Wajasiriamali, benki watofautiana mikopo ya uwekezaji

Jamii Africa

Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji wa sekta ya fedha ili kuongeza wigo wa uzalishaji, biashara na uwekezaji wa mitaji utakaochochea ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) katika ripoti yake ya  April 2018 juu ya utendaji wa sekta ya fedha nchini, imeeleza kuwa Tanzania haifanyi vizuri katika upatikanaji wa mikopo  ya uwekezaji wa mitaji na biashara ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Kutokana na mbadiliko katika sekta ya fedha yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Magufuli, biashara nyingi zimefungwa na uzalishaji wa bidhaa za viwandani umepungua kwasababu ya ongezeko la kodi na masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo katika benki za biashara.

“Tanzania iko nyuma sana ukilinganisha na nchi zingine katika upatikanaji wa mikopo, hasa mikopo ya muda mrefu. Ukosefu wa mikopo ya kuwekeza kwenye mitaji ya kudumu kunazuia kukua kwa uzalishaji”, imeeleza ripoti hiyo.

Wanaoathirika zaidi ni wafanyabiashara wadogowajasiriamali ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea mikopo ya benki kuendesha biashara zao. Hata mikopo inayopatikana kwenye benki huambatana na riba kubwa ambayo wengi wanashindwa kulipa, jambo linalozorotesha ukuaji wa biashara na mzunguko wa fedha nchini.

 “Wajasiriamali wadogo na wa kati hawahudumiwi vizuri, na kuzuiwa kutenengeneza ajira. Mahitaji makubwa ya riba yana matokeo hasi kwa wajasiriamali ambao hawana mitaji mikubwa hasa wanawake. Kadharika vikwazo vya upatikanaji, kuna gharama kubwa za mikopo na masharti ambayo sio rafiki kwa uwekezaji”, imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

 Kutokana na mabadiliko makubwa yenye matokeo hasi kwenye sekta ya fedha hasa uendeshaji wa benki, idadi ya wafanyabiashara na wajasiriamali ambao wanapata mikopo imepungua. “Matokeo yake, asilimia 13 tu ya wajasiriamali wadogo wanaotambulika (rasmi) ndio wanaopata mikopo ya benki”.

 Mkurugenzi Mkazi wa WB katika nchi za Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia, Bella Bird amesema Tanzania inapaswa kujitathmini juu ya mwenendo wa sekta ya fedha na kuhakikisha inarekebisha mapungufu yanayojitokeza kwenye utendaji wa benki na utolewaji wa mikopo ya uwekezaji na biashara.

“Uchambuzi wa ripoti unaonyesha Tanzania inatakiwa kupiga hatua zaidi ili kuboresha uwezo wake wa upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu ili kuinua uchumi. Riba za mikopo bado ziko juu na upatikanaji wa mikopo nao sio wa kuridhisha na matokeo yake ni kupungua kwa wastani mikopo inayopelekwa kwenye sekta binafsi”, amesema Bella Bird.

Kupungua kwa mikopo na ongezeko la riba  kunatokana na gharama kubwa za uendashaji benki nchini ambazo zimechagizwa na ongezeko la kodi na kupungua kwa mitaji ya uwekezaji baada ya serikali kuamua kutunza fedha zake kwenye Benki Kuu ya Tanzania na kuachana benki za biashara ambazo zilikuwa zinatumia amana ya serikali katika shughuli mbalimbali za uwekezaji na biashara.

Amebainisha kuwa njia ya haraka kwa benki kujikwamua na anguko la kibiashara ni kuwekeza katika biashara ya mtandao (mobile money) ambayo ni rahisi kupata wateja wengi watakaofanya miamala popote walipo. Suala hilo litaongeza mzunguko wa fedha.

Miaka nane iliyopita, ufanisi wa miamala ya fedha kwa njia ya mtandao wa simu umeongezeka ambapo mpaka sasa asilimia 60 ya watanzania wameunganishwa na huduma hiyo ukilinganisha na asilimia 11  ya mwaka 2006.

Hata hivyo, serikali imeshauriwa kutengeneza mikakati itakayowahusisha wanawake na vijana zaidi katika sekta ya fedha kwa kuwapatia elimu ya fedha, biashara na kuanzisha miradi itakayosaidia kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Pia kutengeneza mazingira wezeshi kwa benki kufanya shughuli zao kwa uhuru na kutegeneza mwongozo wa kuwalinda watumiaji wa huduma za kibenki dhidi ya mabadiliko ya kifedha ambayo yanaweza kuhatarisha biashara na mitaji yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *