Waziri Nagu ashangazwa na umasikini wa Watanzania

Jamii Africa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu akihutubia mkutano wa Makatibu Muhtasi nchini (TAPSEA), leo jijini Mwanza.

Dk. Mary Nagu

Waziri Nagu akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Welle Ndikilo (kulia), baada ya kufungua mkutano wa TAPSEA leo jijini Mwanza. (Picha zote na Sitta Tumma).

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu Ameeleza kushangazwa kwake na hali mbaya ya umasikini unaowakumba Watanzania, huku taifa lao likiwa imejaa rasilimali nyingi zisizo na kifani.

Amesema, Tanzania ni nchi tajiri sana wa rasilimali, lakini wananchi wake bado wanakabiliwa na tatizo la umasikini, jambo ambalo alisema upo umuhimu zaidi wa uwezeshwaji wa wananchi, ili kuondoa tatizo hilo la umasikini katika ngazi ya kaya, mkoa hadi taifa.

Waziri Nagu ameyasema hayo leo Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili la Chama cha Makatibu Muhtasi wa umma na sekta binafsi Tanzania (TAPSEA), uliofanyika Malaika Hoteli jijini hapa.

“Nchi yetu hii imejawa na utajiri mkubwa sana, lakini bado umasikini nao umekithiri kwa Watanzania. Hivyo uwezeshwaji wa wananchi lazima uwepo”, alisema Waziri Nagu.

Hata hivyo, alikwenda mbali zaidi na kuwaonya Watanzania kwamba, wasibweteke na hali waliyo nayo sasa, bali wachangamkie fursa zilizopo nchini za uwekezaji, ili wasije wakabaki watazamaji tu katika sekta hiyo muhimu na mkombozi mkubwa wa umasikini.

Katika hatua nyingine, aliwataka Makatibu hao Muhtasi nchini kuhakikisha wanafanyakazi zao kwa ufanisi na umakini wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kujenga ushirikiano mzuri kati ya mwajiri, jamii na watumishi wengine.

“Kumbukeni ya kwamba, ninyi makatibu muhtasi ni chombo muhimu sana katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Bila ninyi Waziri, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine hawawezi kufanyakazi zao vizuri. Jengeeni ushirikiano thabiti na imara”, alisema.

Hata hivyo, Waziri Nagu alijikuta akilazimika kuzungumzia vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa yanayolinyemelea taifa kwa sasa, ambapo alisema: “Kwa sasa vuguvugu la mabadiliko limezidi kukolea hapa nchini. Mabadiliko haya yasichochee vurugu bali yawe ya amani”.

Aidha, Dk. Nagu alieleza kukerwa na namna makatibu muhtasi wanavyofanyishwa kazi kwa kufananishwa na jiko la kupikia jinsi lisivyothaminiwa, lakini kila mtu anahitaji ale na kushiba kupitia jiko hilo hilo.

Alisema, dunia ya leo bado inatawaliwa na mfumo dume unaokandamiza na kuminya haki za wanawake, hivyo kwa vile kazi ya ukatibu muhtasi hapa nchini inafanywa na wanawake wengi zaidi, wapambane na kutokomeza mfumo huo dume, na watetee haki zao za kujiendeleza kielimu zaidi ili siku moja wapate nafasi ya juu kama alivyo yeye (Waziri Nagu).

“Msije mkadhani najigamba, majigambo siyo huruka yangu. Mimi nimewahi kufanyakazi nikiwa ofisa wa chini sana kiwandani, lakini baadaye nikawa General Manager (Meneja mkuu), wa kiwanda nikiwa mwanamke miaka ya 86.

“Kwa maana hiyo, nawaombeni sana mjiendeleze kielimu mpate hadi masters ya ukatibu muhtasi na baadaye mje muwe mabosi na mhudumiwe kama mnavyowahudumia mabosi wenu ofisini”, alisema Waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji nchini.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

10 Comments
  • Mambo ya aibu! Wanaimaliza nchi then wana sema hawajui kwanini tuko maskini?kuna siku wataelewa watakapokuwa hawapo tena huko waliko

    • ajabu na aibu kubwa yeye niwaziri wa uwekezaji na uwezeshaji bado anawasimanga wasio ndani ya mfumo wa ulaji bila kuonyesha nini amewawezesha wakashindwa kuendeleza na kuzalisha.ama hi inathibitisha hajui yuko wapi na kwa nin?icheo bila wajibu ni HATARI.

  • heh!!! anaposhangaa anawashangaza wengine!

    kifikra pevu KUSHANGAA,, lina maana ni kitu kipya hujawahi hata kufikiria kama kitaweza kutokea kwa wakati huo, ulitarajia vingine na imetokea tofauti aidha zaidi au chini ya matarajio!!! sasa waziri (Mh.) anaposhangaa, anatushangza zaidi sisii maana hatukutaraji kama angeweza kusema hayo! anaomba kura kutatua kero za wananchi na kubwa ni umaskini leo anaushangaa!! na bado raisi anamuangalia tuu kama mshauri wake!

    Sitamani kuzungumzia u meneja wake kwa kampuni isiyokuwa na mafanikio! asishangae, umaskini unaletwa na wao viongozi wa nchi

  • Ndugu,Mtanzania,Mzalendo mwezangu.Dunia ya leo inaelekea pagumu kisiasa na kiuchumi kwahiyo tuelimishane zaidi kuliko kulaumiana.Wewe ungukuwa katika kiti waziri Dr.Nagu ungesema vipi tofauti naye alipokuwa akihutubia pale mwanza.Kuna msemo unaosema usimpe mtu samaki bali mfundishe kuvua.Kwahiyo rejea hutoba yake kwa undani uta mwelewa vizuri.Hongera Dr.Nagu waamshe walio lala.

  • UMASKINI WA WATANZANIA UNATOKANA NA UONGOZI MBOVUUUUU!!!!!!! hakuna kiongozi atakayesema hilo maana linamgusa? Ona hapa; WATU tunao, AARDHI tunayo yakutosha, SIASA SAFI tena sana hata mataifa mengine wanaiigiza kwetu, UONGOZI BORA? mmhh???? NDIO MAANA VIONGOZI BADALA YA KUBAINISHA ARDHI ILIYO WAZI NA KUWAPA WANACHI HUSUSAN VIJANA AMBAO WANATEGEMEA WAGAWIWE ARDHI NA WAZAZI WAO, wanaita wagenii… TATIZOO NI UONGOZI UONGOZI!!

  • aendelee kushangaa hivyo hivyo kama boss wake ambaye hajui kwa nini watanzania ni maskini!!!!!!!!!!!

  • Mimi sikujua mwaizi akiiba akala akashiba mwisho wake ni kututapikia miguuni mwetu. Hivyo uwaziri alivyoupata siyew tunajua na hakuna sifa ya maana aliyoionyesha zaidi ile ya kitandani…huo ni mshahara wa ngono na kama mfumo dume ndiyo tatizo mbona kitanda kinmemlipa……tatizo ni kuwa vyote hivyo vinapita………

  • Kwanza kabisa nampongeza mheshimiwa wziri Nagu kama waziri mwanamke shupavu aliyefanya kazi tangu utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Ruksa Mwinyi, Benjamini Mkapa na sasa Raisi Jakaya Mrisho Kikwete.

    Hongrea sana mama endelea kuwa mwadilifu kwa kuongoza watanzania na kulinda mali za umma.

    Mbali na hongera hizo taifa hili limeingia kwenye matatizo mengi kama ulivyosema mwenyewe hasa umaskini tatizo ambalo umekiri mwenyewe kuwa nchi yetu ni tajiri sana kwa raslimali lakini unashangaa kwa vipi umaskini hauondoki

    Mheshimiwa waziri ni majuzi tuu uliona baadhi ya wabunge wa upinzani na hata wa chama tawala walianza kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu kisa taarifa ya mkaguzi mkuu na wizi wa matrilion ya shs

    Matokeo yake Mheshimiwa Raisi akaokoa jahazi na kuwaacha baadhi ya mawazori na manaibu waziri waliotajwa kwenye taarifa hizo,

    Mheshimiwa waziri kwavile umeshakuwa waziri siku nyingi najua fika kuwa unafahamu nini maana ya wizi na namna wizi unavyotokea kwenye wizara sina haja ya kusema

    Naomba nitoe mfano mwananchi anataka kiwanja kwa ajili ya kujenga na afanye biashara watendaji waliochini yako wanashindwa kumpa kiwanja hicho kwa wakati na kudai rushwa hadi fedha alizopewa kwenye kustaafu zinaisha je umaskini utaisha

    Mwanafunzi anachaguliwa kwenda chuo kikuu anaambiwa alipe fedha za pango kama tshs 1 mill atarudishiwa mkopo utakapo patikana ukipatikana mkopo shule inakataa kurudisha fedha hizo ambazo mzazi alizikopo na sasa anabakiwa na deni kubwa hilo umaskini utaisha

    Kiwanda kinafunguliwa kwa ajili ya kusindika korosho na menejiment inatoka ulaya waokota kokoto ni wahamiaji haramu wa mataifa mengine ambao wengi sasa wamejaa kariakoo na watoto wetu hawana kazi je huu umaskini utaishaje

    Serekali inajitahidi kutafuta wawekezajiwamepata gesi huko Songosongo ya miaka 120 na huko Mtwara ya kuweza kutumika kwa karibu karne kadhaa

    Serekali hiyo badala ya kujenga mitambo mikubwa ya megawats 500 na kuendelea kwenye mikoa ya ya mtwara Lindi, songea na Mbeya kwa ajili ya kutatua kabisa tatizo la umeme na kuanzisha viwanda vidogo vodogo kwa bei ya kuondoa umaskini gesi hiyo inapimwa na kijiko ili watu waendelee kuuza majenereta yao umaskini utakushaje waziri

    Makaa ya mawe ya Ludewa mwekezaji amesema anaweza kuzalisha mega 600 kwa kuanzia na chuma cha liganga kingeweza kuchimbwa tungejenga madaraja mengi kuliko marekani sasa wewe kama waziri wa uwekezaji hilo nalo hulioni umaskini utakwisha kweli

    Mkaa ya mawe ya Kiwira mmeuza kwa mwekezaji binafsi anadai kila mwezi kulipwa overhead cost za mamilioni ya tshs wakati kiwanda alinunua kwa bei ya kutupa na baya zaidi malalamiko ya wafanyakazi hayaishi je umaskini utaisha

    Mbuga za wanyama tuanzie na pale kwenye bustabi ya ya viwanja vya bunge nikikumbuka wale tausi swala, pumda na wanyama wenginae waliokuwepo pale sasa sijui wamekwenda wapi wametolewa zawadi au wameizwa? Je watalii waliokuwa wanakuja na kuleta fedha za kigeni kuona bustani hizo na wanyama hao je watalii hao si wameishia na fedha zao za kuondoa umasikini

    Vivutio vingi vya utalii hamtaki kuvitangaza nje ya nchi ona hata mlima mrefu barani Afrika unajulikana upo nchi jirani watalii wanakuja kuanzia safari kwao umaskini utaondoka

    Sasa hivi serekali imeanza kuwapa wawekezaji mashamba makubwa ya kulima badala ya kuwataka wawekeze sambamba na wananchi kesho wataanzisha sheria ya no Trace passing na ole mtanzania atakapokanyaka kwenye eneo lililonunuliwa na mwekezaji ni kupigwa risasi tu kama tunavyoona kwenye machimbo ya dhahabu wanainchi wanakuwa watumwa kwenye nchi yao wenyewe

    Badilisheni sera za uwekezaji mapema kabla jua halijachwa, kama makaburu kipindi kile cha ubaguzi wa rangi waliweza kuja Mwadui na kuchukua dhahabu zao na nchi ilikuwa haiwatambui lakini kwa vile sheria ilishasainiwa hatukuwa na namna tuliishia kusema mdomoni tu

    Kuna mengi sana sikuweza kuyaeleza hapa ambayo ni kero kubwa kwa Mtanzania

    Nimeanza kwa kukusifu najua unaweza ni mwanamke shupavu ongea kwenye baraza la mawaziri kataa ufisadi na ukionyesha mwelekeo mwema na watanzania wenzangu na mimi nitakuunga mkono ukigombea Uraisi 2015

    Mungu ibariki Tanzania

  • Ama kweli,ujumbe wa Waziri huyu ni shubiri nyingine,binafsi nayapokea masimango haya ya waziri kwa moyo mkuu,kwa maana ya kutufundisha na kutuamsha Watanzania, na pengine si mlaumu Waziri, tunapaswa kuwalaumu wapiga kura wake, kwa kumruhusu kuwa mbunge wao kwa miaka mingi, na sasa kaneemeka ,kwani naamini nao, wapo hoi bin taabani.Kipimo kikubwa kwa waziri ni kwa wapiga kura wake . Jee amewawezesha kwa kiasi gani, kutumia fursa hizo alizo zisema ,ukilinganisha na umri wake katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri tokea miaka hiyo ?Chama kimekua na viongozi wa ajabu sana ,ambao siku zote wamekua wakitumia nafasi za kujineemesha wenyewe ,na kulindana na inapofikia hatua ya kuwajibishana hapo ndipo upilato unapofanyika .Sahihi ya Waziri huyu haikua miongoni mwa zile sahihi sabini, hili ni la uhakika. Jee, watanzania ni lini wamewezeshwa hata tu kutambua hizo fursa?Hebu jiulize , elimu inayotolewa mashuleni,vyuo vikuu,maeneo ya kazi,katika jamii,inawafanya wananchi hawa waweze kutambua fursa hizo? kwanini fursa hizo zisianze kuandaliwa tokea shule za msingi ,ili mtoto akue akiwa na muelekeo wa nini cha kufanya ukubwani ?jee ,sio, kwamba wananchi wanaandaliwa kuwa watwana wa familia za hawa waungwana na watoto wao?Ni mara ngapi watoto wetu wamekumbana na virungu na mibomu ya machozi ya Polisi pale wanapolilia haki ya kielimu .Mimi naamini kuzitambua fursa hizo na kuzitumia kisawasawa huanza kwanza kwa kuondoa upofu wa ubongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *