Wanaopata huduma za kliniki Bunda, wanajifungulia kwa wakunga wa jadi

Frank Leonard

ASILIMIA 32 ya wajawazito wanaopata huduma za kliniki katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma wilayani Bunda, mkoani Mara hujifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi.

Muuguzi Mkuu wa wilaya hiyo, Aderaid Masige alizitaja baadhi ya sababu zinazochangia hali hiyo kuwa ni pamoja na umbali wa vituo hivyo na uhaba wa wafanyakazi wenye stadi na weledi wa kuhudumia wajawazito.

Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aderaid Masige
Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aderaid Masige

Zingine ni tatizo la miundombinu ya majengo, uchache wa vifaa na dawa na tabia za wafanyakazi wakati wakiwapokea wajawazito na wanapowapa maelekezo.

“Sababu zote hizo zinasababisha wajifungulie majumbani, kwa ndugu na jamaa na kwa wakunga wa jadi wanaotambuliwa kama wasaidizi wa huduma za ukunga,” alisema.

Masige alisema pamoja na serikali kuwazuia wakunga wa jadi kuzalisha, wananchi wanawaamini na wanaendelea kuwatumia.

“Katika wilaya yetu hii, mimba ya kwanza hadi ya nne, wajawazito wengi hujifungulia kwa wakunga wa jadi na baada ya hapo huenda katika vituo rasmi vya kutolea huduma kama zahanati, vituo vya afya na hospitali,” alisema.

Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Rainer Kapinga alisema wilaya hiyo ina vijiji 106 na kila kijiji kina wakunga wa jadi wawili wanaotambuliwa.

Pamoja na kutambuliwa, Dk Kapinga alisema hawatakiwi kuzalisha na badala yake wanatakiwa kuwaelimisha na kuwasindikiza wajawazito katika vituo vya kutolea huduma.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Rainer Kapinga
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Rainer Kapinga

Kuhusu tabia za wafanyakazi alisema, kuna idadi kubwa ya watumishi wanaolalamikiwa kuwa na lugha mbaya kwa wajawazito na wagonjwa wengine.

Juu ya vifaa tiba na dawa alisema hakuna kituo hata kimoja kinachapata kulingana na mahitaji yake na akakosoa mgao wa dawa kwamba hauendani na hali halisi ikiwa ni pamoja na ongezeko la watu.

“Mfumo wa mgao wa dawa na vifaatiba unaotumika ni wa mwaka 2003 kwa zahanati na vituo vya afya, huku hospitali zikipata kulingana idadi ya vitanda,” alisema.

Katika ufafanuzi wake alisema, tangu wakati huo zahanati zimeendelea kupata Sh 390,000 kwa mwezi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa huku vituo vya afya vikipata Sh 800,000 kwa mahitaji yake.

“Wakati huo kopo moja la quinine lilikuwa linauzwa Sh 10,000 lakini hivi sasa linauzwa Sh 80,000,” alisema.

Kuhusu miundombinu ya majengo na watumishi wenye sifa, Dk Kapinga alisema “uboreshaji wa majengo hufanywa kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa serikali na michango ya wananchi na kwa upande wa watumishi, wilaya ina upungufu wa asilimia 61 ya watumishi wenye sifa.”

Mkunga wa Jadi wa Kijiji cha Kambubu wilayani Bunda, Veronica John (62)
Mkunga wa Jadi wa Kijiji cha Kambubu wilayani Bunda, Veronica John (62)

Alisema utafiti wa ndani ya nchi unaweza kusaidia kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoikabili sekta ya afya.

“Serikali iangalie mazingira ya vijijini, watumishi wa huko waendelezwe kitaaluma na wapewe motisha. Nguvu iongezwe katika usambazaji wa vifaa tiba na dawa; miundombinu, mfumo wa rufaa na watumishi wenye sifa ni muhimu kuangaliwa kwa mapana yake katika ngazi zote,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *