Mwitongo kitovu cha utalii kinachohitaji kuwekwa sawa

Eva-Sweet Musiba

Pamoja na kuwepo kwa mbuga ya wanyama ya Serengeti iliyoko Mkoa wa Mara na vivutio vingine kuna baadhi ya vivutio ambavyo havitambuliwi kitaifa ambavyo vinaweza kukuza utalii wa ndani katika Mkoa wa huu.

Nimekutana na Mtoto wa Baba wa Taifa  ambaye ni wa sita kuzaliwa katika familia ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Madaraka Nyerere ambaye anatanabahisha juu ya vivutio vya Mkoa zaidi ya kivutio kikubwa kinachojulikana ambacho ni mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Anasema kuwa kuna maajabu mengi katika Mkoa huu ambayo hayajatambuliwa na mengi yako katika kijiji cha Mwitongo,Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara ndani na nje ya nyumba ya Baba wa Taifa ambayo inahitaji kufanyiwa utafiti wa kina.

Alisema kuwa ndani na nje ya nyumba hiyo kuna michoro ya kale ambayo inakadiriwa kuwa na umri wa miaka 20,000 lakini bado inahitaji kufanyiwa utafiti na watafiti wa mambo ya kale, idara ya historia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuona michoro hiyo ilikuwa ya nini na ilikuwa na maana gani.

Katika mahojiano alisema sasa ni miaka miwili tangu wataalamu hao kusema watafika katika eneo hilo kufanya utafiti na bado hakuna wataalamu waliofika hapo.

Ukiangalia kwa mbali katika jiwe kubwa lililoegemea nyumba hiyo utaweza kuona mnyama kama Twiga, na mchoro mwingine kama vile jua lakini inahitaji utafiti wa kina,michoro iliyoko ndani ya nyumba ya Baba wa Taifa ambayo pia iko kwenye jiwe kubwa ilifutwa na wajenzi wakidhani kuwa ni uchafu,lakini Baba wa Taifa aliwakataza, yenyewe inaonekana kwa mbali lakini inaweza kutambuliwa pale tu watafiti watakapofika kufanya utafiti wao.

Madaraka aliongeza kuwa michoro hiyo ina rangi nyekundu,pia katika msitu wa Muhunda ulioko Mwitongo inasemekana pia kuna unyayo wa mtu wa kale, lakini hauonekani vizuri,yote hayo ni kupoteza dhamani ya vitu tulivyonavyo ambavyo vingetunzwa, kufanyiwa utafiti,kulindwa na kuthaminiwa vingeweza kuutangaza Mkoa huu pia kitaifa na kimataifa vyema hatimaye kukuza pato.

Msitu wa Muhunda  ndio msitu wa kabila la wazanaki waliokuwa wakifanyia matambiko na sasa bado wanafanya matambiko,na inaaminika kuwa mzimu (Msambwa) ukitokea  wazee wa kizanaki (wanyikura) wanakusanyika kuelezea tukio linakuwa na maana gani pale anapotokea mnyama kama chui,mbuzi mkubwa mweupe ama nyani mkubwa.

Alisema hasa hasa nyani mkubwa akitokea wazee hao watakaa na kujadili akiwemo mtabiri ambaye anaelezea kutakuwa na tukio gani katika kipindi hicho,ama mvua yenye madhara, njaa kali na mengineyo mengi yenye madhara ama neema.

Katika msitu huo haruhusiwi mtu yeyote kwenda humo, ila wazee wa kizanaki pekee,ambapo katika familia ya hayati Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere wazee hao walimteua mtoto wa Baba wa Taifa ambaye ndiye pekee anaweza kuingia humo, Madaraka Nyerere (53) na si wengine.

Wanawake wanaruhusiwa kwenda kuokota kuni ndani ya msitu huo lakini si kukata.

Kabla ya mauti kumkuta Mwalimu Nyerere aliweka uzio katika eneo hilo ili kukinga watu wasiingie. Kwa bahati  mbaya ndani  ya msitu huo wa Muhunda kulikuwa na na jiwe kubwa ambalo lilikuwa limekaa mithili ya kiti lakini liliporomoka, Jiwe hili lilifanana na lile la Bismark Rocky ndani ya ziwa Victoria.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *