CCM Mwanza watafunana, walia na Mwenyekiti wa Misungwi

Sitta Tumma

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mwanza, kimesisitiza kuwa msimamo wake wa kumtaka mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani hapa, Benald Polcarp kujivua ‘gamba’ ipo pale pale, na kwamba tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazomkabili ni nzito, hivyo chama hakiwezi kulegeza msimamo wake huo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Clement Mabina na Katibu wa CCM Mkoa Joyce Masunga.

Kauli hiyo imetolewa leo na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Clement Mabina wakati alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, na kusema mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi, ni lazima awajibike kwa kuachia nafasi yake hiyo aliyopewa na madiwani kwa dhamana ya chama.

Polcarp anadaiwa kutajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa matumizi mabaya ya madaraka yake, ikiwa ni pamoja na kujipatia tenda za ujenzi ndani ya halmashauri hiyo kupitia kampuni yake, kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Akifafanua kuhusu tuhuma hizo, mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza, Mabina alisema maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya siasa ya wilaya ya Misungwi kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo ajivue ‘gamba’ kutokana na tuhuma nzito zinazomkabili, hayana lelemama wala mjadala, bali lazima yatekelezwe kwa vitendo.

“Maamuzi ya chama yapo pale pale kuhusu Polcarp kujivua gamba. Hatuwezi kufanya kazi na watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi. CCM mkoa kinaunga mkono uamuzi wa kamati ya siasa ya chama wilaya ya Misungwi kutaka huyu mtu aachie ngazi.

“Hakuna ubishi katika hili maana ripoti ya CAG inamtaja kapewa pesa milioni 440 kujenga kibanio cha josho moja huko Misungwi kupitia kampuni yake ya ujenzi. Kuna milioni 80 nyingine tena zimetajwa na CAG kapewa kujenga mradi”, alisema mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza, Mabina.

Aidha, aliongeza kusema kwamba: “Kwanza kanuni na sheria zinakataza diwani, mwenyekiti au mtumishi wa halmashauri kupewa tenda ndani ya halmashauri. Sasa yeye aliwezaje kuomba na kupewa tenda ndani ya halmashauri wakati akitambua kwamba hilo ni kosa kisheria?. Chama hatulegezi msimamo wetu, aondoke tu”.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mwanza, alikwenda mbali zaidi na kumtuhumu Polcarp kwa madai kwamba ameanza kushawishi madiwani kwa kuwapa kitu kidogo ili wamuunge mkono kwa lengo la kutaka kuzima tuhuma hizo nzito zinazomkabili.

Alisema, kamwe chama hicho tawala hakiwezi kuwafumbia macho watu wa aina hiyo wanaoonekana kutumia vibaya madaraka na rasilimali za nchi, na alimtaka mwenyekiti huyo wa halmashauri ya Misungwi, Polcarp atekeleze kwa vitendo maamuzi ya chama yaliyotolewa dhidi yake, na wala asipoteze muda wake kutafuta huruma pembeni, kwani hiyo haitamsaidia ng’o.

Kwa upande wake, mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi, Polcarp alipotakiwa na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia msimamo huo wa chama juu ya tuhuma zinazomkabili, aliushangaa uongozi wa chama chake kumng’ang’anie aachie nafasi yake, na kuhoji kwamba kama kweli tuhuma hizo ni za kweli kwa nini hajafikishwa mahakamani?.

Alisema, kwanza tuhuma anazohusishwa nazo hazifahamu kwani hajaiona hata hiyo ripoti ya CAG, na kwamba anachoamini ni kwamba kuna mkakati wa muda mrefu wa kummaliza kisiasa unaofanywa na baadhi ya watu wilayani humo, hivyo ni vema chama kikaacha kuingilia mambo kama hayo kwani yeye hana hatia yoyote.

“Kwanza mimi sijaiona hiyo ripoti ya CAG yenye tuhuma zangu. Lakini nashangaa chama kuning’ang’ania…maana huu ni mkakati unaofanywa ili kunimaliza kisiasa. Kwani wewe mwandishi umeiona hiyo ripoti ya CAG na tuhuma zangu unisaidie?”, alihoji mwenyekiti Polcarp huku akivilaumu vyombo vya habari kwa madai kwamba vinapotosha ukweli wa mambo.

Kumekuwepo na tuhuma nzito za ufisadi zinazoikabili halmashauri hiyo, ambapo mei 9 mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kuagiza kushushwa cheo na kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Misungwi, Exavier Tilweselekwa, kutokana na tuhuma hizo za ufisadi wa mamilioni ya fedha za miradi mbali mbali ya maendeleo.

Tayari kuna taarifa zinazodai kwamba agizo hilo la Waziri Mkuu lilishatekelezwa kwa Mkurugenzi huyo kushushwa cheo, lakini inadaiwa hadi sasa bado hajafikishwa mahakamani kama ilivyoagizwa na Pinda.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.

3 Comments
  • nabado kwawni lazima tuwazike siku c nying walizoea mno hata kam aawan njama za kuua watashindwa tu

  • Na bodo nendeni na manispaa ya SUMBAWANGA mkaaibike. Mnaombea kura barara moja tu isiojengwa toka uhuru, Wafipa tumeaka, its time for change.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *