kumuongezea mgonjwa.
Anakiri kuwa ubora wa damu hiyo wanakuwa hawana uhakika zaidi bali wanachoangalia ni kuokoa maisha ya mgonjwa ambaye huchangia Sh.3000 kwa ajili ya chupa ya kutunzia ambapo anasema wanalazimika kuwatoza wagonjwa au ndugu zao fedha hiyo ili kuchangia gharama ya vifaa hivyo.
‘’Tunatoza fedha hiyo ili kununulia begi za kuhifadhia damu hiyo na hali hii tunalazimika kutokana na kutovipata kutoka MSD’’ anasema mganga huyo huku akiwaambia wauguzi wamtundikia haraka damu Remmy Wambura mama aliyefika hospitalini hapo baada ya kujifungua salama nyumbani uzao wake wa saba na kuvuja damu nyingi kisha kukosa nguvu.
Hospitali hiyo ya butiama ndiyo hospitali inayotibu hata familia ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo Dr. Peter Mwera anasema kuwa kila siku ya Alhamisi endapo Mama Maria Nyerere akiwemo kijijini hapo wanakwenda kumfanyia uchungui wa afya yake.
Dr. Mwera anasema kuwa ni zaidi ya awamu mbili ameenda kumfanyia uchunguzi wa afya ya Mama Maria Nyerere na kwamba kuna awamu aliwaambia kuwa anawachosha hivyo atalazimika yeye mwenyewe kwenda katika hospitali hiyo ili kufanya uchunguzi wa afya yake lakini bado hajafanya hivyo.
Naye mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Mara Dr. Iragi Ngerageza anasema tatizo la damu salama ni kubwa katika hospitali hiyo na mkoa kwa ujumla ambapo wanalazimika kukusanya damu kutoka kwa wagonjwa.
Anasema ili kupata vipimo wanapeleka mkoani Mwanza ambako ndiko kuna vipimo sahihi vya kuthibitisha kuwa damu hiyo ni salama au iharibiwe ambapo kwa hospitali ya Mara hutumia Sh. 120,000 kwa ajili ya kulipa kwenye basi kupeleka damu hiyo na watumishi wanaopeleka na kurudi na damu na kwa wiki anasema damu inapelekwa mara nne.
Wanalazimika kusafirisha damu hiyo kwa kutumia mabasi ili kupunguza gharama ambapo anasema kuwa wakitumia gari ya serikali inatumia lita 90 za mafuta kwenda tu na wanalazimika kuwalipa dereva na mhudumu wa afya anayepaswa kukabidhi damu hiyo katika benki ya damu, hivyo wanapunguza matumizi hayo kwa kusafirisha na mabasi ya abiria na kumlipa mtumishi mmoja tu.
‘’Kuna hatari nyingi hivyo naweza kushauri kuwa serikali ipeleke vifaa vya kupimia damu kila mkoa bada ya kuwa kwenye makao makuu ya kanda ambapo unaposafirisha damu hiyo inaweza kujitokeza hitilafu kisha damu hiyo ikamwagika au kumwagikia watu ndani ya basi hivyo mtu anayesafirisha kuwa katika hatari ya kumdhuru’’ anasema Dr. Ngerageza.
Anasema matumizi ya damu ni makubwa ambapo watoto chini ya miaka mitano, majeruhi na wajawazito kwa siku wanatumia zaidi ya unit 8 mpaka 10.
Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa upungufu huo wa damu unaosababisha vifo vingi vya wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, imeelezwa kwamba baadhi wanakufa kutokana na imani za dini zao zinazokataza kuongezewa damu kwa madai kuwa sawa na kuchukua kiungo cha binadamu mwingine.
Mwandishi wa makala anapatikana kwa simu 0754 440749. Barua pepe;[email protected] WEB; www.kalulunga.blogspot.com